Mipira ya vichwa mazoezini kuwa kosa?

    • Author, Katie Gornall
    • Nafasi, BBC Sport correspondent
    • Author, Melissa Sharman
    • Nafasi, BBC Sport senior journalist
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mbunge mmoja nchini Uingereza anaitaka serikali kuweka sheria zitakazodhibiti idadi ya mipira ambayo wachezaji wa soka wanaruhusiwa kupiga kwa vichwa wakati wa mazoezi, kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu madhara ya muda mrefu yanayoweza kutokea kwenye ubongo.

Grahame Morris, mbunge wa chama cha Labour anayewakilisha eneo la Easington, aliwasilisha hoja bungeni Jumanne akiitaka serikali kuchukua hatua za kupunguza idadi ya mipira ambayo wachezaji wanapiga kwa vichwa wakati wa mazoezi.

Tafiti zimebaini kuwa wachezaji wa soka wana uwezekano wa kufariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na kuzorota kwa mfumo wa fahamu (neurodegenerative diseases) kwa kiwango kinachozidi mara tatu na nusu ikilinganishwa na watu wengine kwa ujumla.

Hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni, inayojulikana kama Early Day Motion (EDM), inaeleza kuwa kulinda afya ya ubongo wa wachezaji ni suala muhimu linalohusu afya ya jamii na ustawi wa wanamichezo.

Morris aliiambia BBC Sport kuwa lengo la hoja hiyo ni kuongeza uelewa kuhusu ushahidi unaozidi kuongezeka unaoonyesha uhusiano kati ya kupigwa mara kwa mara kwa kichwa, hususan kwa kupiga mipira ya soka, na hatari kubwa ya kupata magonjwa yanayohusiana na kuharibika kwa mfumo wa fahamu.

Alisema hoja hiyo pia inaitaka serikali kuongeza juhudi katika kuzuia madhara, kutoa elimu na kuweka hatua za kuwalinda wachezaji.

Hoja ya Morris inaunga mkono ombi la kitaifa lililowasilishwa Septemba na shirika la hisani la Head Safe Football. Pia inaitaka serikali kuchukua hatua kadhaa, zikiwemo:

- Kuweka sheria zinazopunguza idadi ya mipira ambayo wachezaji wanaruhusiwa kupiga kwa vichwa mara kwa mara wakati wa mazoezi.

- Kuunda kikosi kazi kinachohusisha wataalamu wa afya, wawakilishi wa wachezaji, wanaharakati na mamlaka za soka ili kuweka kanuni za kuwalinda wachezaji ambazo zitatekelezwa kisheria.

- Kutambua ugonjwa wa Chronic Traumatic Encephalopathy (CTE) kama suala la afya ya umma.

- Kuandaa mpango wa kitaifa wa kulinda afya ya ubongo wa wachezaji.

- Kuongeza elimu na uelewa kuhusu hatari za kupiga mipira kwa kichwa, ikiwemo mashuleni na kupitia mitaala ya somo la elimu ya viungo.

Hoja za Early Day Motion hutumiwa na wabunge kueleza misimamo yao kuhusu masuala mbalimbali na kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wengine.

Hata hivyo, kusainiwa kwa hoja hiyo na idadi yoyote ya wabunge hakumaanishi kuwa lazima itajadiliwa bungeni.

"Miongozo iliyopo haitoshi"

Kwa sasa, tayari kuna baadhi ya hatua zinazodhibiti upigaji wa mipira kwa kichwa katika soka.

Shirikisho la Soka England (FA) limekuwa likitekeleza kwa awamu mpango wa kuondoa matumizi ya mipira ya vichwa katika mechi za soka za ngazi za chini kwa watoto wenye umri wa miaka 11 na chini.

FA pia limetoa mwongozo unaopendekeza wachezaji wa soka la ridhaa wasipige mipira kwa vichwa zaidi ya mara 10 kwa wiki wakati wa mazoezi.

Kwa soka la kulipwa nchini England, klabu zimeelekezwa kupunguza mipira ya vichwa yenye nguvu kubwa hadi isizidi mara 10 kwa wiki wakati wa mazoezi.

Scotland imekwenda hatua zaidi kwa kupiga marufuku mazoezi ya kupiga mipira kwa vichwa siku moja kabla na siku moja baada ya mechi kwa wachezaji wa kulipwa.

Hata hivyo, wanaharakati wanaopigania usalama wa wachezaji, akiwemo Dk Judith Gates, mwanzilishi wa Head Safe Football, wanaamini kuwa miongozo ya hiari haitoshi.

Alisema makocha na wazazi wengi hawafahamu uwepo wa miongozo hiyo au marufuku iliyowekwa, huku wengine wakiwa hawajui sababu za hatua hizo.

Gates aliiambia BBC Sport kuwa kunahitajika ufafanuzi zaidi na vikwazo vilivyo wazi ili kuwalinda wachezaji wa sasa na wa baadaye.

Mume wake, Bill, aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Middlesbrough, alifariki akiwa na ugonjwa wa CTE, ambao ni ugonjwa wa ubongo unaozidi kuathiri uwezo wa ubongo kufanya kazi na unaohusishwa na kupigwa kwa kichwa mara kwa mara.

Gates anakiri kuwa itakuwa vigumu kutekeleza kisheria kiwango maalumu cha idadi ya mipira ambayo mchezaji anaruhusiwa kupiga kwa kichwa.

Waziri Mkuu aunga mkono mpango wa fidia kwa wachezaji wa zamani

Wito wa kuimarisha ulinzi wa afya za wachezaji umeibuka wakati Waziri Mkuu Andy Burnham akitoa wito kwa soka la England kutambua rasmi tatizo la ugonjwa wa shida ya akili (dementia) linalowakabili baadhi ya wachezaji wa zamani.

Katika mahojiano na gazeti la Telegraph, Burnham alipendekeza kuanzishwa kwa mpango wa fidia kwa wachezaji wa zamani walioathirika, unaofanana na mfumo wa fidia unaotolewa kwa wafanyakazi wanaopata magonjwa au majeraha yanayotokana na mazingira ya kazi.

Katika taarifa yake kwa BBC Sport, alisema amezungumza na familia zilizoathirika na magonjwa ya dementia na majeraha ya ubongo, na kusikiliza changamoto walizopitia.

Alisema juhudi na msimamo wa familia hizo katika kuhakikisha suala hilo linachukuliwa kwa uzito ni wa kupongezwa, akiongeza kuwa hawakupaswa kulazimika kupambana kwa muda mrefu ili sauti zao zisikike.

Kauli ya Burnham imekuja baada ya uchunguzi kuhusu vifo vya nyota wa zamani wa England, Nobby Stiles, aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 1966, na beki wa zamani wa Scotland, Gordon McQueen.

Uchunguzi huo ulibaini kuwa kupiga mipira kwa kichwa mara kwa mara kulichangia vifo vyao.

Chama cha Wachezaji Soka wa Kulipwa (PFA) na Ligi Kuu England vilianzisha mfuko wa kusaidia afya ya ubongo wa wachezaji, ambao umekuwa ukitoa takribani pauni milioni moja kila mwaka tangu 2023.

Hata hivyo, wanaharakati wanasema kiasi hicho hakitoshelezi kugharamia mahitaji ya matibabu na huduma za wale walioathirika.

Shirikisho la Soka England (FA) halijatoa mchango wa kifedha katika mfuko huo. Hata hivyo, limesema linaendelea kuwekeza katika tafiti na limeweka miongozo ya usalama kwa soka la kulipwa na lile la ngazi za chini.

Msemaji wa FA alisema, licha ya uhusiano kati ya kupiga mipira kwa kichwa katika soka na afya ya ubongo kwa muda mrefu kuendelea kufanyiwa utafiti wa kisayansi na kitabibu, shirikisho hilo limekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuboresha usalama wa mchezo huo.