Wanasiasa 11 wa Afrika waliowahi kufungwa kabla ya kuwa Marais

    • Author, Beldeen Waliaula
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Kabla ya kuwa Marais na viongozi wa mataifa yao, baadhi ya marais wa Afrika waliwahi kuzuiliwa na kufungwa jela kwa miezi kadhaa au hata miaka.

Wengi wao walikamatwa wakati wanapinga utawala wa kikoloni, serikali za kiimla au wakidai mabadiliko ya kisiasa.

Kwa wengi wao, kuzuiliwa na kufungwa jela ilikuwa sehemu muhimu ya safari yao ya kisiasa. Baadhi yao walitoka gerezani na kuendeleza harakati ambazo baadaye zilichochea wao kuchaguliwa kuwa Rais au kushikilia nyadhfa za juu za uongozi wa nchi zao.

Kuanzia kwa Nelson Mandela wa Afrika Kusini hadi Hakainde Hichilema wa Zambia na Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, historia zao ni tofauti, lakini katika safari yao ya siasa na kuwa viongozi, wote wamewahi kutumikia kifungo gerezani.

Hawa ni baadhi ya viongozi wa Afrika waliowahi kufungwa kabla ya kuwa marais, ingawa wapo wengine wengi wanaofungwa na ndoto zao kisiasa kuzima;

Hakainde Hichilema - Miezi 4

Hichilema, ambaye amewahi kuwa kiongozi wa upinzani nchini Zambia, alikamatwa mwezi Aprili mwaka wa 2017 na polisi wa taifa hilo na kushtakiwa kwa kosa la uhaini.

Tuhuma hizo zilitokana na tukio ambalo msafara wake ulidaiwa kuzuia msafara wa Rais Edgar Lungu.

Hichilema alikanusha tuhuma hizo, huku mashirika ya haki za binadamu yakikosoa kukamatwa kwake na matumizi mabaya ya shtaka la uhaini.

Alikaa gerezani kwa takribani karibu miezi minne, kuanzia Aprili hadi Agosti 2017.

Mashtaka hayo ya uhaini yaliondolewa na aliachiliwa huru tarehe 16 mwezi Agosti 2017.

Baada ya kushindwa katika kampeni kadhaa za urais, Hichilema hatimaye alimshinda Edgar Lungu katika uchaguzi wa 2021.

Aliapishwa tarehe 24 Agosti 2021 kuwa rais wa Zambia.

Hichilema ameshinda tena hivi karibuni uchaguzi wa Urais uliofanyika mwezi Agosti mwaka wa 2026, na ameanza kuhudumu muhula wake wa pili kama rais wa Zambia.

Bassirou Diomaye Faye - Miezi 11

Faye alikuwa kiongozi wa upinzani na katibu mkuu wa chama cha PASTEF.

Alikamatwa mwezi Aprili mwaka wa2023 baada ya chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii na akashtakiwa kwa makosa ya kusambaza taarifa za uongo na kudharau mahakama.

Kukamatwa kwake kulitokea wakati kulikuwa na mzozo mkubwa wa kisiasa nchini Senegal uliomuhusisha pia kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko na serikali ya Rais Macky Sall.

Alikamatwa tarehe 14 Aprili 2023 na kukaa gerezani hadi mwezi Machi 2024 takribani miezi 11.

Aliachiliwa muda mfupi kabla ya uchaguzi wa urais kufuatia msamaha wa jumla.

Faye alishinda uchaguzi wa urais mwezi Machi mwaka wa 2024 na kuapishwa kuwa Rais tarehe 2 Aprili 2024.

Faye bado ni Rais wa Senegal na amekuwa madarakani kwa takribani miaka 2 na miezi 4.

Alpha Condé - Miaka 2

Condé alikuwa mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa akipinga utawala wa Rais Lansana Conté.

Baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 1998, Condé alikamatwa karibu na mpaka wa Côte d'Ivoire.

Alituhumiwa kujaribu kuondoka nchini Guinea kinyume cha sheria, kupinga kukamatwa na kupanga kuipindua serikali.

Baadaye alihukumiwa kwa makosa yaliyohusishwa na kutishia usalama wa taifa.

Condé alikamatwa mwezi Disemba mwaka wa 1998 na kuachiliwa mwezi Mei 2001 takribani miaka 2 na nusu baadaye.

Condé alishinda uchaguzi wa urais wa Guinea mwaka wa 2010 na kuingia madarakani mwezi Desemba mwaka huo.

Alihudumu kama rais kwa miaka 11 kuanzia 2010 hadi 2021

Aliondolewa madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwezi Septemba mwaka wa 2021.

Olusegun Obasanjo - Miaka 3

Obasanjo alikuwa tayari amewahi kuwa kiongozi wa kijeshi wa Nigeria kabla ya kukamatwa mwaka 1995.

Serikali ya kijeshi ya Jenerali Sani Abacha ilimkamata baada ya kumtuhumu kuhusika katika njama ya mapinduzi.

Obasanjo alikanusha tuhuma hizo. Kesi hiyo ilikosolewa sana, baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha, ambacho baadaye kilipunguzwa kuwa miaka 15.

Alifungwa jela kwa takriban miaka mitatu kuanzia 1995 hadi 1998

Aliachiliwa baada ya kifo cha Abacha mwaka 1998.

Obasanjo alishinda uchaguzi wa urais wa Nigeria mwaka 1999 na kuapishwa tarehe 29 Mei 1999.

Alihudumu kwa mihula miwili (miaka 8) kama rais kuanzia mwaka wa 1999 hadi 2007.

Jacob Zuma - Miaka 10

Zuma alijiunga na ANC na baadaye akawa mwanachama wa Umkhonto we Sizwe, kikosi cha kijeshi cha ANC kilichopigana dhidi ya mfumo wa apartheid.

Mwaka wa 1963, alipokuwa akijaribu kuondoka Afrika Kusini pamoja na wanachama wengine wa harakati hiyo, alikamatwa.

Alihukumiwa kwa mujibu wa sheria za utawala wa apartheid na kupewa kifungo cha miaka 10 kuanzia mwaka wa 1963 hadi 1973 muda mwingi akizuiliwa Robben Island.

Alikuwa na umri wa miaka 21 tu alipoanza kutumikia kifungo hicho.

Baadaye alikuja kuwa rais wa Afrika Kusini tarehe 9 Mei 2009.

Alihudumu kama rais wa Afrika Kusini kuanzia mwaka wa 2009 hadi 2018

Alijiuzulu mwezi Februari mwaka wa 2018 baada ya shinikizo kubwa kutoka ndani ya chama cha ANC.

Robert Mugabe - Miaka 11

Mugabe alikuwa mpinzani mkubwa wa utawala wa wazungu katika taifa hilo la Rhodesia Kusini kwa sasa Zimbabwe.

Alikamatwa baada ya kurejea nchini humo mwishoni mwa mwaka wa 1963.

Alituhumiwa kwa kutoa kauli za uchochezi na alikuwa akihusishwa na harakati za kitaifa za ZANU.

Ingawa awali alipewa kifungo kifupi, aliendelea kuzuiliwa kwa miaka mingi huku serikali ya wazungu ikikandamiza harakati za waliokuwa wakipinga utawala wao.

Mugabe alizuiliwa kwa takriban miaka 11 kuanzia 1963 hadi 1974

Akiwa gerezani, aliendelea kushiriki katika shughuli za kisiasa na hata kutoa masomo kwa wafungwa wenzake.

Zimbabwe ilipopata uhuru mwaka wa 1980, Mugabe akawa Waziri Mkuu.

Mwaka wa 1987 akawa rasmi rais wa Zimbabwe.

Alihudumu kama rais kwa muda wa miaka 30 kuanzia mwaka wa 1987 hadi 2017

Alijiuzulu mwezi Novemba mwaka wa 2017 baada ya jeshi kuingilia siasa za nchi hiyo na chama chake kumgeuka na kumtaka aondoke madarakani.

Hastings Kamuzu Banda - Miezi 13

Hastings Banda alirejea Nyasaland, ambayo leo ni Malawi, mwaka wa 1958 baada ya kuishi miaka mingi nje ya nchi hiyo.

Alikuwa kiongozi wa Nyasaland African Congress na alipinga vikali Central African Federation, ambayo wazalendo wengi Waafrika waliiona kama mfumo wa kuendeleza nguvu za wazungu.

Mwaka 1959, serikali ya kikoloni ilitangaza hali ya hatari na kupiga marufuku chama hicho. Banda alikuwa miongoni mwa viongozi waliokamatwa.

Alizuiliwa kwa takribani miezi 13, kuanzia Machi 1959 hadi Aprili 1960.

Alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Malawi mwaka wa 1964, wakati taifa hilo lilipopata uhuru.

Malawi ilipokuwa jamhuri mwaka 1966, Banda alikuwa rais wa kwanza.

Banda alihudumu kama rais kwa muda wa miaka 28 kuanzia mwaka wa 1966 hadi 1994

Aliondolewa madarakani baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kufanyika nchini humo mwaka wa 1994.

Kwame Nkrumah - Mwaka 1

Kwame Nkrumah alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa harakati za kupigania uhuru wa Ghana, wakati huo ikiitwa Gold Coast.

Mwaka wa 1950 alianzisha kampeni yake ya "Positive Action", iliyohusisha migomo, maandamano na kutoshirikiana na serikali ya kikoloni ya Uingereza.

Alikamatwa na serikali ya kikoloni na kuhukumiwa kwa uchochezi.

Alifungwa jela mwaka wa 1950, lakini aliachiliwa tarehe 12 Februari 1951, baada ya chama chake, Convention People's Party, kushinda uchaguzi wakati yeye bado alikuwa anazuiliwa gerezani.

Alikaa gerezani kwa takribani mwaka mmoja.

Kwame alishinda uchaguzi akiwa bado ni mfungwa.

Alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Gold Coast mwaka wa 1952, na baadaye Waziri Mkuu wa Ghana baada ya taifa hilo kupata uhuru mwaka wa 1957.

Ghana ilipokuwa jamhuri mwaka 1960, Nkrumah alikuwa rais wa kwanza wa taifa hilo.

Nkurumah alihudumu kama rais kwa muda wa maika sita kuanzia mwaka wa 1960 hadi 1966.

Aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi mwezi Februari 1966.

Jomo Kenyatta - Miezi 9

Jomo Kenyatta alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa wakipigania uhuru wa Kenya kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza.

Baada ya hali ya hatari kutangazwa mwezi Oktoba mwaka wa 1952, serikali ya kikoloni ilifanya operesheni ya kuwakamata viongozi wa kisiasa wa Kenya. Kenyatta alikuwa miongoni mwa viongozi hao, wanaojulikana kama The Kapenguria Six.

Serikali ya kikoloni ilimtuhumu Kenyatta kuwa kiongozi wa Mau Mau na kumhusisha na uasi dhidi ya utawala wa kikoloni. Kenyatta alikanusha mara kwa mara kuwa alikuwa kiongozi wa Mau Mau.

Kenyatta alikamatwa tarehe 20 mwezi Oktoba 1952 na kuzuiliwa hadi mwaka wa 1961.

Alizuiliwa katika maeneo tofauti nchini Kenya.

Baada ya kuachiliwa huru, Kenyatta alitangazwa kuwa Waziri Mkuu wa Kenya mwaka wa 1963, Kenya ilipopata uhuru. Mwaka wa 1964, Kenya ilipokuwa jamhuri, akawa rais wa kwanza wa taifa hilo

Kenyatta alihudumu kama rais kwa miaka 14 kuanzia mwaka wa 1964 hadi 1978.

Alifariki tarehe 22 mwezi Agosti mwaka wa 1978.

Nelson Mandela - Miaka 27

Nelson Mandela alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa harakati za kupinga mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid nchini Afrika Kusini.

Alijiunga na chama cha African National Congress (ANC) na baadaye akasaidia kuanzisha kikosi chake cha kijeshi, Umkhonto we Sizwe, baada ya serikali kuendelea kukandamiza upinzani.

Mwaka wa 1962, Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kwa kuondoka nchini bila kibali na kuwahamasisha wafanyakazi kugoma

Baadaye, katika kesi ya Rivonia, yeye na viongozi wengine wa ANC walihukumiwa kwa makosa ya hujuma na kupanga kuipindua serikali.

Mandela alifungwa gerezani kwa muda wa miaka 27 kuanzia mwaka 1962 hadi tarehe 11 Februari mwaka wa 1990.

Alifungwa katika magereza kadhaa, likiwemo gereza la Robben Island.

Aliapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini tarehe 10 mwezi Mei mwaka wa 1994, baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini ambao ulihusisha watu wa rangi zote.

Alihudumu kama rais kwa muda wa miaka mitano kuanzia 1994 hadi 1999. Mandela alistaafu kwa hiari baada ya kumaliza muhula mmoja.

Abdoulaye Wade - Senegal

Abdoulaye Wade alikuwa mwanasiasa wa muda mrefu wa upinzani ambaye alikuwa akipinga chama cha Socialist Party kilichokuwa madarakani nchini Senegal.

Baada ya uchaguzi wa urais wa 1988, Wade na viongozi wengine wa upinzani walidai uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu na maandamano yakazuka.

Wade alizuiliwa kwa kushiriki katika maandamano dhidi ya serikali na akahukumiwa ila hakutumikia kifungo.

Alikamatwa tena mwaka wa 1994 baada ya kutuhumiwa kuhusishwa na mauaji ya afisa wa serikali. Tuhuma hizo baadaye ziliondolewa.

Vipindi vyake vya kuzuiliwa vilikuwa vya muda mfupi, tofauti na viongozi wengine kama Mandela, Kenyatta au Zuma.

Alishinda uchaguzi wa urais mwaka wa 2000 na kuongoza Senegal kwa miaka 12 kuanzia mwaka wa 2000 hadi 2012.