Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maswali matano ya kisheria kuhusu rufaa ya Lissu
Baada ya kukabiliwa na shtaka la uhaini kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, aliachiliwa huru kwa shtaka hilo Novemba 6, 2026, lakini Mahakama Kuu ikamtia hatiani kwa kosa la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.
Uamuzi huo wa jopo la majaji watatu umeibua mjadala miongoni mwa wanasheria kuhusu matumizi ya sheria, mamlaka ya mahakama, haki ya mshtakiwa kujitetea na aina ya adhabu iliyotolewa.
Lissu alishtakiwa kwa uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Hata hivyo, Mahakama ilisema upande wa mashtaka haukuthibitisha nia inayohitajika kisheria kwa kosa hilo, lakini ushahidi uliowasilishwa ulitosha kuthibitisha kosa la uchochezi chini ya kifungu cha 390 cha sheria hiyo.
Katika kutoa uamuzi huo, Mahakama ilitumia kifungu cha 319(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinachoruhusu mtu kutiwa hatiani kwa kosa dogo linalotokana na shtaka kubwa hata kama hakushtakiwa moja kwa moja kwa kosa hilo.
Hata hivyo, wakili wa Lissu, William Maduhu, amesema timu ya utetezi ina zaidi ya sababu 10 zinazoweza kuibua hoja katika rufaa, zikiwemo mamlaka ya Mahakama Kuu kusikiliza kosa la uchochezi na haki ya Lissu kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.
Wakati wanasheria wakiendelea kutoa tafsiri tofauti kuhusu matumizi ya vifungu hivyo, maswali matano ya kisheria yanaibuka katika mjadala kuhusu rufaa yake.
1. Je, Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kumtia hatiani kwa uchochezi?
Moja ya hoja zinazoweza kujitokeza katika rufaa ni mamlaka ya Mahakama Kuu kumtia Lissu hatiani kwa kosa la uchochezi, wakati shtaka lililokuwa mbele yake ni la uhaini.
Wakili William Maduhu, ambaye alisaidia timu ya utetezi katika utafiti wa kesi hiyo, amesema moja ya hoja wanazotaka kuziwasilisha katika rufaa ni kama Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kosa la uchochezi ambalo kwa tafsiri yao lilipaswa kuanza kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Hoja hiyo inaibua mjadala kuhusu mipaka ya mamlaka ya mahakama na utaratibu unaopaswa kufuatwa pale ambapo ushahidi katika kesi moja unaibua uwezekano wa kosa jingine.
Wakili Peter Madeleka anasema Lissu alishtakiwa kwa uhaini na si uchochezi, hivyo uamuzi wa kumtia hatiani kwa kosa ambalo halikuwa shtaka lake la awali unahitaji kuchunguzwa kisheria.
"Lissu alishtakiwa kwa uhaini, hakushtakiwa kwa uchochezi. Mahakama imesema Lissu hana kosa lolote ndiyo maana ikamuachia kwa uhaini," anasema Madeleka.
Hata hivyo, wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa, Nathaniel Maseke, ana mtazamo tofauti kuhusu mamlaka ya mahakama kutumia kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Anasema kifungu hicho kinaipa mahakama mamlaka ya kumtia mtu hatiani kwa kosa dogo hata kama hakushtakiwa moja kwa moja kwa kosa hilo, iwapo ushahidi utathibitisha kuwa alilitenda.
"Huwezi ukamshtaki mtu kwa kosa kubwa na kosa dogo kwa wakati mmoja," anasema Maseke, akieleza kuwa sheria ina utaratibu wa kushughulikia mazingira ambayo ushahidi unashindwa kuthibitisha kosa kubwa lakini unaonyesha kuwepo kwa kosa dogo.
Pamoja na kauli hii, Lissu ana kesi ingine ya uchochezi kwneye Mahakama ya Kisutu. Wakili Fulgence Massawe anasema kwa uamuzi wa Mahakama kuu ni kama kesi ya Kisutu imekufa kibudu; "kisheria huwezi kuhukumiwa mara mbili kwa kosa hilo hilo, kwa hiyo kwa maamuzi ya Mahakama kuu imeshafuta shauri la Kisutu".
2. Je, Lissu alipewa haki ya kujitetea dhidi ya shtaka la uchochezi?
Hili ni swali jingine linalohusu haki ya kusikilizwa na nafasi ya mshtakiwa kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hoja ya utetezi ni kwamba Lissu alijiandaa kujibu shtaka la uhaini, lakini hakujulishwa mapema kuwa angeweza kutiwa hatiani kwa uchochezi.
Maduhu amesema hoja yao ni kwamba Lissu hakupewa muda wa kutosha kuandaa utetezi dhidi ya kosa ambalo hatimaye alikutwa nalo na hatia.
Wakili Peter Madeleka anaunga mkono mjadala huo akisema:
"Mahakama imeanzisha kesi ya uchochezi halafu haimpi haki ya kusikilizwa, kwa maana ya kuleta mashahidi ili ajitetee kwamba je, alichochea watu ama hakuchochea."
Hoja hii inagusa suala la kama mshtakiwa anapaswa kupewa nafasi ya kujua na kujibu kosa ambalo mahakama inazingatia kabla ya kutoa hukumu.
Kwa upande mwingine, katika uamuzi wake, Mahakama ilisema ilikuwa imezingatia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili na kwamba Lissu alikuwa na nafasi ya kujibu mazingira yaliyohusishwa na kosa la uchochezi.
Hivyo, mjadala wa kisheria unaohitaji kuangaliwa ni kama utetezi aliokuwa nao katika kujibu shtaka la uhaini ulihusisha pia vipengele vya kosa la uchochezi, au kama kulikuwa na haja ya kumpa nafasi nyingine maalumu ya kujitetea.
3. Je, uchochezi unaweza kuwa kosa dogo linalotokana na shtaka la uhaini?
Hili ni mojawapo ya masuala yenye mitazamo inayotofautiana zaidi miongoni mwa wanasheria waliozungumzia hukumu hiyo.
Mahakama ilitumia kifungu cha 319(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambacho kinaruhusu mtu kutiwa hatiani kwa kosa dogo pale ambapo shtaka lina vipengele kadhaa, baadhi yake vikithibitishwa kuwa vinaunda kosa jingine dogo.
Hata hivyo, wakili Edson Kilatu anahoji kama kosa la uchochezi lina uhusiano wa kisheria unaolifanya kuwa kosa dogo linalotokana na uhaini.
"Hapakuwepo na mazingira ya kuifanya uchochezi ni cognate (kosa la familia moja na uhaini). Kwa maoni yangu, uhaini halina mdogo wake, halina pacha, linajitegemea lenyewe," anasema Kilatu.
Anaongeza kuwa makosa hayo yako katika sehemu tofauti za Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
"Ndo maana waliotengeneza sheria hii wakaona kosa la uhaini likae sura ya saba ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, hili jingine la uchochezi likae sura ya 46. Makosa haya hayapo familia moja," anasema.
Wakili Peter Madeleka pia anahoji kama uhaini unaweza kuwa na kosa dogo la uchochezi kwa kuangalia msingi wa kisheria ulioanzisha kosa hilo.
"Kosa dogo ni uchochezi, kosa kubwa ni uhaini, je, kosa la uhaini kisheria lina kosa dogo?" anauliza.
Lakini Nathaniel Maseke anatoa mfano tofauti kueleza kwa nini sheria inaweza kuruhusu mahakama kubadilisha hukumu kutoka kosa kubwa kwenda kosa dogo.
"Kwa mfano ukiwa na kosa la mauaji, tukienda ku-establish zile element za kosa la mauaji, tukazikosa, ni rahisi sana wewe kuangukia kwenye kosa la kuua bila kukusudia. Makosa haya yanaangukia kwenye familia moja," anasema.
Kwa maelezo yake, kifungu cha 319 kinaipa mahakama mamlaka ya kumtia mtu hatiani kwa kosa dogo iwapo ushahidi uliotolewa katika shauri unathibitisha kuwa kosa hilo lilifanyika.
Hata hivyo, kuhusu swali kama uhaini na uchochezi yana uhusiano unaokidhi masharti ya kifungu hicho, Maseke anasema ni suala linalopaswa kujadiliwa ndani ya mahakama.
"Nimesema hivi kwa sababu mimi ninaheshimu Ibara ya 107(a) na (b) ya Katiba yetu. Tunaposema uhuru wa Mahakama, wengi tunadhani ni pale ambapo muhimili mmoja wa nchi unaamua kuingilia maamuzi ya muhimili mwingine, lakini hata mimi ninaweza kuingilia maamuzi kwa kusema inatakiwa iwe hivi," anasema akihojiwa na Jambo TV kama ilivyo kwa Wakili Kilatu.
Tofauti hizi za tafsiri zinaweka mbele swali la msingi: Je, masharti ya kifungu cha 319(1) yalitimia katika mazingira ya kesi ya Lissu?
4. Je, ushahidi ulithibitisha kosa la uchochezi?
Tofauti kati ya kuachiwa huru kwa uhaini na kutiwa hatiani kwa uchochezi pia imeibua maswali kuhusu namna ushahidi ulivyotafsiriwa na mahakama.
Katika hukumu yake, Mahakama ilisema upande wa mashtaka haukuthibitisha nia ya uhaini iliyokuwa ikihitajika kisheria, lakini ushahidi wa kauli za Lissu na maelezo ya mashahidi ulithibitisha kosa la uchochezi.
Kwa mujibu wa taarifa za hukumu hiyo, baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka walieleza kuwa kauli za Lissu ziliwaathiri na kuwafanya washiriki katika vitendo vilivyolenga kuvuruga uchaguzi wa mwaka 2025.
Mahakama ilisema ilikuwa imeridhika kwamba ushahidi wa pande zote mbili ulithibitisha kosa la uchochezi chini ya kifungu cha 390 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Kifungu hicho kinahusu mtu anayemshawishi au kumchochea mwingine kutenda kosa, bila kujali kama ushawishi au uchochezi huo ulizaa matokeo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo, ili hoja hii ichunguzwe kwa upana, kuna maswali ya kisheria yanayohitaji kujibiwa: Ni vipengele gani hasa vya kosa la uchochezi vilipaswa kuthibitishwa? Je, kauli zilizotolewa zilitimiza vipengele hivyo? Na kuna tofauti gani kati ya kauli kali za kisiasa na kauli zinazokidhi vigezo vya kosa la uchochezi?
Hapa, si suala la kuamua upya ushahidi uliosikilizwa na Mahakama Kuu, bali ni kuchunguza kama tafsiri ya ushahidi huo ilikidhi masharti ya kisheria ya kosa ambalo Lissu alipatikana nalo na hatia.
5. Kwa nini kifungo cha miaka minne badala ya faini?
Uamuzi wa Mahakama Kuu kumhukumu Lissu kifungo cha miaka minne badala ya faini ni eneo jingine linaloweza kujadiliwa katika rufaa.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa hukumu, kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezekano wa kifungo kisichozidi miaka mitano, faini au adhabu zote mbili kwa kosa husika.
Wakili Peter Madeleka anasema pale ambapo sheria inaruhusu faini na kifungo, mahakama inapaswa kuangalia uwezekano wa faini na kumbukumbu za awali za mshtakiwa kabla ya kuamua aina ya adhabu.
"Mahakama inaanza kuangalia faini, na akishindwa kulipa faini ndiyo anakwenda gerezani. Na kabla ya hapo lazima iangalie kwanza kumbukumbu za kihalifu za huyu mshtakiwa, je, aliwahi kutwa hatiani?" anasema.
Anasema mazingira ya mshtakiwa na historia yake ya makosa yanapaswa kuzingatiwa katika uamuzi wa adhabu.
Katika kesi ya Lissu, taarifa za hukumu zinaonyesha kuwa upande wa mashtaka ulikiri kuwa hakuwa na hukumu za awali za makosa ya jinai. Hata hivyo, uliomba apewe adhabu kali kwa kuzingatia uzito wa kosa na athari zinazoweza kutokana na uchochezi.
Mahakama nayo ilisema ilizingatia hoja za pande zote mbili, ikiwemo kutokuwa na kumbukumbu za makosa ya awali na hali ya afya ya Lissu. Hata hivyo, ilieleza kuwa mazingira ya kosa na uzito wake yalihalalisha adhabu ya kifungo badala ya faini.
Kwa vyovyote vile, kama mjadala umekuwa mkubwa sasa kwenye jamii baada ya mahakama kutoa hukumu, na haya maswali matano yanao ngeza mjadala zaidi. Kwa sasa mcvhakato wa rufaa ya Lissu unaendelea, huenda sasa mjadala huu ukahamia ndani ya Mahakama, ukiwa na sura ya kisheria zaidi.