Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Microdramas: Tamthilia fupi zinazoteka kizazi cha mitandao
Spare Arrow ilitoa tamthilia yake ya kwanza fupi ya vichekesho, Glen's Boutique, kupitia mitandao ya kijamii mapema mwaka huu.
Kila jioni, Heather Sharrock hujiandaa kutazama kipindi anachokipenda.
Lakini haikuonyeshwa kwenye Netflix, BBC iPlayer wala televisheni yake, bali kwenye simu yake.
Wakati baadhi yetu tunaweza kutazama vipindi vichache vya tamthilia tunayoipenda kila usiku, Heather anaweza kutazama vipindi vingi zaidi kwa mfululizo, kwa sababu mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 55 kutoka Scotland ni shabiki wa microdramas.
"Kuna mambo mengi mabaya yanayoendelea duniani kwa sasa," anasema Heather. "Ni vizuri tu kujitenga na yote hayo na kutofikiria chochote kwa muda mfupi."
Microdramas, ambazo tayari zimepata umaarufu mkubwa nchini China, zinazidi kupendwa nchini Uingereza na zinapatikana kwenye programu kama ReelShort, CandyJar na DramaBox.
Wiki iliyopita, watayarishaji walitangaza kuwa simulizi za zamani za tamthilia ya Neighbours zitabadilishwa na kuwa vipindi vifupi vinavyoonyeshwa kwa mfumo wa video fupi za mitandao ya kijamii, ikiwa ni mojawapo ya ishara kwamba aina hii ya burudani inazidi kupata nafasi katika soko kuu.
Tamthilia hizi huwa na vipindi vifupi vyenye matukio mengi na kasi kubwa, ambavyo kwa kawaida hudumu kati ya sekunde 60 na 90. Nyingi huzungumzia mapenzi, migogoro ya kifamilia na mabilionea wanaoficha siri, huku karibu kila kipindi kikiishia katika tukio linalomfanya mtazamaji atake kujua kitakachofuata.
Kila tamthilia huwa na vipindi 50 au zaidi, hivyo muda wa jumla wa kuitazama unaweza kulingana na filamu moja ndefu.
Diane Aitken, 45, shabiki mwingine kutoka Scotland, anazilinganisha tamthilia fupi zinazohusu mbwa-mwitu na vampires anazopenda na tamthilia za Kimarekani za miaka ya 1980 kama Dallas na Dynasty, lakini zikiwa na msisimko wa hali ya juu zaidi.
Diane na Sarah-Jayne wanasema kuwa walianza kuvutiwa na microdramas baada ya kuona matangazo yake kwenye mitandao ya kijamii.
Jinsi microdramas zilivyoanza kupata umaarufu
Tamthilia hizi fupi zilianza kujitokeza nchini China mwishoni mwa miaka ya 2010, zikitokana na riwaya za mtandaoni zilizobadilishwa kuwa vipindi vya gharama nafuu na vinavyoweza kurekodiwa kwa muda mfupi, anasema Samantha Sun, mtengenezaji wa filamu aliyezaliwa China.
Kwa mashabiki wengi, tamthilia hizi ni njia ya kujitenga kwa muda na changamoto za maisha.
Sarah-Jayne Lunn, 46, kutoka Doncaster, anasema zilimsaidia kukabiliana na kipindi kigumu maishani mwake.
"Mara moja nilivutiwa nazo," anasema. "Sikulazimika kufikiria sana."
Jen Cooper, ambaye ni mtazamaji wa microdramas na sasa anafanya kazi kama mshauri katika tasnia hiyo, anakubaliana naye.
Anasema awali tamthilia hizi zilikuwa maarufu zaidi miongoni mwa wanawake wa umri wa makamo waliopenda simulizi za mapenzi, huku wapenzi wa vitabu na hadithi za kimapenzi mtandaoni pia wakizifuatilia. Hata hivyo, sasa zimepata umaarufu miongoni mwa hadhira pana zaidi.
Watazamaji nchini China wamevutiwa na simulizi zenye matukio ya kusisimua na kasi ya haraka katika microdramas.
Mwaka jana, soko la microdramas nchini China lilikuwa na thamani ya zaidi ya yuan bilioni 100 (dola za Marekani bilioni 14), huku idadi ya watazamaji ikizidi milioni 800, kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Redio na Televisheni ya China.
Hata hivyo, tamthilia hizi pia zimepata umaarufu nchini Korea Kusini, India na Marekani, huku huduma za kuonyesha tamthilia kama Prime, Peacock na Disney+ zikitangaza mipango ya kuziongeza kwenye majukwaa yao.
Nchini Uingereza, TattleTV, inayojitambulisha kama programu ya kwanza nchini humo inayojikita katika microdramas, ilizinduliwa mapema mwaka huu.
Kampuni mbalimbali pia zinatumia umaarufu wa microdramas kutengeneza matangazo mafupi ya video kwaajili ya mitandao ya kijamii.
Tamthilia fupi za kutazama ukiendelea na shughuli zako
Microdramas zinahitaji kuwa na matukio ya haraka ili kuvutia na kudumisha umakini wa watazamaji, anasema Charlotte Brokenbrow kutoka kampuni ya utayarishaji wa vipindi ya Spare Arrow nchini Wales, iliyotengeneza tamthilia yake ya kwanza mwaka huu.
"Ikiwa utaacha nafasi kubwa ya ukimya kwenye maandishi na video, mtu atachoshwa na kuendelea kuperuzi," anasema.
Mbali na kasi ya matukio, microdramas zimepata umaarufu kwasababu watu wanaweza kuzitazama katika vipande vifupi, jambo lililowafanya baadhi ya wachambuzi kuziita burudani za 'snackable' yaani maudhui mafupi yanayotazamika kwa urahisi.
Pia zinaendana na mabadiliko ya namna watu wanavyotumia maudhui ya burudani kwa urahisi, bila kujifunga kuyatazama kwa muda mrefu, anasema Dkt Tina Kendall, profesa mshiriki wa filamu na habari katika Chuo Kikuu cha Anglia Ruskin.
Baadhi ya watu waliozungumza na BBC News walisema huzitazama wakiwa kwenye magari wakisubiri kuwachukua watoto wao shuleni, huku wengine wakiziweka zikiendelea huku wakifanya usafi au shughuli nyingine za nyumbani.
Sarah-Jayne anasema matukio yake huwa rahisi kutabirika kiasi kwamba anaweza kuzifurahia hata akiwa kazini.
Programu maalumu za microdramas kwa kawaida huwavutia watazamaji kwa kuwaruhusu kutazama vipindi vichache vya mwanzo bila malipo kabla ya kuhitaji kulipia usajili.
Unapoendelea kuperuzi programu hizo, utakutana mara kwa mara na simulizi kuhusu mabosi wa magenge ya uhalifu, maadui wanaogeuka kuwa wapenzi na wachunga ng'ombe.
Sun anasema kampuni za utayarishaji nchini China mara nyingi hurudia mifumo ya simulizi zilizofanikiwa, zikifanya mabadiliko madogo tu.
Hilo pia limemvutia Heather. "Nyingi zina simulizi zilezile, tofauti ni mazingira tu," anasema, akiongeza kuwa sasa amechoshwa na simulizi za wakurugenzi wakuu wa kampuni ambao ni mabilionea.
Baadhi ya mashabiki wanasema simulizi fulani zimekuwa zikidhalilisha wanawake, huku nyingine zikionyesha kwa namna isiyofaa matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kingono.
"Ilifikia hatua ya kuwa kama mzaha kwamba muigizaji mwanamke alikuwa amekumbwa na mambo mengi ya kutisha, akilia na kupiga kelele mara nyingi kabla hata ya kufika wakati wa chakula cha mchana," anasema Coco Taylor, muigizaji aliyeigiza katika microdrama yake ya kwanza mwaka 2024.
Taylor anasema amewahi kukataa nafasi katika baadhi ya tamthilia kwasababu alihisi zilikuwa na maudhui yanayowadhalilisha wanawake.
Hata hivyo, yeye na mashabiki wengine wanasema uandishi wa simulizi hizo umeimarika, hasa kutokana na kuongezeka kwa timu za Marekani na Uingereza zinazoshiriki kuandika hadithi hizo.
Pia wanafurahia kuona microdramas zikitanuka na kujumuisha aina nyingine za burudani kama vichekesho, filamu za kusisimua na za kutisha.
Coco Taylor anaigiza katika microdrama ya uchunguzi wa mauaji iliyorekodiwa na kampuni ya utayarishaji wa filamu kutoka Wales.
Ni za haraka kutengeneza, gharama nafuu na zenye faida
Haydn Wakeling, mwanzilishi wa kampuni ya utayarishaji wa filamu ya Black Swan, anasema alisikia kuhusu microdramas kwa mara ya kwanza mapema mwaka huu kupitia mtu anayefanya kazi katika tasnia ya filamu.
"Kwa muda mfupi tu, sasa kila mtu anazungumzia jambo hili," anasema.
Wakeling anasema microdramas zina mvuto mkubwa kifedha kwa wakurugenzi na watayarishaji wa filamu, kwani kwa kawaida huchukua chini ya wiki mbili kurekodi tamthilia yenye jumla ya dakika 60 hadi 90, jambo linalopunguza gharama za utayarishaji.
Mkurugenzi Dan Löwenstein alishiriki katika utayarishaji wa microdrama yake ya kwanza, Mafia Lover, mwezi Februari 2024. Sasa anashiriki katika utayarishaji wa tamthilia yake ya 38.
Mwanzoni alifanya kazi katika tamthilia zilizoagizwa na programu za China, lakini anasema sasa anafanya kazi na majukwaa ya Marekani, huduma za kimataifa za utiririshaji na kampuni za Uingereza, baada ya tasnia ya microdramas nchini China kuelekeza nguvu zake katika utayarishaji kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba (AI).
Watayarishaji wa filamu katika kampuni ya Black Swan wanafanya maandalizi ya mwisho ya microdrama yao ya kwanza, simulizi ya uchunguzi wa mauaji yenye vipindi 50, iliyorekodiwa mwezi Julai.
Kwasasa, Uingereza ndiyo nchi yenye watazamaji wengi zaidi wa microdrama barani Ulaya. Huku mashabiki wengi na watayarishaji katika tasnia hiyo wakifurahishwa na mustakabali wa aina hii ya burudani, pia kuna wanaoikosoa.
Baadhi ya wakosoaji wanazibeza microdrama wakisema ni maudhui yasiyo na ubora yanayoharibu uwezo wa watu wa kuzingatia jambo kwa muda mrefu. Katika makala ya maoni iliyochapishwa na gazeti la The Guardian, mwandishi mmoja alizitaja tamthilia hizo kuwa "maudhui yasiyo na maana kabisa na ambayo kwa hakika hayana ubora".
Hata hivyo, Jen Cooper, ambaye alianza kama shabiki wa microdrama kabla ya kuwa mshauri katika tasnia hiyo, anasema: "Hakuna anayesema kwamba hizi ni kazi zenye ujumbe wa kina. Lakini ikiwa zimekugusa kihisia, zimemfanya mtu atabasamu au kumrahisishia mtu siku ngumu, basi bila shaka hilo ni jambo zuri la kusherehekea."
Imetafsiriwa na Elizabeth Kazibure