Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Carrick kutimuliwa Man Utd? Hawa ndiyo wnaaotajwa kumrithi
- Author, Paul Birch
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Uongozi wa juu wa Manchester United unatarajiwa kufanya uamuzi kuhusu hatima ya kocha Michael Carrick katika kikao cha viongozi wa klabu hiyo kitakachofanyika Jumatano, Novemba 11, mjini Monaco, huku majina ya makocha kadhaa yakitajwa kuwa wagombea wa kumrithi iwapo ataondolewa madarakani.
Mkurugenzi mkuu Omar Berrada na mkurugenzi wa masuala ya soka Jason Wilcox wanatarajiwa kumshauri mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe, kuwa Carrick aondoke, baada ya timu hiyo kushinda mchezo mmoja pekee kati ya 10 ya mwanzo ya Ligi Kuu England msimu huu.
Matokeo hayo ni mabaya zaidi katika historia ya timu hiyo.
Hata hivyo, uamuzi wa mwisho bado haujafanywa. Iwapo kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 na aliyewahi kuichezea United ataondoka, atakuwa kocha wa nane wa kudumu kuiongoza klabu hiyo tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu miaka 13 iliyopita.
Idadi hiyo ya mabadiliko ya makocha itakuwa sawa na yale ambayo Manchester United imefanya katika kipindi cha miaka 68 iliyotangulia, tangu Matt Busby alipoteuliwa kuwa kocha mwaka 1945.
Manchester United inashika nafasi ya 18 katika msimamo wa ligi, ikiwa na alama moja tu zaidi ya Crystal Palace inayoshika mkia, hali inayoongeza uwezekano wa klabu hiyo kutafuta kocha mwingine.
BBC inaangazia makocha wanaotajwa kwamba wanaweza kuchukua nafasi ya Carrick iwapo ataondoka Old Trafford:
Mauricio Pochettino
Mataji makubwa aliyoshinda: Ligi Kuu Ufaransa mara moja, Kombe la Ufaransa mara moja.
Rekodi yake Ligi Kuu England: Mechi 294, ushindi 150; asilimia ya ushindi 51; wastani wa alama kwa mechi 1.77.
Pochettino alikuwa na wastani wa alama 1.89 kwa kila mechi wakati akiinoa Tottenham Hotspur, rekodi bora kuliko kocha mwingine yeyote wa klabu hiyo aliyeiongoza katika angalau mechi 25 za Ligi Kuu England.
Nia ya Manchester United ya kumtaka kocha huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 54 imekuwepo kwa muda mrefu, tangu takribani miaka 10 iliyopita.
Akiwa Tottenham, alitengeneza timu iliyokuwa miongoni mwa timu bora zaidi katika kizazi chake, ingawa hakufanikiwa kutwaa taji lolote, baada ya kupoteza fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi. Pia aliiongoza klabu hiyo kumaliza katika nafasi za pili na tatu kwenye ligi.
Alifanikiwa kutwaa mataji akiwa Paris St-Germain (PSG), ikiwemo ubingwa wa ligi, lakini kipindi chake Chelsea kilikuwa kigumu zaidi, akipoteza fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Liverpool mwaka 2024.
Baada ya kuiongoza Marekani hadi hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia lililofanyika nyumbani kwao, alisaini mkataba mpya majira ya kiangazi utakaomuweka kwenye timu hiyo hadi michuano ya mwaka 2030.
Pochettino ana kundi la wachezaji vijana wenye vipaji katika timu ya taifa, akiwemo Cavan Sullivan mwenye umri wa miaka 17, ambaye anatarajiwa kujiunga na Manchester City. Hata hivyo, kocha huyo amekuwa akieleza kuwa bado ana jambo la kukamilisha katika soka la Ligi Kuu England.
Inaripotiwa kuwa mkataba wake una kipengele kinachoruhusu kuvunjwa kwa fidia ya dola milioni 10 (pauni milioni 7.44). Pia unaelezwa kuwa na masharti yanayomruhusu kuondoka endapo atapata ofa kutoka kwa baadhi ya klabu kubwa.
Julian Nagelsmann
Mataji makubwa aliyoshinda: Ligi kuu ujerumani (Bundesliga) mara moja.
Rekodi yake Ligi Kuu England: Hana uzoefu wa kufundisha ligi hiyo.
Ni Hansi Flick pekee mwenye asilimia kubwa ya ushindi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa kocha wa Bayern Munich kuliko Nagelsmann, ambaye ana asilimia 83.3.
Nagelsmann alianza kujitengenezea jina kupitia kazi yake akiwa Hoffenheim, ambako aliteuliwa kuwa kocha akiwa na umri wa miaka 28, na kuwa kocha mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Bundesliga.
Aliibadilisha timu hiyo kutoka kwenye mapambano ya kuepuka kushuka daraja na kuifikisha katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baadaye aliiwezesha RB Leipzig kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2020, jambo lililovutia Bayern Munich na kumteua kuwa kocha wake.
Hata hivyo, licha ya kushinda taji la Bundesliga katika msimu wake wa kwanza, inaripotiwa kuwa alikumbana na tofauti za kimtazamo na baadhi ya wachezaji muhimu, hali iliyochangia kuondoka kwake kabla ya kumaliza msimu wake wa pili.
Mwaka 2023, Nagelsmann aliteuliwa kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani iliyokuwa katika kipindi cha mabadiliko. Timu hiyo ilitolewa robo fainali ya Euro 2024 na Hispania, ambayo baadaye ilitwaa ubingwa.
Alijiuzulu majira ya kiangazi baada ya Ujerumani kufungwa na Paraguay katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia.
Akiwa na umri wa miaka 39 pekee, sifa yake huenda imeathiriwa na matokeo hayo, lakini bado anatajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaoheshimika barani Ulaya.
Mkurugenzi wa usajili wa wachezaji wa Manchester United, Christopher Vivell, pia anamfahamu vizuri Nagelsmann kutokana na kufanya naye kazi pamoja RB Leipzig.
Eddie Howe
Mataji makubwa aliyoshinda: Kombe la Ligi mara moja.
Rekodi yake Ligi Kuu England: Mechi 369, ushindi 140; asilimia ya ushindi 37.9; wastani wa alama kwa mechi 1.36.
Eddie Howe ni miongoni mwa makocha watatu pekee waliofanikiwa kumfunga Mikel Arteta angalau mara tano katika mashindano yote. Wengine ni Pep Guardiola aliyemfunga mara 11 na Jurgen Klopp mara sita.
Historia ya Howe katika soka la England inajieleza yenyewe. Aliiongoza Bournemouth kupanda hadi Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo, kabla ya kuandika historia nyingine Newcastle United kwa kutwaa taji lao la kwanza kubwa la ndani tangu waliposhinda Kombe la FA mwaka 1955.
Ushindi wa Newcastle dhidi ya Liverpool katika fainali ya Kombe la Ligi ulikuwa miongoni mwa siku muhimu zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Pia aliisaidia Newcastle kumaliza katika nafasi tano za juu mara mbili, na hivyo kurejea katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.
Howe, mwenye umri wa miaka 48, aliondoka Newcastle majira ya kiangazi baada ya timu hiyo kumaliza katika nafasi ya 12 msimu uliopita, matokeo ambayo hayakukidhi matarajio.
Newcastle itataka kiasi kidogo tu cha fidia iwapo Manchester United itamshawishi Howe kujiunga nayo.
Antonio Conte
Mataji makubwa aliyoshinda: Serie A mara tano, Ligi Kuu England mara moja na Kombe la FA mara moja.
Rekodi yake Ligi Kuu England: Mechi 132, ushindi 83; asilimia ya ushindi 62.9; wastani wa alama kwa mechi 2.03.
Chelsea ilishinda mechi 30 kati ya 38 za Ligi Kuu England ilipotwaa ubingwa katika msimu wa kwanza wa Conte mwaka 2016-17.
Conte ni kocha mwenye rekodi ya kutwaa mataji mengi, hivyo uwezo wake katika benchi la ufundi hauhitaji maelezo marefu.
Aliondoka Napoli kwa uamuzi wake mwenyewe majira ya kiangazi, mwaka mmoja tu baada ya kuipa klabu hiyo ubingwa wa nne wa ligi katika historia yake.
Taji hilo liliongeza mafanikio yake mengine ya kutwaa ubingwa wa Serie A akiwa Juventus mara tatu na Inter Milan, pamoja na vipindi vyake vya kuifundisha Chelsea na Tottenham.
Conte, mwenye umri wa miaka 57, anaweza kuonekana kuwa chaguo linalowezekana kwa Manchester United kutokana na rekodi yake ya mafanikio. Hata hivyo, swali ni iwapo tabia yake ya kuwa mkali na historia ya kutofautiana na baadhi ya klabu inaweza kuwa kikwazo.
Kipindi chake cha mwisho katika soka la England kilimalizika kwa utata, baada ya kuondoka Tottenham mwaka 2023 kufuatia kuwakosoa wachezaji na utamaduni wa klabu hiyo.
Licha ya mafanikio yake Chelsea, Conte pia anaripotiwa kuwa aliwahi kukwaruzana na baadhi ya wachezaji pamoja na viongozi wa klabu hiyo.
Unai Emery
Mataji makubwa aliyoshinda: Europa League mara tano, Ligue 1 mara moja, Kombe la Ufaransa mara mbili na Kombe la Ligi Ufaransa mara mbili.
Rekodi yake Ligi Kuu England: Mechi 200, ushindi 101; asilimia ya ushindi 50.5; wastani wa alama kwa mechi 1.75.
Emery ana asilimia bora ya ushindi ya asilimia 51 na wastani wa alama 1.75 kwa kila mechi kuliko kocha mwingine yeyote wa kudumu wa Aston Villa katika Ligi Kuu England.
Kocha huyo raia wa Hispania ana uzoefu mkubwa na kiwango cha heshima yake katika soka kimeendelea kupanda kutokana na kazi nzuri aliyoifanya tangu alipochukua mikoba ya Aston Villa Oktoba 2022.
Aliiwezesha Villa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 41, kabla ya kumaliza ukame wa klabu hiyo wa miaka 30 bila taji kwa kushinda Europa League msimu uliopita.
Licha ya kupoteza baadhi ya wachezaji muhimu katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi, kikosi chake kipya kinaanza kupata mwelekeo.
Hata hivyo, uwezekano wa Emery kuondoka na kujiunga na Manchester United unaonekana kuwa mdogo zaidi kufuatia taarifa kwamba anatarajiwa kusaini mkataba mpya.
Hali ya Michael Carrick
Mataji makubwa aliyoshinda: Hakuna.
Rekodi yake Ligi Kuu England: Mechi 29, ushindi 14; asilimia ya ushindi 48.3; wastani wa alama kwa mechi 1.76.
Baada ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa kocha wa muda wa United Januari, Carrick alikuwa na idadi kubwa zaidi ya ushindi (12) na alama (39) kuliko kocha mwingine yeyote wa Ligi Kuu England katika kipindi kilichosalia cha msimu wa 2025-26.
Licha ya kuwa kwenye shinikizo kubwa la kupoteza kazi yake Old Trafford, bado kuna uwezekano viongozi wa Manchester United wakaamua kuendelea kumwamini Carrick.
Baada ya kuanza na kumaliza vizuri msimu kufuatia kuwasili kwake Januari 2026, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa msimu huu, huku timu yake ikipata ushindi mara tatu pekee katika mechi 15 za mashindano yote.
Hata hivyo, timu yake imeonyesha uwezo wa kupambana katika baadhi ya mechi za hivi karibuni, ikiwemo kurejea na kuifunga Roma na kupata alama moja katika sare ya mabao 4-4 dhidi ya Aston Villa.
Lakini takwimu za jumla za timu yake haziridhishi, huku mwenendo wa matokeo ukiendelea kumuweka katika wakati mgumu kocha huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye akiwa mchezaji wa Manchester United alishinda mataji matano ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Klabu hiyo ipo katika hatari ya kushuka daraja, ikiwa nafasi ya 18, ambayo ni nafasi yake ya chini zaidi baada ya kucheza mechi 10 za ligi ndani ya miaka 40.
Pia ni mara ya pili pekee katika historia ya Ligi Kuu England kwa Manchester United kucheza mechi nane mfululizo bila kupata ushindi.