Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Mashirika ya haki za binadamu yalaani hukumu ya Tundu Lissu

Shirika la Amnesty International limesema hukumu hiyo ni matokeo ya mchakato uliokosa haki tangu mwanzo.

Muhtasari

  • ACT Wazalendo wakosoa hukumu ya LISSU, wasema ni pigo kwa demokrasia
  • Karua, Bobi Wine na Maraga wamtetea Lissu baada ya hukumu ya miaka minne
  • Mashirika ya haki za binadamu yalaani hukumu ya Tundu Lissu

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. ACT Wazalendo wakosoa hukumu ya LISSU, wasema ni pigo kwa demokrasia

    Viongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo wamekosoa vikali hukumu iliyotolewa dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, wakieleza kuwa uamuzi huo ni siku ya giza kwa demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.

    Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, wameeleza wasiwasi wao kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu kumtia hatiani Lissu kwa kosa la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela, baada ya kumuondolea shtaka la uhaini.

    Katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, Semu alisema hukumu hiyo inaleta maswali mazito kuhusu hali ya demokrasia na ulinzi wa haki za msingi nchini Tanzania.

    Alisisitiza kuwa msimamo wa ACT Wazalendo kuhusu kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa Lissu haujabadilika, akidai kuwa kesi hiyo ina misingi ya kisiasa na inalenga kunyamazisha sauti za upinzani pamoja na kuzuia uhuru wa shughuli za kisiasa.

    Semu alieleza kuwa chama chake kinaona hukumu hiyo kama jambo linalotia wasiwasi kuhusu mustakabali wa demokrasia na utawala wa sheria nchini.

    Aidha, alieleza mshikamano wa chama hicho kwa Lissu, familia yake na wanachama wa CHADEMA, huku akiahidi kuwa ACT Wazalendo itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kudai haki na kuhimiza kuachiliwa kwake.

    Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, aliukosoa uamuzi huo wa mahakama, akieleza kuwa ni siku ya giza kwa utawala bora na utawala wa sheria nchini Tanzania.

    Kauli ya Shaibu inaongeza uzito katika msimamo wa chama hicho kuhusu hukumu ya Lissu, huku ikionyesha wasiwasi wake kuhusu athari zinazoweza kujitokeza katika misingi ya haki, uhuru wa kisiasa na uendeshaji wa shughuli za kidemokrasia.

    Awali, Lissu alikuwa akikabiliwa na shtaka la uhaini, lakini Mahakama Kuu ilimkuta na hatia ya kosa mbadala la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.

    Mahakama ilieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa ulihusisha matamshi ya Lissu ya kuwataka wananchi kuzuia na kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuhitimisha kuwa yalifikia kiwango cha uchochezi.

    Hata hivyo, Lissu amepinga hukumu hiyo, akiieleza kesi yake kuwa na misingi ya kisiasa. Timu yake ya mawakili pia imetangaza nia ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo na kuomba dhamana wakati rufaa ikiendelea.

    Kauli za viongozi hao wa ACT Wazalendo zinaongeza mjadala kuhusu uhuru wa kisiasa, uhuru wa kujieleza, haki za binadamu na nafasi ya taasisi za mahakama katika kulinda misingi ya demokrasia nchini Tanzania.

    ACT Wazalendo imesisitiza kuwa itaendelea kudai haki kwa Lissu, ikieleza kuwa tofauti za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kupitia misingi ya kidemokrasia, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria.

  2. Karua, Bobi Wine na Maraga wamtetea Lissu baada ya hukumu ya miaka minne

    Viongozi kadhaa wa kisiasa na wanaharakati kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wamekosoa hukumu ya kifungo cha miaka minne jela dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kumwondolea shtaka la uhaini lakini kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.

    Kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) nchini Kenya, Martha Karua, alitaka Lissu aachiliwe huru mara moja, akisema kufutwa kwa shtaka la uhaini kunathibitisha kuwa hakukuwa na msingi wa kumshikilia gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja. Karua alieleza kuwa hukumu ya uchochezi na kifungo cha miaka minne ni ukiukwaji wa haki na inaibua maswali kuhusu mwenendo wa kesi hiyo.

    Karua pia alisema kuwa kesi dhidi ya Lissu inapaswa kutazamwa katika muktadha mpana wa kisiasa nchini Tanzania, hususan baada ya CHADEMA kuzuiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Alionya dhidi ya matumizi ya mashitaka ya jinai kama njia ya kudhoofisha wapinzani wa kisiasa na kupunguza ushindani wa kidemokrasia.

    Kwa upande wake, kiongozi wa Linda Mwananchi Movement (LMM) na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, alikaribisha uamuzi wa mahakama wa kumuondolea Lissu shtaka la uhaini, akisema hakupaswa kushtakiwa kwa kosa hilo tangu mwanzo. Sifuna alidai kuwa kosa pekee la Lissu lilikuwa kudai mageuzi katika mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi wa haki na wa uwazi.

    Naye kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, alisema kuondolewa kwa shtaka la uhaini ni ushindi dhidi ya kile alichokiita matumizi ya mfumo wa dola kutishia wapinzani wa kisiasa. Hata hivyo, alikosoa hukumu ya uchochezi, akidai kuwa shtaka hilo lilitumika kumweka Lissu gerezani kwa kuendelea kuitetea ajenda yake ya "No Reforms, No Election".

    Bobi Wine alisema hukumu hiyo inaonesha namna mifumo ya mahakama inaweza kutumiwa kuwanyamazisha viongozi wa upinzani wanaodai mageuzi ya kidemokrasia.

    Wakati huo huo, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, alikosoa mwenendo wa kesi hiyo akisema mashitaka ya uhaini dhidi ya Lissu hayakuwa na msingi wa kisheria. Maraga alisisitiza kuwa wito wa mageuzi ya kikatiba, mikutano ya amani na kususia uchaguzi haupaswi kutafsiriwa kama uhaini.

    Aidha, mwanasheria na mwanaharakati wa Kenya Miguna Miguna alijiunga na viongozi wengine wa kikanda kulaani hukumu hiyo, akisema kutiwa hatiani kwa Lissu licha ya kuondolewa shtaka la uhaini kunazua maswali kuhusu haki na uhuru wa kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

    Viongozi hao kwa pamoja wametoa wito wa kuheshimiwa kwa haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na ushindani wa kidemokrasia nchini Tanzania.

    Soma Zaidi:

  3. Mashirika ya haki za binadamu yalaani hukumu ya Tundu Lissu

    Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu yamekosoa hukumu ya kifungo cha miaka minne jela dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, baada ya Mahakama Kuu kumkuta na hatia ya kosa la uchochezi huku ikimuondolea shtaka la uhaini.

    Shirika la Amnesty International limesema hukumu hiyo ni matokeo ya mchakato uliokosa haki tangu mwanzo. Mkurugenzi wake wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah, alisema Lissu hakupaswa kukamatwa, kushtakiwa wala kutiwa hatiani.

    Kwa mujibu wa Amnesty, Lissu ametumia siku 577 akiwa mahabusu kutokana na kile shirika hilo linachodai kuwa matumizi ya haki zake za msingi kwa njia ya amani. Shirika hilo pia lilidai kuwa alinyimwa fursa ya kuwasiliana kwa siri na mawakili wake, jambo lililomlazimu kujitetea mwenyewe mahakamani.

    Amnesty ilidai pia kuwa matangazo ya moja kwa moja ya mwenendo wa kesi yalikatizwa, huku baadhi ya waangalizi wa kimataifa wa kesi hiyo wakikamatwa na baadaye kufukuzwa nchini. Aidha, ilisema Lissu alizuiliwa katika mazingira yasiyofaa na kuitaka Tanzania kufuta hukumu hiyo, kumuachilia huru bila masharti na kuheshimu haki za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

    Kwa upande wake, Human Rights Watch (HRW) ilisema hukumu hiyo ni ishara ya kile ilichokiita ukandamizaji unaoendelea dhidi ya wapinzani wa kisiasa nchini Tanzania. Shirika hilo lilibainisha kuwa kesi ya Lissu ilizua wasiwasi wa haki za binadamu kutokana na ucheleweshaji wa mara kwa mara wa shauri hilo pamoja na madai kwamba alizuiwa kuwasiliana kwa faragha na mawakili wake.

    HRW ilizitaka mamlaka za Tanzania kuacha kutumia mfumo wa haki ya jinai dhidi ya wapinzani wa kisiasa na badala yake kuheshimu haki za kisiasa na uhuru wa kujieleza.

    Nalo Pan-African Solidarity Network (PASNet) limetaka kuachiliwa kwa Lissu mara moja na bila masharti, likisema hukumu hiyo imeibua maswali kuhusu haki ya usikilizwaji wa kesi na uhuru wa mahakama nchini Tanzania.

    PASNet ilidai kuwa Lissu alitiwa hatiani kwa kosa ambalo hakushtakiwa moja kwa moja nalo na kwamba hakupata fursa ya kutosha kujitetea. Shirika hilo pia lilieleza wasiwasi kuhusu afya yake, upatikanaji wa matibabu maalumu na athari za kuendelea kushikiliwa kwake kwa familia yake.

    Aidha, PASNet imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuunda tume huru ya kimataifa kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kutokea baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025.

    Mashirika hayo kwa pamoja yameitaka Tanzania kuheshimu haki za msingi za kisiasa na kuhakikisha mfumo wa sheria hautumiki kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali na viongozi wa upinzani.

    Soma Zaidi Hapa:

  4. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara mimi ni Asha Juma.