Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
2026 yatikisa Dunia: Washuhudia Joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa
Wanasayansi wameiambia BBC kwamba dunia iko mbioni kurekodi mwaka wenye joto la juu zaidi kuwahi kushuhudiwa, huku sayari ikikabiliwa kwa wakati mmoja na athari za ongezeko la joto duniani linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na hali ya El Niño.
Onyo hilo linatolewa wakati viongozi wa dunia na wajadiliani wamekuwa wakikutana nchini Uturuki tangu Jumatatu kwa ufunguzi wa COP31, mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Berkeley Earth, taasisi huru ya utafiti ya Marekani iliyotoa makadirio hayo, imesema kuwa huku zikiwa zimesalia miezi miwili kabla ya mwaka kuhitimishwa, ina uhakika wa asilimia 95 kwamba mwaka 2026 utavunja rekodi ya awali iliyowekwa mwaka 2024.
Nchi zinazoshiriki mkutano huo zimehisi kwa karibu athari za ongezeko la joto katika miezi ya hivi karibuni: kuanzia moto mkubwa wa misitu ulioenea kote Ulaya hadi kuporomoka kwa ghafla kwa barafu kubwa (glacier) nchini Nepal, tukio lililosababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja.
"Tumeshuhudia miaka miwili mfululizo iliyovunja rekodi za joto," anasema Robert Rudd wa taasisi ya Berkeley Earth. "Kadiri ongezeko la joto duniani linavyoendelea kuongezeka, tunatarajia hali kama hiyo kuendelea..."
Ijumaa, Kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi cha cha Umoja wa Ulaya kilisema kwamba Oktoba ulikuwa mwezi wenye joto la juu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Hata hivyo, Bw. Rudd alionya kuwa huu ni mwanzo tu wa mabadiliko yanayotarajiwa kutokea.
"Huenda tukashuhudia mabadiliko makubwa zaidi na yenye athari kubwa zaidi katika siku zijazo," alisema.
Sababu kuu ya ongezeko la joto duniani imekuwa kuongezeka kwa kiwango cha dioksidi kaboni (CO₂) katika angahewa, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linatokana na uchomaji wa nishati za visukuku kama mafuta, gesi asilia na makaa ya mawe.
Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani (WMO) la Umoja wa Mataifa lilitoa ripoti yake, likitabiri kwa tahadhari zaidi kuliko Taasisi ya Berkeley Earth kwamba mwaka 2026 utakuwa miongoni mwa miaka minne yenye joto la kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Shirika hilo linasema mwaka 2027 huenda ukawa na hali kama hiyo, kwani El Niño yenye nguvu isiyo ya kawaida itaendelea hadi mwaka ujao na kusababisha ongezeko zaidi la viwango vya joto.
Celeste Saulo, Katibu Mkuu wa Shirika hilo la utabiri wa hali ya hewa duniani alisema hali iliyopo imevunja rekodi zote zilizowahi kuwekwa.
Matokeo hayo yanaonyesha ukubwa wa changamoto zinazowakabili wadau wa majadiliano katika mkutano wa COP31 unaofanyika katika mji wa pwani wa Antalya, Uturuki.
Katika mikutano ya awali, msisitizo ulikuwa katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi zinazochochea ongezeko la joto duniani, yaani kushughulikia chanzo cha mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, sasa idadi inayoongezeka ya nchi inakabiliwa na uhalisia kwamba zinapaswa wakati huohuo kujenga uwezo wa kukabiliana na hali mpya za hewa kali zitakazoendelea kujitokeza kadiri dunia inavyozidi kupata joto.
"Hakuna mkutano mmoja ambao ni suluhisho la kila tatizo," mkuu wa masuala ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Steele, aliwaambia wajumbe siku ya kwanza ya mkutano huo.
"Hakuna mkutano mmoja unaoweza kuziba pengo kubwa kati ya sayansi na hali halisi. Uharaka wa wakati huu unapaswa kuongoza hatua zetu. Tayari ongezeko la joto duniani linaigharimu dunia pakubwa."
Mwezi uliopita, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza alionya kwamba nchi zinapaswa kuanza kufikiria jinsi ya kukabiliana na ongezeko la majanga ya asili, ikiwemo kuweka akiba ya chakula.
Wes Streeting alitaja moto wa misitu na mawimbi ya joto kali yaliyoshuhudiwa majira ya kiangazi mwaka huu, ambayo Ofisi ya utabiri wa hali y ahewa ya Uingereza (Met Office) ilisema yalikuwa na uwezekano mkubwa mara 130 zaidi kutokea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia alizungumzia ongezeko la hatari ya mafuriko katika msimu huu wa baridi kutokana na athari za El Niño.
"Miundombinu na mifumo yetu ilibuniwa kwa ajili ya tabianchi ya karne ya 20, tabianchi ambayo haipo tena.
Hivyo, hali hii itabadilisha kila nyanja ya maisha yetu," mwanasayansi mwandamizi wa Met Office, Steven Belcher, aliiambia BBC.
Kiwango kikubwa cha gesi chafuzi kilichoongezwa katika angahewa kimezuia joto zaidi kutoka duniani, na karibu asilimia 90 ya joto hilo limefyonzwa na bahari.
Hapo ndipo nafasi ya El Niño inapokuja, anasema Bi. Saulo:
"El Niño haiongezi joto jipya duniani. Huachilia joto kutoka baharini, ambako tayari ndiko bahari yenye joto kubwa zaidi kuwahi kupimwa.
Kwa ufupi, kuna joto zaidi."
Mzunguko huo wa asili wa hali ya hewa unaendelea kusukuma viwango vya joto duniani kufikia kiwango cha juu zaidi.
COP31 inaweza kuleta maendeleo gani?
Nchi zitafanya mazungumzo kwa kipindi cha wiki mbili, huku viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, wakihudhuria mkutano huo wiki hii.
Mikutano ya awali ya kimataifa kuhusu tabianchi imewezesha kuwekwa kwa malengo mapya ya kupunguza matumizi ya nishati za visukuku, kuongeza misaada ya kifedha kwa nchi zinazoendelea na kuimarisha ulinzi wa misitu.
Ingawa uzalishaji wa gesi chafuzi unaendelea kuongezeka, nchi mbalimbali pia zimepiga hatua kubwa katika kupanua uwezo wa kuzalisha nishati jadidifu. Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) linatabiri kwamba sekta hiyo itakua kwa asilimia 57 katika kipindi cha miaka sita ijayo.
Bw. Steele pia alisema kuwa upanuzi wa matumizi ya nishati jadidifu ni suluhisho si tu kwa changamoto za tabianchi bali pia kwa changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na misukosuko ya hivi karibuni katika sekta ya nishati.
Bw. Steele pia alisema kuwa kupanua matumizi ya nishati jadidifu ni suluhisho la tabianchi na pia suluhisho la kiuchumi kwa misukosuko ya hivi karibuni katika sekta ya nishati.
"Nishati jadidifu ziliokoa takribani dola za Marekani trilioni nusu duniani kote mwaka jana."
China bado ndiyo nchi inayochangia sehemu kubwa zaidi ya ukuaji wa uwezo wa kuzalisha umeme kutoka vyanzo vya nishati jadidifu duniani.
Hata hivyo, mchango wake unatarajiwa kupungua kadiri sekta hiyo inavyopanuka katika nchi nyingine zinazoendelea.
Serikali ya Uturuki imesema inataka mazungumzo ya mwaka huu yajikite katika lengo jipya la kuharakisha mpito kuelekea matumizi makubwa ya umeme katika mifumo ya nishati.
Hii inamaanisha kuondoka katika utegemezi wa nishati za visukuku na kuelekea zaidi katika matumizi ya umeme, sambamba na kupunguza upotevu wa nishati.
Hata hivyo, mjadala huo unatarajiwa kugawa nchi katika makundi mawili yenye misimamo tofauti.
Rasimu za awali za msimamo wa Umoja wa Ulaya (EU), ambazo BBC imezishuhudia, zinaonyesha kuwa umoja huo utakubali mpito huo wa nishati ikiwa tu malengo hayo hayawezi kufikiwa kwa kutegemea gesi.
"Ni muhimu kwamba maendeleo katika mpito kuelekea matumizi ya umeme yawe yamejengwa juu ya vyanzo vya nishati safi," waraka uliotumwa kwa nchi wanachama unasema.
Lakini nchi kama Saudi Arabia na Urusi hapo awali zimekuwa zikitetea matumizi ya muda ya gesi asilia, zikiiwasilisha kama mbadala wa "nishati safi zaidi" wa mafuta ya visukuku ikilinganishwa na makaa ya mawe.
Celeste Saulo wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) amesema hawezi kueleza kwa nini nchi zimekuwa zikishindwa kufikia mwafaka kuhusu baadhi ya masuala kwa miaka mingi, lakini anaonya kuhusu matokeo yake.
"Ninachokiona ni kwamba athari za kukosekana kwa mwafaka huu zinasababisha matukio mabaya zaidi na makali zaidi," alisema.
BBC imefahamu kuwa serikali ya Uingereza inaonekana kusita kuweka malengo mapya katika COP31, ikiamini kwamba msisitizo unapaswa kuwa katika kutekeleza makubaliano yaliyopo tayari.
Hata hivyo, iliripotiwa Jumatatu kwamba malengo ya serikali ya Uingereza kuhusu matumizi ya magari ya umeme yanatarajiwa kupunguzwa, kulingana na makundi ya utetezi wa maendeleo endelevu. Hatua hiyo inaweza kuhatarisha malengo ya muda mrefu ya nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mnamo Septemba, wabunge wa kamati ya maendeleo ya kimataifa ya Bunge la Uingereza waliikosoa serikali kwa kupunguza bajeti ya misaada ya nje, hatua ambayo inaweza kuifanya ishindwe kutimiza ahadi zake za awali za ufadhili wa miradi ya tabianchi.
Katika mikutano ya awali, nchi tajiri zilikubaliana kuongeza mara tatu kiwango cha fedha za kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2035, hadi kufikia angalau dola bilioni 85 kwa mwaka.
Takwimu za hivi karibuni za mwaka 2024 zinaonyesha kuwa nchi hizo zimefikia takribani theluthi moja tu ya kiwango hicho. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa ulisema wiki hii kwamba uharibifu unaosababishwa kwa sasa na mabadiliko ya tabianchi ni "mkubwa", na kwamba huenda fedha nyingi zaidi zikahitajika.
Lakini baada ya kupanda kwa bei za mafuta na gesi kufuatia vita vya Iran na Marekani, nchi nyingi zimeelekeza sehemu ya bajeti zao za misaada katika matumizi ya ulinzi na misaada ya muda mfupi kwa kaya zinazokabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Serikali pia zinatarajiwa kutumia mkutano huo kujadili sera za kimataifa kuhusu Akili Bandia (AI), ikiwa ni pamoja na ongezeko la mahitaji ya nishati na rasilimali za maji kutoka kwa vituo vya kuhifadhi na kuchakata data (data centres) vinavyoendesha teknolojia hiyo inayozidi kuenea duniani.