Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siri ya utamaduni wa mabusu hadharani Hispania
Nchini Hispania, kubusiana hadharani ni jambo la kawaida katika maisha ya kila siku. Lakini uhuru huo wa kuonesha mapenzi mbele ya watu una historia ya kushangaza inayohusisha ukandamizaji na mapambano ya kudai uhuru.
Kubusiana ni jambo linaloonekana kila mahali nchini Hispania. Kuna busu mbili za mashavuni wakati wa kusalimiana, jambo ambalo ni la kawaida. Lakini pia kuna mabusu ya kimapenzi. Nimewahi kujikuta nikitembea nyuma ya wapenzi wa makamo waliosimama katikati ya barabara yenye shughuli nyingi na kuanza kubusiana. Nimewahi pia kuhisi furaha na kukumbuka ujana nilipowaona vijana wakibusiana katika bustani zilizojaa mwanga wa jua, na kulazimika kupita pembeni ya wapenzi waliokuwa wamelewa kidogo na kujibusu huku fataki zikilipuka katika tamasha la Las Fallas mjini Valencia.
Hata mhasibu wangu humalizia barua pepe zake kwa neno besos (mabusu).
Baada ya kuishi nchini Hispania kwa zaidi ya miaka sita, nimezoea kuona watu wakioneshana mapenzi hadharani. Hata hivyo, rafiki yangu aliyerejea Valencia baada ya safari ya Japan aligundua jambo hilo mara moja. Alipotoka tu katika kituo cha treni, alikutana na wapenzi waliokuwa wakibusiana kwenye benchi. Baada ya kukaa nchini ambako watu hawaoneshi mapenzi hadharani mara kwa mara, tukio hilo lilimfanya ajisikie amerejea nyumbani.
"Hatimaye, nimerudi nyumbani," alijiambia.
Jambo hilo lilinifanya nijiulize: Je, kweli Hispania ni nchi ya watu wanaopenda kubusiana? Na tabia hii ya kuoneshana mapenzi hadharani inaweza kutueleza nini kuhusu utamaduni, historia na mitazamo ya watu kuhusu ukaribu wa kimapenzi?
Huenda sababu moja ikawa namna Wahispania wanavyotumia maeneo ya wazi. Katika maeneo mengi ya nchi hiyo, shughuli za kila siku hufanyika nje, katika mitaa yenye pilikapilika, mikahawa na bustani.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Warwick ulibaini kuwa Hispania ni miongoni mwa nchi ambazo watu wake huhitaji umbali mdogo zaidi wanapokutana na mtu wanayefahamiana naye kwa mara ya kwanza. Umbali huo ni mdogo hata ukilinganisha na nchi nyingine za kusini mwa Mediterania kama Ugiriki, Italia na Ureno.
Tabia hiyo inaonekana katika viwanja vya umma vya Hispania, ambako maeneo ya nje ya mikahawa hujaa marafiki wanaokaa karibu kwa karibu huku wakinywa cañas (bia) kwenye mwanga wa jua.
Amparo Lasén, profesa wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Complutense cha Madrid, anasema watu nchini Hispania huwa na mazoea zaidi ya kuonesha hisia zao kupitia mgusano wa kimwili ikilinganishwa na watu wa kaskazini mwa Ulaya.
"Tofauti inaonekana zaidi unapolinganisha na nchi za Nordic au Uingereza," alisema.
Huenda si kwamba Wahispania wana upendo zaidi kuliko watu wa mataifa mengine, bali wana uhuru zaidi wa kuuonesha. Kubusiana hadharani si lazima kuwe ishara kubwa ya mapenzi; ni sehemu tu ya maisha yao ya kawaida.
Namna watu wanavyoishi katika makazi yao inaweza pia kuwa na mchango. Takribani asilimia 65 ya wakazi wa Hispania wanaishi katika nyumba za ghorofa, kiwango cha juu zaidi katika Umoja wa Ulaya. Wakati huohuo, kupanda kwa bei ya nyumba kumefanya iwe vigumu zaidi kwa vijana kujitegemea na kuondoka katika nyumba za familia zao.
'Huenda jambo la kushangaza zaidi kuhusu kubusiana nchini Hispania ni kwamba limekuwa jambo la kawaida kiasi kwamba halishangazi tena.'
Lasén anasema ukosefu wa faragha nyumbani unaweza kuwafanya watu kutafuta maeneo ya umma kwa ajili ya kuwa na muda wa faragha na wapenzi wao.
"Nchini Hispania tuna changamoto ya upatikanaji wa nyumba, jambo linalotufanya tuzoee zaidi kukutana na marafiki nje ya nyumba, kwenda kwenye baa na mikahawa badala ya kukutana majumbani," anasema.
Anaongeza kuwa wapenzi sasa hulazimika kutafuta benchi lililojitenga ili kupata muda wa kuwa pamoja, ingawa si lazima wawe peke yao kabisa.
Hata hivyo, Lasén anasema changamoto ya makazi si sababu kuu ya watu kuoneshana mapenzi hadharani. Jambo muhimu zaidi ni mtazamo uliolegea wa jamii kuhusu tabia hiyo.
"Kama hakuna anayekutazama vibaya au kama hujali watu wanavyokuangalia, basi hilo ndilo linalorahisisha watu kuoneshana mapenzi hadharani."
Isabel Nieto Tous, mwenye umri wa miaka 28, ambaye alirejea kuishi na wazazi wake miaka mitatu iliyopita baada ya kukaa nje ya nchi, anafahamu changamoto za kuwa katika mahusiano bila kuwa na faragha ya kutosha.
"Sikutaka kuwaambia wazazi wangu kwamba nilikuwa nakaa nyumbani kwa watu niliokuwa nikikutana nao kimapenzi kwa sababu ilikuwa inatia aibu kidogo. Kwa hiyo nilikuwa nawaambia kwamba nakaa kwa rafiki yangu," alisema.
Tous, ambaye amewahi kuishi Japan, Ufaransa, Ujerumani na Tunisia, anaamini kuwa mahusiano ya kimapenzi nchini Hispania yana tofauti yake. Anasema kuna hali ya ukaribu na uchangamfu inayojitokeza tangu mwanzo wa mahusiano.
"Watu wanakuwa karibu sana na wanapenda kugusana haraka. Huenda uko katika mahusiano ambayo bado hayajaeleweka vizuri, umekutana na mtu mara mbili tu, lakini tayari mnashikana mikono hadharani na kugusana sana," anasema.
"Nadhani kwa ujumla, kubusiana hadharani kunakubalika sana," anaongeza. "Hakuna tofauti kati ya namna watu wanavyojiendesha ndani ya nyumba na nje. Watu wanaonesha hisia zao kwa namna ileile katika maeneo ya faragha na maeneo ya wazi."
Ingawa leo hii kuoneshana mapenzi hadharani ni jambo la kawaida nchini Hispania, hapo awali maonesho ya mapenzi na ujinsia yalikuwa yakidhibitiwa vikali.
Wakati wa utawala wa kidikteta wa Francisco Franco (1939-1975), misingi ya kihafidhina ya Kanisa Katoliki na sheria kali zilidhibiti mwenendo wa watu katika jamii. Ushoga ulihalalishwa kuwa kosa la jinai na maonesho ya mapenzi hadharani yalidhibitiwa.
Wapenzi wangeweza hata kutozwa faini kwa kubusiana hadharani.
Baada ya kifo cha Franco mwaka 1975, Hispania ilipitia mabadiliko makubwa ya kitamaduni. Katika mji wa Madrid, vuguvugu la utamaduni wa vijana lililojulikana kama La Movida Madrileña lilisherehekea uhuru na kujieleza bila woga.
Watengenezaji wa filamu kama Pedro Almodóvar walipinga misingi ya kihafidhina iliyokuwa imetawala hapo awali. Kadiri vuguvugu hilo lilivyoendelea kukua, maonesho ya mapenzi na ujinsia yalizidi kuonekana katika maisha ya umma.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakujitokeza yenyewe. Wanaharakati wa haki za watu wa LGBT walikuwa wamekuwa wakipigania haki zao kwa miaka mingi, na hivyo kuweka msingi wa jamii iliyo wazi na yenye kukubali tofauti za watu.
Moja ya maandamano muhimu yalifanyika mjini Madrid Februari 23, 1987. Mwaka mmoja kabla, wanawake wawili walikuwa wamekamatwa kwa kubusiana katika eneo la Puerta del Sol mjini Madrid na kushikiliwa na polisi kwa siku mbili chini ya sheria iliyojulikana kama Escándalo Público (Sheria ya Kashfa ya Umma).
Kukamatwa kwao kulichochea makundi ya wanaharakati wa eneo hilo kuandaa maandamano ya watu kubusiana hadharani ili kupinga hatua hiyo.
Kuanzia mwaka huo hadi takribani miaka ya 1990, kila maandamano ya Pride yaliyofanyika Madrid yalikuwa yakihitimishwa kwa tukio la watu kubusiana katika eneo la Puerta del Sol.
Kubusiana mitaani kulikuwa kumebadilika na kuwa njia yenye nguvu ya maandamano ya amani, na sheria iliyotumika kuwatuhumu watu kwa kusababisha kashfa ya umma ilifutwa mwaka 1988.
Leo hii, maonesho ya mapenzi hadharani yanaonekana katika maeneo mbalimbali ya Hispania, lakini si kila mtu anafurahia uhuru huo kwa kiwango sawa.
Lasén anasema wapenzi wa umri mkubwa wanaobusiana kwenye benchi la umma wanaweza kuvutia macho ya watu zaidi, huku wapenzi wa jinsia moja wakikabiliwa na uchunguzi na hukumu kali zaidi kutoka kwa jamii.
"Si kila mtu anajisikia huru kwa kiwango sawa kuonesha uhusiano wake hadharani," alisema.
Kwa Paula Furió, aliyekuwa mpiga picha wa harusi mjini Valencia, kubusiana ni ishara ya jambo kubwa zaidi.
"Bado kuna kazi ya kufanya, lakini kwa ujumla jamii ya Hispania iko wazi sana. Kubusiana ni kama sehemu ndogo tu ya jambo kubwa zaidi: kunakupa taswira ya uhuru unaoweza kuwa nao nchini Hispania. Ni namna ya kuonesha uhuru," alisema.
Jambo hilo lilinikumbusha tena rafiki yangu aliyerejea kutoka Japan na furaha aliyohisi baada ya kumuona wanandoa wakibusiana kwenye benchi.
Huenda hakufurahia tu kurejea nyumbani, bali pia kurejea katika nchi ambako kuwa halisi na kujieleza kwa uhuru kunapewa nafasi kubwa kuliko kufuata taratibu za kijamii.
Labda jambo la kushangaza zaidi kuhusu kubusiana nchini Hispania ni kwamba limekuwa jambo la kawaida kiasi kwamba halishangazi tena.