Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Edda Sanga: "Baada ya kupokea cheti kutoka kwa Baba Mtakatifu, niko tayari kuondoka duniani"
- Author, Martha Saranga
- Nafasi, BBC SWAHILI
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
"Miaka 50 ya ndoa haikuwa rahisi. Kulikuwa na nyakati za kulia na kucheka, changamoto na mafanikio. Lakini kwa kujitolea na kushikamana, yote tuliyapitia pamoja na kuyashinda," anasema Mama Edda Sanga kwa sauti iliyojaa bashasha.
Akiwa na umri wa miaka 79, Edda Sanga aliyetoa mchango mkubwa katika historia ya uandishi wa habari Tanzania anajivunia kupokea cheti cha pongezi 2024 kutoka Vatican kwa aliyekuwa kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis.
'Kuna zawadi kubwa kuliko hiyo? Namimi nilisema ingekuwa kuna namna ya kumuomba Mungu kwamba baada ya kupata hiki cheti sasa baba niko tayari kuondoka katika dunia hii,nimemaliza kazi yangu'
'Maisha ya watu wawili hayawezi kuwa a bed of roses' alisisitiza Edda Sanga kuwa maisha ya ndoa sio raha mustarehe tu.
Unajua mume wangu alikuwa hataki,akaniuliza kwanini unataka kuuambia ulimwengu kuhusu ndoa yako?
Anasema kwake hatua hiyo ilikuwa ni ya muhimu na ya kumshukuru Mungu kwa kumfanikisha kwakuwa si wengi huweza.
Kinyume na matarajio ya baadhi ya watu kwamba ndoa ni maisha ya furaha yasiyo na misukosuko, Mama Edda anaamini mafanikio ya safari hiyo yanajengwa na uvumilivu. "Wanasema marriage is not a bed of roses, lakini ukweli ni kwamba maisha ya ndoa yana kupanda na kushuka. Hakuna mteremko wa moja kwa moja," anafafanua.
Mapambano ya kumkomboa mwanamke yamekuwa nongwa?
Mama Edda Sanga ambaye ni mama wa watoto wanne na wajukuu wawili alisema jamii kuendelea kushuhudia vitendo vya ukatili miongoni mwa wanandoa ni jambo linalompa maswali mengi.
Anahoji kazi zote ambazo harakati za waandishi wa habari wanawake tulizofanya hazikusaidia au watu wameamua kutokaa kimya na taarifa za kuumiza?
Je ni simu,maendeleo mitandao au wanawake tuliowapigania wasome sasa wamesoma na kudai haki zao imekuwa nongwa? alijiuliza mama Edda.
Hatuwezi kuendelea kuficha masuala ya ukatili ndani ya ndoa kwa kudai kuwa ni mambo ya watu wawili.
'Kazi ya kufanya bado ipo' vyombo vya habari na jamii ifanyie kazi jambo hili'alisisitiza.
Ninajivunia kushiriki katika harakati za kumkomboa mwanamke na ninakiri zilifanikiwa, lakini bado kuna kazi ya kufanya hasa kwa upande wa mtoto wa kiume.
'Ningependa kufanya kazi zama hizi za AI'
Unajua kwenye umri huu tunashauriwa kucheka kwa kadri tunavyoweza. Ninaweza kukaa mwenyewe nikiangalia Tiktok ninacheka sana vitu vya kuchekesha na maarifa mengi sana kupitia mtandao huu wa kijamii.
Mbali ya mitandao ya kijamii ningependa sana kufanya kazi katika zama hizi za akili mnemba.
'Kusema ukweli katika zama hizi mna mambo mengi ya kuwawezesha waandishi wa habari kufanya kazi ya kusifika'.
Hii akili mnemba inamsaada mkubwa sana kwa taaluma hii lakini ni muhimu sana kuwa waangalifu ili kuhakikisha kila mnachokipata na kukitumia kutokana na hiyo teknolojia ni sahihi.
Waandishi wa habari wanatakiwa kuhakikisha wanatumia kwa usahihi ili kuendelea kulinda imani ya uandishi wa habari.
Anaenda mbali na kusema ni kama mitandao ya kijamii sasa hivi inavyoweza kusambaza taarifa nyingi kwa muda mfupi lakini je ni sahihi? anauliza
Mama Edda Sanga anaamini kwamba uandishi wa habari usiokuwa wa kuaminika ni sawa na kupoteza kila kitu.
Aidha amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuzingatia maadili ili kujiepusha kupotosha jamii.
'Ninatazama hadi leo hii jina langu bado linasifika kwa kufanya kazi zilizosifika'
Mama Edda anasema kizazi cha sasa kipatiwe elimu itakayokisaidia kujitambua,ili kutafuta maarifa na taarifa ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi.
Wanawake wasirizike na urembo tu bali watafute maarifa yatakayowasaidia katika ulimwengu huu unaopiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Mama Edda hakuwaacha kando wanaume, amewaasa kujiona kuwa wajenzi wa taifa hili.
'Wanaume wasitafute tu kuwa active sexually na kuwa wavivu..kwa sababu tunasikia malalamiko kwamba baadhi ya wanaume ni wavivu, hawachangamkii fursa ya upatikanaji wa taarifa nyingi kufanya mambo yenye tija kwa jamii'.