Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
PAUL MACKENZIE:: Kutoka muhubiri mpaka mfungwa wa miaka 200 jela kwa mauaji
- Author, Asha Juma
- Nafasi, Journalist,
- Akiripoti kutoka, BBC, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kesi ya Paul Nthenge Mackenzie ni mojawapo ya kesi kubwa zaidi za vifo vinavyohusishwa na dhehebu la kidini nchini Kenya. Ilivuta hisia za kimataifa mwaka 2023 baada ya kugunduliwa kwa mamia ya miili katika msitu wa Shakahola, karibu na Malindi, katika eneo la pwani ya Kenya.
Mackenzie, aliyeanzisha kanisa la Good News International Ministries mwaka 2003, alishtakiwa kwa kupanga mauaji ya wafuasi wake kwa kuwahimiza kufunga kula hadi kufa wakiamini kwamba 'Wangekutana na Yesu'.
Hii hapa historia ya matukio muhimu, kuanzia kuanzishwa kwa kanisa lake, maonyo ya awali kwa mamlaka, ugunduzi wa miili na kesi mahakamani hadi hukumu ya miaka 200 jela.
2003: Mackenzie aanzisha kanisa lake
Paul Mackenzie alianzisha kanisa la Good News International Ministries mwaka 2003 katika eneo la Malindi, kaunti ya Kilifi.
Kanisa hilo lilipata umaarufu na kuvutia maelfu ya wafuasi kupitia matawi yake mbalimbali nchini Kenya. Baadaye lilianzisha kituo cha televisheni kilichoitwa Times TV, kilichokuwa kikirusha mahubiri yake.
Katika mafundisho yake, Mackenzie alipinga elimu ya kawaida, huduma za afya na baadhi ya sera za serikali, akidai kuwa zilikuwa kinyume na mafundisho ya Biblia.
2017: Malalamiko ya kwanza yafikishwa mahakamani
Mackenzie alianza kukabiliwa na matatizo ya kisheria mwaka 2017 kutokana na madai ya kuendesha taasisi ya elimu isiyosajiliwa na kuwanyima watoto haki ya kupata elimu.
Tarehe 17 Oktoba 2017, alifikishwa mahakamani pamoja na washirika wake Winne Alexander Gandi na Betty Mwaka.
Mashtaka yalihusisha kutoa elimu katika taasisi isiyosajiliwa na kuzuia watoto kupata elimu ya msingi. Mackenzie aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 100,000 za Kenya na kutakiwa kuripoti polisi kila wiki.
Baadhi ya watoto waliokuwa katika mazingira ya kanisa walipelekwa katika vituo vya uangalizi na ulinzi.
2019: Kanisa lafunga shughuli zake Malindi
Mwaka 2019, mamlaka ziliendelea kufuatilia shughuli za Mackenzie na kanisa lake. Katika kikao cha Kamati ya Watumiaji wa Mahakama ya Kaunti ya Kilifi, kilichofanyika Novemba 15, suala la madai ya kueneza itikadi kali kwa watoto kupitia kanisa na kituo chake cha televisheni lilijadiliwa.
Mamlaka ya Mawasiliano Kenya baadaye ilifuta leseni ya Times TV.
Kanisa kuu lilifungwa mwaka huo na Mackenzie akahamia katika msitu wa Shakahola, ambako aliwahimiza wafuasi wake kujiunga naye. Makazi yao yalikuwa yamegawanywa katika maeneo yenye majina ya kibiblia kama Yerusalemu na Yudea.
2021–2023: Mafundisho ya kufunga kula yaanza kutekelezwa
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mfumo wa kufunga kula hadi kufa ulianza Januari 2021 na kuendelea kwa zaidi ya miaka miwili.
Mackenzie na viongozi wengine wa dhehebu hilo waliwahimiza wafuasi kujinyima chakula ili kujiandaa kukutana na Yesu na kwenda mbinguni kabla ya mwisho wa dunia.
Ushahidi ulionyesha kuwa mfumo huo ulianza kwa madai ya hiari, lakini baadaye baadhi ya watu walilazimishwa kushiriki. Watoto walitajwa kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutakiwa kufunga kula, wakifuatiwa na vijana, wanawake na hatimaye wanaume.
2023: Ugunduzi wa makaburi ya halaiki na kukamatwa kwa Mackenzie
Machi 2023: Taarifa za vifo zaanza kufikishwa kwa mamlaka
Machi 2023, taarifa za watoto waliokuwa wamefariki kutokana na njaa na kukosa hewa ndani ya msitu wa Shakahola zilianza kufikishwa kwa mamlaka.
Tarehe 21 Machi, Francis Wanje alipata amri ya mahakama iliyotaka miili ya watoto wawili ifukuliwe kwa uchunguzi wa kitabibu na upimaji wa DNA. Hata hivyo, hatua za kufukua miili hazikuchukuliwa mara moja.
Machi 22–23, 2023: Mackenzie akamatwa kwa mara ya kwanza
Mackenzie alikamatwa kuhusiana na vifo vya watoto wawili waliodaiwa kufariki baada ya kufuata maagizo ya kufunga kula.
Hata hivyo, aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 10,000 za Kenya.
Aprili 2023: Ugunduzi wa miili zaidi na kukamatwa tena
Tarehe 14 Aprili, polisi waliingia msituni kufuatia amri ya mahakama ya kufukua miili ya watoto wawili. Hatua hiyo ilifichua ukubwa wa mkasa wa Shakahola.
Mackenzie alikamatwa tena huku uchunguzi ukipanuka. Tarehe 17 Aprili, serikali iliomba ruhusa ya kufukua miili mingine 14 kwa uchunguzi wa kitaalamu.
Operesheni za uokoaji na ufukuaji ziliendelea katika eneo hilo lenye ukubwa wa takribani ekari 800. Baadhi ya wafuasi waliokolewa wakiwa katika hali mbaya ya utapiamlo.
Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa wengi walikufa kwa njaa, huku wengine wakifariki kutokana na kukosa hewa, kunyongwa au majeraha ya kichwani.
Mei 2023: Serikali ya Kenya yaingilia kati
Rais William Ruto alianzisha tume ya uchunguzi kuhusu mkasa huo na kuunda kikosi kazi cha kuchunguza mfumo wa usimamizi wa taasisi za kidini nchini.
Mackenzie na washukiwa wengine walizuiliwa huku uchunguzi ukiendelea kuhusu mauaji, ugaidi, itikadi kali na unyanyasaji wa watoto.
2024: Mackenzie afikishwa mahakamani kwa mashtaka ya mauaji
Februari 6, 2024: Mackenzie na washirika wake wasomewa mashtaka
Mackenzie na washukiwa wengine 30 walifikishwa katika Mahakama Kuu ya Malindi, ambapo walisomewa mashtaka 191 ya mauaji yaliyohusisha watoto 190 na mtu mzima mmoja.
Washtakiwa wengi walikana mashtaka. Enos Amanya Ngala alikiri makosa yote, huku mshtakiwa mwingine akiahirishiwa kusomewa mashtaka kutokana na hali yake ya kiafya.
Mei 17, 2024: Mahakama yashughulikia pingamizi la awali
Baadhi ya washtakiwa waliwasilisha pingamizi kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka na haki yao ya kupata kesi ya haki.
Mahakama ilishughulikia pingamizi hilo katika uamuzi wa Jaji M. Thande na kuruhusu mchakato wa kesi kuendelea.
Julai 8, 2024: Kesi ya mauaji yaanza kusikilizwa
Kesi ya mauaji dhidi ya Mackenzie na wenzake ilianza kusikilizwa. Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi, wakiwemo manusura, wataalamu wa uchunguzi wa maiti na maafisa waliohusika katika uchunguzi.
Ushahidi ulieleza jinsi mafundisho ya Mackenzie yalivyotumiwa kuwashawishi wafuasi kuhamia Shakahola na kushiriki katika mfungo uliosababisha vifo.
2025–2026: Ushahidi wa kesi waendelea kuwasilishwa
Katika kipindi hiki, upande wa mashtaka uliendelea kuwasilisha ushahidi kuhusu mfumo wa uongozi wa dhehebu hilo, ukiwemo majukumu ya walinzi, wachimbaji makaburi na viongozi wengine.
Makazi ya wafuasi yalikuwa yamegawanywa katika maeneo yenye majina ya kibiblia kama Galilaya, Bethlehemu, Yudea na Emau.
Januari 9, 2026: Upande wa mashtaka wafunga ushahidi katika kesi nyingine
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ilitangaza kufunga ushahidi wake katika kesi nyingine iliyohusisha Mackenzie na washtakiwa wengine 96.
Kesi hiyo ilihusu masuala mapana ya ugaidi, itikadi kali za kidini na unyanyasaji wa watoto, tofauti na kesi ya mauaji ya watu 191.
Oktoba 19, 2026: Mackenzie na washirika wake wapatikana na hatia
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama Kuu iliyoketi Mombasa ilimpata Mackenzie na washtakiwa wengine 28 na hatia ya mauaji.
Jaji Diana Kavedza alisema upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha mashtaka yote 191.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa dhidi ya watu 31, lakini wawili walifariki wakati kesi ikiendelea, hivyo waliobaki 29 ndio waliopatikana na hatia.
Mahakama ilibaini kuwa Mackenzie alikuwa na jukumu kuu katika kuhamasisha wafuasi kufunga kula hadi kufa kwa imani kwamba wangekutana na Yesu.
Ushahidi ulionyesha kuwa baadhi ya wafuasi walilazimishwa kutekeleza maagizo hayo kwa vitisho na kupigwa.
Uamuzi huo ulihusisha vifo vya watu 191 pekee, licha ya miili 429 kufukuliwa katika msitu wa Shakahola kati ya Aprili na Julai 2023.
Novemba 6, 2026: Mackenzie ahukumiwa miaka 200 jela
Mahakama Kuu ya Mombasa imemhukumu Paul Mackenzie kifungo cha miaka 200 jela kutokana na mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190.
Jaji Diana Kavedza aligawa adhabu hiyo katika sehemu mbili:
Miaka 100 kwa mauaji yaliyotokana na njaa.
Miaka 100 kwa mauaji ya moja kwa moja.
Adhabu hizo zitatumikia moja baada ya nyingine, na kufanya jumla ya kifungo chake kuwa miaka 200.
Msaidizi wake wa karibu, Smart Mwakalama, alihukumiwa kifungo cha miaka 160 jela.
Kwa mujibu wa taarifa za Reuters na Associated Press, watu 183 kati ya wahanga 191 walifariki kutokana na njaa, huku wanane wakiuawa moja kwa moja.
Hukumu hiyo imekuwa hatua muhimu katika kesi iliyotikisa Kenya na kuvutia hisia za kimataifa.
Hata hivyo, Mackenzie bado anakabiliwa na kesi nyingine zinazohusiana na ugaidi, unyanyasaji wa watoto na vifo vingine vilivyohusishwa na shughuli za dhehebu lake.
Maswali ambayo bado hayajajibiwa
Licha ya hukumu hiyo, mkasa wa Shakahola bado unaacha maswali mengi. Miili 429 ilifukuliwa, lakini kesi ya mauaji iliyotolewa hukumu inahusu watu 191 pekee.
Pia, uchunguzi umeibua maswali kuhusu namna mamlaka za serikali na vyombo vya usalama vilivyoshindwa kuchukua hatua za mapema licha ya taarifa zilizokuwa zikitolewa kuhusu shughuli za dhehebu hilo.
Kwa familia za wahanga, hukumu ya Mackenzie ni hatua muhimu ya kutafuta haki, lakini bado kuna mchakato mpana wa kuwawajibisha wote waliohusika na mkasa huo.
Na Asha Juma