Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matapeli wanawasubiri watumiaji wapya wa intaneti ili kuwaibia. Wanawezaje kujilinda?
Mtandao wa intaneti duniani unaendelea kupokea watumiaji wapya kwa mara ya kwanza, na wengi wao hawana uzoefu wa kutosha wa kutambua mbinu za ulaghai zinazotumiwa na matapeli. Tunawezaje kuwalinda?
Mwaka wa 2022, Anicet Etekpo, afisa wa usalama nchini Benin, alibofya kiungo alichotumiwa kupitia Facebook na mtu aliyedhani kuwa rafiki yake.
"Kiungo hicho kilinipeleka kwenye tovuti ya kitapeli iliyonitaka kutoa taarifa zangu binafsi, ikiwemo taarifa za akaunti yangu ya benki," aliiambia BBC.
Etekpo alipoteza kiasi kikubwa cha fedha na kuanza kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa taarifa zake binafsi.
Wakati tukio hilo lilipotokea, alikuwa ametumia intaneti kwa miaka michache tu. Kadiri upatikanaji wa intaneti unavyozidi kupanuka katika maeneo kama Afrika Magharibi, mamilioni ya watu watakabiliwa kwa mara ya kwanza na hatari za mtandaoni kama zilizompata Etekpo. Je, wanawezaje kulindwa?
Inakadiriwa kuwa watu bilioni 2.6, sawa na takriban theluthi moja ya idadi ya watu duniani, bado hawana uwezo wa kutumia intaneti.
Iwapo upatikanaji wa intaneti utaendelea kuongezeka kwa kasi ya sasa, takriban watu wengine bilioni mbili watapata huduma hiyo ifikapo mwaka 2030.
Kwa watumiaji wengi wapya, hali hiyo itamaanisha kukutana kwa mara ya kwanza na jumbe taka (spam), programu hasidi zinazodai fedha ili kurejesha taarifa zilizofungwa (ransomware), pamoja na tovuti bandia zinazotumiwa kuwalaghai.
Hali hiyo inawapa wahalifu wa mtandaoni fursa mpya za kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, katika kile kinachoweza kuelezwa kama "mbio za kutafuta utajiri kupitia uhalifu wa mtandaoni".
Hata hivyo, mifumo iliyoundwa kuwalinda watumiaji wapya, kuanzia mafunzo ya matumizi salama ya teknolojia ya kidijitali hadi hatua za kuwalinda watumiaji dhidi ya ulaghai, haijapanuka kwa kasi sawa na ongezeko la watumiaji wa intaneti.
"Kinachojitokeza ni mfumo wa uhalifu wa mtandaoni unaozidi kuwa wa kitaalamu na unaotumia fursa zinazojitokeza," anasema Zeki Turedi, afisa mkuu wa teknolojia katika eneo husika wa kampuni ya CrowdStrike, inayojihusisha na usalama wa mtandao na kufuatilia wahalifu wa kidijitali.
"Ingawa kazi yetu kubwa ni kusaidia makampuni, athari chanya za juhudi hizo za ulinzi huwafikia pia watu binafsi. Hasa tunaposaidia kulinda miundombinu muhimu kama vile huduma za afya, elimu na huduma za umma ambazo watumiaji wengi wapya wa intaneti wanazitegemea."
Wahalifu wa mtandaoni wanatumia teknolojia za kiotomatiki, akili mnemba (AI) na mbinu za kisaikolojia za kuwahadaa watu ili kutumia mianya yoyote ya kiusalama katika mifumo ya kidijitali, bila kujali muda ambao watumiaji wamekuwa wakitumia intaneti.
Hata hivyo, kwa watu wanaokutana na vitisho hivyo kwa mara ya kwanza, mabadiliko katika mazingira ya mtandao yanaweza kufanya iwe vigumu zaidi kuvitambua, anasema Turedi.
"Kwa upande mmoja, mtumiaji mpya wa intaneti leo anapata fursa ya kupata taarifa, huduma na nafasi zinazoweza kubadilisha maisha yake. Kwa upande mwingine, anakutana na mazingira ya kidijitali ambayo ni changamani zaidi na yenye hatari kubwa kuliko yalivyokuwa wakati wengi wetu tulipoanza kutumia intaneti," anasema.
Siku hizi, wahalifu wa mtandaoni wanaweza kutumia ujumbe wa ulaghai uliotengenezwa kulingana na utamaduni au lugha ya eneo husika ili kujifanya kuwa benki za ndani, kutoa ahadi za msaada bandia wa serikali au kutangaza programu za simu zinazoonekana kuwa salama lakini kwa hakika zina programu za ujasusi zinazoweza kufuatilia shughuli za watumiaji.
"Tunatarajia hali hii kuongezeka zaidi kadiri wahalifu wanavyobadilisha mbinu zao na kutumia maudhui yanayotengenezwa na akili mnemba pamoja na teknolojia ya kutengeneza video au sauti bandia zinazofanana na za watu halisi (deepfakes)," anaongeza Turedi.
Mara nyingi wahalifu hawa huratibu mipango yao kupitia majukwaa ya mtandao wa giza (dark web) na njia za mawasiliano zilizofichwa kwa teknolojia ya usimbaji fiche.
Baadhi ya makundi hata huuza kile kinachoitwa "vifurushi vya kuanzia" vya uhalifu wa mtandaoni. Vifurushi hivyo huwa na vifaa vilivyoandaliwa tayari kwa ajili ya ulaghai wa kupata taarifa binafsi (phishing), au ufikiaji wa taarifa za siri zilizoibwa, na hivyo kurahisisha hata wahalifu wasio na ujuzi mkubwa wa teknolojia kuingia katika shughuli hizo.
Mashirika ya kimataifa ya kutekeleza sheria yameonya kuwa uhalifu wa mtandaoni unazidi kupangwa kwa utaratibu na kuendeshwa kama biashara.
Kwa mfano, Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU) kuhusu Kielezo cha Usalama wa Mtandao Duniani (Global Cybersecurity Index) inaangazia hatari zinazowakabili watumiaji wapya wa intaneti, zikiwemo ulaghai, wizi wa taarifa kupitia ujumbe bandia (phishing) na ongezeko la mashambulizi ya programu hasidi zinazodai fedha ili kurejesha taarifa zilizofungwa (ransomware).
Kwa Etekpo, madhara ya ulaghai huo yalikuwa halisi.
"Nilijihisi sina ulinzi na nilikuwa katika hatari kubwa," alisema.
Anaamini kuwa udhaifu wa watu wengi hautokani sana na kutokuwa na ujuzi wa teknolojia, bali na suala la uaminifu.
"Watu wengi huwaamini watu wanaowasiliana nao mtandaoni na kuchukua hatua haraka bila kwanza kuthibitisha kama ujumbe waliopokea ni halali," alisema.
Hatari hii ni kubwa zaidi barani Afrika. Licha ya kuwa na baadhi ya viwango vya juu zaidi vya ukuaji wa matumizi ya intaneti duniani, Afrika bado ndiyo bara lenye idadi ndogo zaidi ya watu waliounganishwa na intaneti.
Utafiti mmoja wa hivi karibuni pia ulibaini tofauti kubwa katika viwango vya upatikanaji wa intaneti katika maeneo mbalimbali ya bara hilo.
Wakati nchi kama Afrika Kusini na Ushelisheli sasa zina viwango vya upatikanaji wa intaneti vinavyokaribia asilimia 80, maeneo ya vijijini katika baadhi ya sehemu za Benin na nchi zenye idadi kubwa ya watu kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado zina idadi kubwa ya watu ambao hawajaunganishwa na intaneti.
Huduma za intaneti kupitia satelaiti ni ghali, miundombinu ya intaneti ya nyaya za kudumu ni michache na mara nyingi si ya kuaminika. Aidha, ukosefu wa mifumo madhubuti ya ulinzi unawaweka katika hatari ya kutapeliwa watu wanaofanikiwa kupata huduma ya intaneti.
Kwa kuzingatia kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti barani Afrika inatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya watu milioni 280 katika kipindi cha miaka minne ijayo, kuna haja ya haraka ya kuweka mikakati bora zaidi ya kuzuia uhalifu wa mtandaoni.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol), hasara zinazotokana na uhalifu wa mtandaoni barani Afrika zimeongezeka zaidi ya mara mbili tangu mwaka 2024, kutoka dola milioni 192 hadi dola milioni 484.
Baadhi ya hatua za kuwalinda watumiaji tayari zimewekwa, lakini wataalamu wanaamini kuwa zinahitaji kuimarishwa zaidi. Hatua hizo ni pamoja na programu za kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya kidijitali shuleni na kuimarisha ulinzi wa watumiaji dhidi ya ulaghai wa mtandaoni.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) imebuni teknolojia za kisasa za kugundua vitisho vya mtandaoni pamoja na mifumo ya usalama iliyojengewa ndani, kama vile udhibiti wa ufikiaji wa mifumo na utambuzi wa programu hasidi, kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.
Wakati huo huo, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lina vikosi maalumu vya maafisa waliopewa mafunzo ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni katika kila ofisi yake ya kikanda.
Nchini Uingereza, Shirika la Kitaifa la Uhalifu (NCA) limeongoza uchunguzi kadhaa wa kimataifa uliofanikiwa dhidi ya makundi ya wahalifu wa mtandaoni.
Hata hivyo, hatua hizi nyingi zimejikita katika kuchunguza uhalifu wa mtandaoni baada ya kutokea, badala ya kushughulikia hatari zinazowakabili watumiaji wapya wa intaneti.
"Usalama wa mtandao ni suala kubwa sana linalotia wasiwasi," anasema Robert Anderson, mwanzilishi wa Telecom4Good, shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma za teknolojia ya habari kwa mashirika mengine yasiyo ya kiserikali duniani, mengi yakiwa barani Afrika, ili kuyasaidia kupata huduma salama na za bei nafuu za intaneti.
Kampuni ya CrowdStrike inapendekeza mashirika "yasichukulie usalama wa mtandao kama orodha ya hatua za kukamilisha mara moja, bali kama mchakato endelevu wa kuboresha mifumo ya ulinzi."
Hatari hizo zinatarajiwa kuongezeka kadiri mifumo ya kidijitali inavyoendelea kupanuka. Kwa mujibu wa makadirio ya sekta hiyo, idadi ya vifaa vilivyounganishwa na intaneti duniani, kuanzia mitambo ya kuzalisha umeme, vifaa vya kudhibiti mapigo ya moyo (pacemakers) hadi magari yanayojiendesha yenyewe, inatarajiwa kufikia zaidi ya bilioni 38 ifikapo mwaka 2030.
Kadiri idadi ya mifumo inayounganishwa na intaneti inavyoongezeka, ndivyo mianya inayoweza kutumiwa na wadukuzi kufanya mashambulizi ya mtandaoni inavyoongezeka.
Serikali na mashirika ya kutekeleza sheria yanajitahidi kutafuta na kujaribu mbinu mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo. Baadhi ya serikali zimejaribu kuweka sheria zinazofanya aina mbalimbali za uhalifu wa mtandaoni kuwa makosa ya jinai.
Umoja wa Afrika umeweka usalama wa mtandao kuwa mojawapo ya vipaumbele muhimu chini ya mpango wake wa "Ajenda 2063". Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol) linasaidia vyombo vya polisi barani Afrika kuzuia na kuchunguza uhalifu wa mtandaoni. Juhudi hizo zinajumuisha kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wadogo kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya ulaghai wa mtandaoni.
Nchini Myanmar, ambako matumizi ya intaneti yaliongezeka kwa kasi katika miaka ya 2010, Idara ya Mambo ya Nje ilifadhili kampeni ya kutoa elimu kwa umma iliyolenga watumiaji wapya wa intaneti.
Mwaka 2024, Nigeria ilifanyia marekebisho Sheria yake ya Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrimes Act), na kuongeza hatua za kuwalinda watumiaji katika masoko mapya ya kidijitali.
Nchini India, kwa upande mwingine, serikali ilianzisha nambari maalumu ya simu ya kitaifa inayowawezesha waathiriwa kuripoti ulaghai mara moja na kuzuia fedha zilizoibwa kupitia benki na programu za malipo.