Canada yaja na mpango mpya wa kupokea wahamiaji 5,500: Watanzania, Wakenya kunufaika?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Canada imezindua mpango mpya wa uhamiaji unaolenga kuwapa watu 5,500 kutoka nchi mbalimbali duniani nafasi ya kupata ukaazi wa kudumu, hatua inayoweza kuwa fursa kwa Watanzania, Wakenya na raia wengine wa Afrika Mashariki wanaotafuta maisha nje ya nchi.

Mpango huo unalenga zaidi wafanyakazi wenye ujuzi wanaoweza kujaza nafasi za ajira katika maeneo ya pembezoni mwa miji mikubwa ya Canada, ambako kuna upungufu wa wataalamu katika sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa serikali ya Canada, programu hiyo itaanza Januari 1, 2027, na itatoa nafasi kwa wahamiaji kuishi na kufanya kazi katika jamii zinazoshiriki mpango huo.

Kwa Watanzania na Wakenya wanaofikiria kuhamia Canada, jambo la kuzingatia ni kwamba mpango huo hauwahusu watu wenye nia ya kuhamia tu, bali unalenga zaidi wale wenye taaluma, uzoefu wa kazi na uwezo wa kupata ajira nchini humo.

Fursa kwa Watanzania na Wakenya

Canada haijaweka wazi idadi ya nafasi zitakazokwenda kwa kila nchi, wala hakuna mgao maalumu uliotangazwa kwa Afrika.

Hata hivyo, Watanzania na Wakenya wanaweza kuomba kama waombaji kutoka nchi nyingine, iwapo watatimiza masharti ya programu hiyo.

Miongoni mwa maeneo yatakayopokea wahamiaji ni Pictou County, North Bay, Sudbury, Timmins, Thunder Bay, Brandon na Moose Jaw.

Maeneo hayo yako mbali na miji mikubwa inayovutia wahamiaji wengi kama Toronto na Vancouver, lakini yanakabiliwa na mahitaji ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali.

Sifa zinazohitajika ni zipi na kwanini Canada inahitaji wahamiaji?

Mtu anayetaka kutumia fursa hiyo anahitaji kuwa na ofa ya kazi kutoka kwa mwajiri aliyeidhinishwa katika mojawapo ya maeneo yanayoshiriki programu hiyo.

Pia anatakiwa kuwa na angalau mwaka mmoja wa uzoefu wa kazi unaohusiana na nafasi anayoomba, ndani ya miaka mitatu iliyopita.

Masharti mengine ni pamoja na kuwa na kiwango kinachotakiwa cha ujuzi wa Kiingereza au Kifaransa, elimu inayotambulika Canada na fedha za kujikimu wakati wa kuanza maisha nchini humo.

Mwombaji pia anahitaji kupata pendekezo kutoka katika jamii inayoshiriki programu hiyo kabla ya kuomba ukaazi wa kudumu.

Kwa nini Canada inawatafuta wahamiaji? Wengi wanaweza kujiuliza swali hili.

Sababu kubwa ni upungufu wa wafanyakazi katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, hasa yale yaliyo nje ya miji mikubwa.

Sekta kama afya, elimu na huduma nyingine zinahitaji wataalamu zaidi, lakini si rahisi kuvutia wafanyakazi wa kutosha kutoka maeneo mengine ya Canada.

Kupitia mpango huo, serikali inatarajia kuwavutia wahamiaji wenye ujuzi watakaosaidia kujaza nafasi hizo na wakati huohuo kuchangia maendeleo ya jamii watakakokwenda kuishi.

Kwa Watanzania na Wakenya wanaotamani kufanya kazi Canada, hii ni fursa inayoweza kuangaliwa, lakini kupata ukaazi wa kudumu hakutakuwa jambo la moja kwa moja. Kwanza wanahitaji kukidhi masharti ya mpango wenyewe ama programu husika na kupata ajira inayokubalika.