Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ndani ya magenge ya dawa za kulevya yanayotumia watoto kuua
- Author, James Waterhouse
- Nafasi, Correspondant à Paris
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 10
Tahadhari: Maudhui haya yana lugha chafu na maelezo ya ukatili wa kingono.
Mwaka 2022, mwanamke mmoja jijini Marseille nchini Ufaransa aliamua kuwasiliana na polisi baada ya kununua bangi kutoka kwa kijana aliyekuwa akiuza dawa za kulevya.
Lakini kilichomfanya achukue hatua hiyo hakikuwa bangi aliyokuwa amenunua, bali ujumbe aliokabidhiwa na kijana huyo.
Ujumbe huo ulisema:
"Tunazuiliwa kinyume na matakwa yetu na tunahitaji msaada. Tuna umri wa miaka 15."
Katika kesi iliyosikilizwa katika mahakama ya Ufaransa mapema mwaka huu, ilibainika kuwa kijana huyo alikuwa mmoja wa wavulana wawili waliokuwa wakishikiliwa na genge la wahalifu. Awali, wote wawili walikuwa wamejiunga na genge hilo wakitafuta kazi ya kulipwa, ingawa ilikuwa shughuli haramu.
Mmoja wa wavulana hao alikuwa na jukumu la kusimamia fedha, huku mwingine akizunguka mitaa ya eneo la Frais-Vallon. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, viongozi wao waliwatuhumu kwa kusababisha upungufu wa mapato ya genge hilo.
Mahakama ilielezwa kuwa wavulana hao walianza kupigwa mara kwa mara. Pia walilazimishwa kucheza wakiwa uchi mbele ya kamera ili kurekodiwa na kutumiwa kuwatishia. Mmoja wao alibakwa.
Saa chache baada ya mwanamke huyo kupokea ujumbe huo, vijana hao wawili walijaribu kutoroka kupitia dirisha la ghorofa ya pili na kujeruhiwa. Mmoja alifanikiwa kutoroka, lakini mwenzake alikamatwa, akapigwa na kuchomwa kisu. Hata hivyo, alinusurika.
Polisi walifanya operesheni na kuwakamata washukiwa. Picha zilizopatikana katika simu ya mmoja wa watu wanaotuhumiwa kuwatesa vijana hao zilionyesha wanaume wengine kadhaa wakiwa katika hali kama hiyo ya dhiki. Baadaye, wanaume sita walihukumiwa vifungo virefu gerezani kwa kuwatesa vijana hao wawili.
Kisa cha wavulana hao kinaonyesha jinsi magenge ya dawa za kulevya yalivyoteka baadhi ya maeneo ya jiji la Marseille, ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini Ufaransa.
Mchanganyiko wa utamaduni wa Mediterania, sanaa za mijini na muziki wa hip hop umeifanya Marseille kuwa kivutio maarufu cha watalii. Hata hivyo, hali ni tofauti kabisa katika maeneo yaliyo nje ya katikati ya jiji.
Baada ya miezi kadhaa ya juhudi, timu ya BBC ilifanikiwa kuingia katika ulimwengu huo hatari, unaojikita katika mitaa yenye umaskini na makazi makubwa ya nyumba za kijamii katika jiji hilo la bandari, ambako hata polisi huingia kwa tahadhari kubwa.
Tulibaini kuwa magenge hayo yasiyo na huruma huwavutia vijana walio katika mazingira magumu kwa kuwaahidi kupata fedha kwa urahisi, lakini huishia kuwanasa katika ulimwengu wa biashara ya dawa za kulevya, ukatili na unyonyaji.
Tulichunguza jinsi magenge hayo yanavyotumia mitandao ya kijamii kuajiri watu wa kutekeleza mauaji ya kukodiwa na kuzungumza na vijana kadhaa walionaswa katika mzunguko wa ghasia.
Akiwa gerezani, mwanachama mmoja wa genge anayetuhumiwa kuhusika na mauaji kadhaa alieleza jinsi utulivu wake ulivyomwezesha kupanda vyeo ndani ya genge hilo.
Genge lenye nguvu zaidi jijini humo, linalojulikana kama DZ Mafia, lilishinda vita vya umwagaji damu vilivyohusisha mapambano ya kugombea maeneo ya ushawishi. Sasa ni miongoni mwa mashirika ya kihalifu yanayoogopwa zaidi nchini Ufaransa.
Herufi DZ ni msimbo rasmi wa intaneti wa nchi ya Algeria. Mmoja wa waanzilishi wa genge hilo, Mehdi Laribi, ambaye ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria, alikamatwa nchini Algeria mapema mwaka huu kwa mujibu wa hati ya kukamatwa iliyotolewa na Ufaransa.
Genge hilo lilipata umaarufu mkubwa mwaka 2023, lilipokuwa la kwanza nchini Ufaransa kutumia umaarufu wake kwa kuchapisha video za kutoa taarifa na kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii kama chapa. Hayo yanaelezwa na Dimitri Zoulas, mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya nchini humo.
Taarifa yake ya mwisho ilitolewa mwezi Julai, wakati meya wa mji jirani alipowekwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya taarifa za kiintelijensia kuonyesha kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kutokana na uwezekano wa kushambuliwa na genge hilo.
Katika video iliyochapishwa mtandaoni, wanaume sita waliovaa nguo nyeusi na kufunika nyuso zao walionekana wakiwa wamesimama nyuma ya meza. Mmoja wao alisoma taarifa iliyokanusha kuhusika kwa DZ Mafia katika tukio hilo.
Ukuaji wa soko haramu la dawa za kulevya nchini Ufaransa pia umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa nguvu za genge hilo. Soko hilo limeshuhudia ongezeko kubwa la uingizaji wa kokeini, pamoja na biashara kubwa ya bangi na dawa za kulevya zinazotengenezwa kwa kemikali.
Kwa mujibu wa Zoulas, idadi ya watumiaji wa kokeini nchini Ufaransa inatarajiwa kufikia watu milioni mbili hivi karibuni, ikilinganishwa na 600,000 mwaka 2017.
Anaongeza kuwa biashara ya dawa za kulevya nchini humo huzalisha mapato ya euro bilioni saba kwa mwaka na kuwahusisha watu 200,000.
Watoto wengi wanahusika katika biashara hiyo, huku mamlaka zikishuhudia ongezeko la idadi ya walio chini ya umri wa utu uzima wanaojihusisha nayo. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa mwaka 2024, karibu watoto 10,000 walihusika kwa namna moja au nyingine katika biashara hiyo.
DZ Mafia ni mfano wa wazi wa hali hiyo. Ili kuwafikia wateja wengi zaidi, genge hilo linahitaji wanachama zaidi, wakiwemo watoto.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa sasa genge hilo linawaajiri vijana katika maeneo mbalimbali ya Ufaransa, si kwa ajili ya kuuza dawa za kulevya pekee, bali pia kutekeleza utekaji nyara, vitendo vya mateso na mauaji.
Vijana hao wanaonekana na viongozi wa magenge kuwa kizazi ambacho ni rahisi kushawishiwa kuingia katika uhalifu, lakini pia ni rahisi kutupwa wanapokuwa hawana tena manufaa. Viongozi hao mara nyingi huendelea kuwasimamia wakiwa gerezani au nje ya nchi.
Polisi na majaji wanaonya kuwa mara tu watoto hao wanapoingia katika mazingira ya uhalifu wa mitaa ya Marseille, huwa vigumu sana kuwaondoa.
Gharama ya kibinadamu ya biashara hiyo
Watu wachache wanafahamu madhara ya magenge ya Marseille kwa maisha ya watu kama Karine Brouillard, mama anayeishi upande mwingine wa Ufaransa, mbali sana na pwani ya Mediterania.
Mwanawe, Hugo, alitoroka nyumbani kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 15, baada ya kutofautiana na familia yake. Alikuwa akiishi katika kijiji kaskazini mwa Ufaransa. Siku tatu baadaye, polisi walimkamata jijini Marseille, umbali wa karibu kilomita 1,000 kutoka nyumbani kwao. Alikutwa akiwa na fedha na bangi, kisha akarudishwa nyumbani.
Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, mwaka 2023, Hugo alipanga kurejea kusini mwa nchi hiyo. Aliwaambia wazazi wake kuwa alikuwa amepata kazi ya muda katika mgahawa mmoja karibu na Marseille.
Karine anakumbuka:
"Alikuwa akinijulisha mara kwa mara kuhusu hali yake. Alikuwa akinipigia simu na kusema kila kitu kilikuwa sawa."
Wiki tatu baadaye, daktari alimpigia simu. Karine anasema hataisahau kamwe taarifa aliyopewa:
"Mwanao amefikishwa hapa jana usiku. Amepigwa risasi kichwani."
Polisi wanaamini kuwa Hugo alipelekwa kupata matibabu kutoka eneo linalodhibitiwa na genge la wahalifu. Pia wanashuku kuwa alikuwa na uhusiano na mojawapo ya magenge hayo.
Eneo hilo lilijulikana kama Northern Quarter.
Kuingia katika eneo linalodhibitiwa na DZ Mafia
Njia bora ya kuingia katika eneo la Northern Quarter, ambako DZ Mafia inaendesha shughuli zake, ni kupitia kwa Fadella Ouidef, mkazi wa eneo hilo mwenye umri wa miaka 41 na mama wa watoto wanne. Alikubali kutuongoza.
Sekunde 37 tu baada ya kuingia katika makazi hayo, tulijikuta tumekwama.
Magari yalipiga honi huku gari aina ya Peugeot alilokuwa akiendesha Fadella likipita katika kizuizi cha barabarani kilichokuwa kinasimamiwa na wanachama wa genge hilo. Vijana waliokuwa katika kizuizi hicho walitambua mara moja kamera yetu.
"Subiri, acha kurekodi," Fadella alituonya, wakati gari aina ya SUV la rangi ya kijivu lilipotuzuia na kutulazimisha kusimama.
"Naandaa ripoti kwa ajili ya taasisi inayosimamia makazi yetu ya kijamii," alimweleza dereva aliyekuwa na shauku ya kujua kilichokuwa kikiendelea.
Hatimaye, dereva huyo alikubali tuendelee na safari yetu kwa sharti la kusitisha upigaji picha.
Ilikuwa hali ya kutia wasiwasi kuona gari lisilohusiana na polisi likifanya kazi kwa kujiamini kiasi hicho. Tulipumua kwa afueni lilipoondoka.
Fadella anaeleza: "Hivi karibuni, magenge yamekuwa na ukatili mkubwa. Tunachojaribu kufanya ni kuwafanya vijana wetu waelewe kuwa kinachoendelea si sahihi."
Kauli yake inaakisi hofu inayowakabili familia nyingi katika eneo hilo, kwamba watoto wao wanaweza kushawishiwa kwa kuahidiwa kiasi kikubwa cha fedha na kuishia kujiingiza katika uhalifu unaowanyang'anya maisha yao ya kawaida ya ujana.
Ahadi za magari, nyumba na fedha
Ahadi za fedha ndizo zilizomshawishi kijana mmoja kutumia sehemu kubwa ya ujana wake akiwa ndani ya DZ Mafia.
Ili kuwawezesha watu tuliowahoji kuzungumza kwa uhuru na kulinda usalama wao, tulikubali kutofichua utambulisho wao.
Kijana huyo, anayetumia jina la Camil, anasema alipanda vyeo ndani ya genge hilo hadi kufikia nafasi ya mkuu wa usalama katika eneo lililokuwa chini ya udhibiti wake.
Kwa sasa ana umri wa miaka 20 na anadai kuwa amejiondoa katika genge hilo. Hata hivyo, alikuwa na mashaka kuhusu uwepo wetu kabla ya kukubali kueleza jinsi genge hilo linavyowavutia na kuwaajiri vijana wapya.
"Wanajua namna ya kukushawishi. Wanakupa kila kitu unachotaka," anasema.
Anaeleza kuwa vitu hivyo vinaweza kuwa magari mazuri, nyumba kubwa, dawa za kulevya na makahaba.
"Tunahisi kuwa na uaminifu kwao kutokana na wanachotupatia. Tunaendelea kuwa nao hadi mwisho, ama kifo au gereza."
Camil pia anaeleza jinsi genge hilo linavyotumia udhaifu wa mwanachama mpya kumdhibiti.
"Wakigundua udhaifu wako, watautumia. Utakuwa mtumishi wao tu, hakuna zaidi."
Mwanachama mwingine wa DZ Mafia, ambaye jina lake halisi halijatajwa na anayetumia jina la Adam, alituambia kupitia mazungumzo ya video kwenye Snapchat kuwa alikuwa sehemu ya kikosi cha genge hilo kilichohusika na kutekeleza mauaji ya kukodiwa.
Kwa sasa yuko gerezani akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake baada ya kuhusishwa na mauaji kadhaa.
Adam anaeleza: "Watu walitambua uthubutu wangu na utulivu wangu. Bila hata kukusudia, nilipanda vyeo ndani ya genge hilo. Hatimaye, lilikuwa sehemu yangu na ilinibidi kuzoea maisha hayo."
Katika mazungumzo hayo, anakiri kuwa mauaji anayohusishwa nayo ni matukio ya kutisha.
"Mashambulizi yaweza kutekelezwa mchana kweupe, hata katika foleni za magari. Vitendo hivyo vinaweza kuanzia kumpiga mtu kofi hadi kumchukua mbele ya mama yake na kumchoma akiwa hai ndani ya gari. Nafikiri mimi huwa mtulivu na ninaweza kukabiliana na hali hiyo vizuri."
Tulimuuliza Adam iwapo hujisikia kujutia anapotekeleza vitendo hivyo vya ukatili.
Alisema:
"Kwa kiasi fulani najihisi na hatia," lakini akadai kuwa hana majuto.
"Kama nisingefanya yote hayo, wengine wangefanya badala yangu. Mimi ni kama tofali moja tu katika ukuta mkubwa."
Kama vijana wengine wengi jijini Marseille, Adam alifahamu kuwa biashara ya dawa za kulevya inaweza kumpatia mtu fedha nyingi kwa muda mfupi. Hata hivyo, sasa akiwa katika miaka ya ishirini, anakiri kuwa mazingira aliyokuwa akiishi yalikuwa mtego.
Katika makazi moja ya kijamii yaliyojitenga na yanayodhibitiwa na DZ Mafia, kuna kituo cha kuuzia dawa za kulevya ambacho kinapaswa kuwa eneo salama kwa wateja. Hata hivyo, bei za kokeini, hashish na bangi zimeandikwa kwa michoro kwenye ukuta.
Eneo hilo limekuwa kama ngome ya asili kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Kwa kuwa kuna barabara moja kuu ya kuingia na kutoka, wanaweza kudhibiti mwendo wa wateja na kufuatilia polisi wanapokaribia.
Katika maeneo hayo, si jambo la kushangaza kusikia milio ya risasi za bunduki za kivita wakati wa usiku.
Baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo, msimamizi wa kituo cha mauzo cha genge hasimu alikubali kukutana nasi katika eneo lake la kazi.
Maisha katika maeneo yanayotawaliwa na magenge
Tuliingia katika makazi hayo mapema asubuhi. Sauti za ndege wakiimba na watoto wakielekea shuleni zilikuwa tofauti kabisa na shughuli kubwa ya uhalifu iliyokuwa ikiendelea katika eneo hilo.
Mwanaume huyo, anayetumia jina la Joe, anasema alikuwa akipata euro 3,000 kwa mwezi akiwa na umri wa miaka 13. Kwa sasa anadai kuwa mapato yake yameongezeka hadi kati ya euro 5,000 na 10,000 kwa mwezi.
Anaonekana kuamini kuwa maisha aliyochagua yalikuwa sehemu ya hatima yake, licha ya kuwa yanamletea fedha nyingi.
Tulipomuuliza iwapo huwaza kuhusu watu waliopoteza maisha kutokana na ghasia zinazotekelezwa na genge lake, Joe, ambaye ana umri wa miaka 23, alionekana kuwa tayari amekubaliana na maumivu na uharibifu unaosababishwa na biashara ya dawa za kulevya.
"Biashara hii inaharibu maisha ya watu, lakini kila mtu hufanya maamuzi yake mwenyewe," alisema huku akitikisa mabega.
Kwa mujibu wa Zoulas kutoka kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, shughuli za genge la Joe pamoja na DZ Mafia zinatishia usalama wa taifa.
Anasema biashara hiyo inachangia ajali za barabarani, ukatili wa majumbani, msongo wa mawazo, kujiua na vifo vinavyotokana na matumizi ya dawa za kulevya kupita kiasi, ambavyo huzidi 700 kila mwaka. Pia, shughuli hizo huvuruga uchumi.
Anaonya:
"Tunaelekea katika hali ambayo inaweza kusababisha mfumo wa haki jinai kushindwa kufanya kazi ipasavyo."
Mitandao ya kijamii yageuka kuwa chombo cha kuajiri wauaji
Polisi wamefanikiwa kupata ushindi kadhaa dhidi ya magenge ya biashara ya dawa za kulevya jijini Marseille na katika miji mingine. Operesheni za kihalifu zimezuiwa, idadi ya viongozi wa magenge wanaokamatwa imeongezeka na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kimekamatwa.
Kwa mujibu wa polisi, tangu mwaka 2024, takriban watu 1,000 wanaohusishwa na DZ Mafia wamekamatwa na 600 kati yao wamefungwa gerezani.
Hata hivyo, kwa ujumla, mapambano dhidi ya magenge hayo yanazidi kuwa magumu.
Magenge hayo yanapotafuta kupanua shughuli zao au kujaza nafasi za wanachama waliokamatwa au kuuawa, mitandao ya kijamii imekuwa nyenzo muhimu ya kuajiri vijana. Hali hiyo imeongezeka zaidi tangu janga la Covid, wakati biashara nyingi za dawa za kulevya mitaani zilipoanza kuhamia kwenye mitandao ya kijamii.
Katika mitandao hiyo, tulibaini matangazo mengi ya nafasi za kazi jijini Marseille kwa ajili ya madereva, wasafirishaji na watu wanaotaka kuwa wauaji wa kukodiwa. Baadhi ya matangazo hayo yaliambatana na picha zilizotengenezwa kwa teknolojia ya akili unde na kuonyesha maisha ya kifahari.
Magenge hayo pia yamepanua wigo wa kuwatafuta wanachama wapya, hasa kwa kuwa inazidi kuwa vigumu kuwashawishi vijana wa maeneo yao baada ya wengi wao kufahamu hatari zinazohusiana na biashara hiyo.
Kwa mujibu wa polisi, matangazo hayo yanaweza kuwafikia vijana katika maeneo mengi ya Ufaransa, yakiwemo Paris, Nantes na Lille, na kuwavutia kujiunga na magenge ya Marseille na eneo la Northern Quarter.
Kwa mujibu wa vyombo vya usalama, matangazo ya mtandaoni yamebadilisha pia aina ya vijana wanaovutiwa kujiunga na magenge hayo.
Mara nyingi ni vijana ambao hawajawahi kuwa na rekodi za uhalifu, lakini wana udhaifu ambao magenge yanaweza kuutumia kuwashawishi, kama vile kukulia katika mazingira magumu ya kifamilia.
Mapambano dhidi ya magenge yazidi kuwa magumu
Thibaut Fontaine, mkuu wa kitengo cha Ufaransa kinachopambana na uhalifu uliopangwa, anaeleza:
"Watu hawa huajiriwa na wafadhili wasio na maadili ambao baadaye huwapeleka katika mazingira hatari."
Kwa mujibu wake, kutokuwa na uzoefu wa awali katika uhalifu kunawafanya vijana hao kuwa rahisi kukamatwa na polisi kwa muda mfupi.
Karine bado hajafahamu sababu iliyosababisha mwanawe Hugo kupigwa risasi na kuuawa.
Alipoulizwa angewaambia nini viongozi wa magenge wanaowashawishi watoto na vijana kujiunga na uhalifu jijini Marseille, alisema:
"Wanaharibu familia. Dada wadogo, kaka wadogo, babu na bibi. Lakini nafikiri watu hawa hawana moyo wa huruma kabisa."
Mgahawa ambao Hugo aliwaambia wazazi wake kuwa angefanya kazi ulikuwepo kweli. Hata hivyo, wafanyakazi wa mgahawa huo walimweleza Karine kuwa hawakuwahi kumwajiri mtu yeyote kwa jina la Hugo.
Inaaminika kuwa chanzo cha kifo chake kinahusishwa na eneo la Northern Quarter jijini Marseille.
Ripoti za ziada za Marianne Baisnee, Lea Guedj na Paul Pradier