Hivi ndivyo vifungo virefu zaidi kuwahi kutolewa duniani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Adhabu ya kifungo cha miaka 200 jela iliyotolewa nchini Kenya dhidi ya mhubiri mwenye utata Paul Nthenge Mackenzie imeibua mjadala kuhusu hukumu kali na ndefu zaidi za vifungo kuwahi kutolewa duniani.

Mackenzie alihukumiwa na Mahakama Kuu ya Mombasa kutokana kuhusika kwake katika vifo vya watu 191, wakiwemo watoto 190, vilivyotokea katika Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Hapa tunaangalia wafungwa wengine ambao wamewahi kuhukumiwa vifungo vya miaka mamia au maelfu.

5. Allan Wayne McLaurin- Marekani

McLaurin na mshirika wake, Darron Bennalford Anderson, walihukumiwa kwa makosa ya kuteka, kubaka, na kumuibia mwanamke mzee.

Muda wa hukumu: McLaurin alipewa adhabu kali zaidi kuliko mshirika wake miaka 21,250.

Hata hivyo, miaka mitatu baadaye, adhabu yake ilipunguzwa kwa miaka 500 baada ya kukata rufaa na kufanya kifungo chake kubaki miaka 20,750.

Kufuatia hukumu hiyo, tarehe yake ya kuachwa huru (kama ingewezekana kimaisha) ingekuwa Septemba 20, 9837.

4. Charles Scott Robinson - Marekani

Mnamo tarehe 14 Desemba 1994, Charles Scott Robinson alipatikana na hatia katika mashtaka sita yanayohusiana na uhalifu wa kingono dhidi ya watoto, ikiwemo ubakaji kwa kutumia vitu, ulawiti wa kulazimishwa kwa njia ya mdomo, na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 16.

Robinson alihukumiwa kifungo cha miaka 5,000 kwa kila shtaka kati ya hayo sita na kufanya jumla ya miaka 30,000 kwa kosa la kubaka na kufanyia vitendo vya unyanyasaji mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 3.

Baraza la wazee wa mahakama lilipendekeza adhabu hizo za miaka 5,000, ambazo Jaji wa Wilaya Dan Owens aliamuru zitumikiwe mfululizo (moja baada ya nyingine).

Lengo lilikuwa kuhakikisha kuwa Robinson hatatoka gerezani kamwe, kwani adhabu ya "kifungo cha maisha bila uwezekano wa kuachiliwa kwa masharti" haikuwa adhabu inayofaa kisheria kwa uhalifu alioutenda.

3. Jamal Zougam - Uhispania

Jamal Zougam ni raia wa Morocco aliyehukumiwa kwa kuhusika katika mashambulizi ya mabomu kwenye treni yaliyotokea Machi 11, 2004, mjini Madrid, Uhispania.

Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu 191 na kujeruhi zaidi ya watu 1,800.

Zougam, awali alifuatiliwa na mamlaka kutokana na uhusiano wake na wanachama wa kundi la al-Qaeda, alitega moja ya mabomu hayo.

Pia alimiliki duka ambalo liliuza simu za mkononi zilizotumika kulipua mabomu hayo.

Mnamo Oktoba 2007, Zougam alipatikana na hatia ya mauaji katika mashtaka 191 na Mahakama kuu ya Uhispania, na kuhukumiwa kifungo cha miaka 42,922 jela; hata hivyo, atatumikia miaka 40 pekee, ambayo ndiyo adhabu ya juu zaidi inayoweza kutolewa chini ya sheria za Uhispania.

Zougam alizaliwa Tangier, Morocco, lakini baadaye alihamia Madrid, Uhispania.

Akiwa Madrid, Zougam alimiliki duka la simu za mkononi, ambalo baadaye ilibainika kuwa ndilo lililouza simu zilizotumika kulipua mabomu hayo mnamo Machi 11, 2004.

Zougam alianza kufuatiliwa na mamlaka mnamo Julai 2001, baada ya mamlaka za Ufaransa kudokeza kuwa huenda alikuwa na uhusiano na kundi la al-Qaeda nchini Uhispania.

Mamlaka zilifanya upekuzi katika makazi yake mjini Madrid na kukuta nyenzo za propaganda za kijihadi, ikiwemo video ya mahojiano ya Osama bin Laden, pamoja na namba za simu za magaidi wanaojulikana kuwa na uhusiano na al-Qaeda.

2. Otman el-Gnaoui - Uhispania

Othman El Gnaoui, raia wa Morocco aliyehukumiwa kwa kuhusika katika mashambulizi ya mabomu kwenye treni yaliyotokea Machi 11, 2004, mjini Madrid, Uhispania mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu 191 na kujeruhi zaidi ya watu 1,800.

El Gnaoui, anayeaminika kuwa mtu wa pili kwa mamlaka baada ya kiongozi wa njama hiyo, Jamal Ahmidan (anayefahamika pia kama "El Chino"), alipatikana na hatia ya kusafirisha vilipuzi vilivyotumika katika shambulio hilo na kutega bomu moja kati ya yale yaliyolipuka.

Mnamo Oktoba 2007, Mahakama ya Uhispania ilimtia hatiani El Gnaoui kwa makosa 191 ya mauaji na kumhukumu kifungo cha miaka 42,924 jela; hata hivyo, atatumikia miaka 40 pekee, ambayo ndiyo adhabu ya juu zaidi inayoweza kutolewa chini ya sheria za Uhispania.

El Gnaoui alizaliwa Tétouan, Morocco, na baadaye akahamia Uhispania. Inasemekana kuwa alifanya kazi kama fundi ujenzi kabla ya kukamatwa kwake mwaka 2004.

Mamlaka zilianza kumfuatilia El Gnaoui kutokana na tuhuma za biashara haramu ya dawa za kulevya, hatua iliyopelekea polisi kuweka kifaa cha kusikiliza mawasiliano kwenye simu yake ya mkononi. Kupitia uchambuzi wa mazungumzo hayo yaliyorekodiwa baada ya kukamatwa kwake, mamlaka ziligundua kuwa El Gnaoui alikuwa amewasiliana na magaidi wengine pamoja na washiriki wa njama hiyo katika wiki zilizotangulia mashambulizi ya Madrid.

Anaaminika kukutana na Shazad Ali Gutjar, raia wa Pakistan mwenye uhusiano na kundi la al-Qaeda ambaye alishtakiwa kwa kupanga shambulio jijini Barcelona.

Chamoy Thipyaso - Thailand

Adhabu ndefu zaidi ya kifungo kuwahi kutolewa kwa kosa la udanganyifu ilitolewa kwa Chamoy Thipyaso na washirika wake saba.

Kila mmoja wao alihukumiwa kifungo cha miaka 141,078 na mahakama ya Jinai ya Bangkok, nchini Thailand, mnamo tarehe 27 Julai 1989, kwa kosa la kuwalaghai wananchi kupitia biashara ya kukusanya amana iliyohusisha mamilioni ya dola.

Katika kesi dhidi ya Gabriel March Grandos, mwenye umri wa miaka 22, iliyosikilizwa huko Palma de Mallorca, Uhispania, mnamo tarehe 11 Machi 1972, upande wa mashtaka uliomba adhabu ya kifungo cha miaka 384,912 kwa kushindwa kuwasilisha barua 42,768 sawa na miaka 9 kwa kila barua.

Imeandaliwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Yusuph Mazimu