Mambo 4 kuhusu kashfa ya "mikataba ya ngono" inayomkabili aliyekuwa rais wa Colombia, Gustavo Petro

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Gustavo Petro yuko katikati ya dhoruba ya kisiasa na ya vyombo vya habari kutokana na madai yaliyotolewa na mwanamke mmoja, anayedai kuwa alipata mikataba ya serikali kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na kiongozi huyo.

Suala hilo lililipuka mnamo tarehe 25 Oktoba. Deicy Jiménez, ambaye hapo awali hakuwa akijulikana kwa umma, alifanya mahojiano ya dakika 22 na mwandishi wa habari Vicky Dávila mkurugenzi wa Revista Semana, aliyewahi kugombea urais, ambaye pia ni mpinzani wa Petro.

Katika kauli hiyo, alidai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Petro, na kwamba alipewa kazi na taasisi kadhaa za serikali kabla na wakati wa kipindi cha urais wake.

Pia alidai kuwa yeye hakuwa peke yake. Kwa mujibu wa maelezo yake, kulikuwa na mtandao wa "wanawake kati ya 30 na 40" ambao walinufaika na mikataba ya serikali pamoja na nafasi mbalimbali, kwa kubadilishana na "kuongozana" na rais huyo wa zamani kwenda kwenye "sherehe za ngono."

Kwa sasa, hakuna ushahidi kutoka kwa wanawake wengine wala ushahidi wowote unaothibitisha kuwepo kwa mtandao wa aina hiyo.

Baada ya mahojiano hayo, Jiménez alichapisha video kwenye mitandao yake ya kijamii ambayo kuthibitisha kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Petro.

Rais huyo wa zamani hakatai uhusiano wake na mwanamke huyo, lakini anakataa vikali madai ya kutoa mikataba ya serikali kwa ajili ya ngono.

"Ningejitapikia mwenyewe endapo ningewahi kufanya jambo la Kijinga namna hiyo," alieleza katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya X.

Petro anadai kuwa hili ni operesheni iliyoanzishwa na serikali ya De la Espriella na kuashiria kuwa Jiménez alilipwa ili kutoa kauli hizo.

Kufuatia ushuhuda wa mwanamke huyo na video hiyo, uchunguzi tayari umeanza dhidi ya rais huyo wa zamani katika mamlaka mbalimbali za kisheria.

Zifuatazo ni hoja kuu 4 za sakata hilo, lililopewa jina na vyombo vya habari vya Colombia kama "mikataba ya ngono".

1. Shutuma kuhusu kinachodaiwa kuwa "mikataba ya ngono"

Kwa mujibu wa ushahidi alioutoa katika jarida la *Semana*, Deicy Jiménez alikutana na Petro kupitia jukwaa la uanamitindo wa mtandaoni (webcam modeling). "Alionekana kama mteja mwingine tu," alisema.

Inasemekana kuwa Petro alijitambulisha kwa jina bandia, lakini wakati fulani aliwasha kamera yake na Jiménez akamtambua.

Mwanamke huyo kijana alisema kuwa, baada ya mwezi mmoja, walikubaliana kukutana ana kwa ana katika hoteli moja jijini Cali na wakaanzisha uhusiano wa kimapenzi.

Baadaye, alihamia Bogotá. Alisema kuwa hapo ndipo alipoanza kunufaika na mikataba na taasisi za serikali, ingawa hakufafanua ikiwa Petro alimpa mikataba hiyo kabla au baada ya kukutana naye kimapenzi.

Jiménez alidai kuwa "wanawake kadhaa" walikuwa na makubaliano na Petro kama yake; kwa maneno yake mwenyewe, "kati ya 30 na 40."

"Sote tunajua mambo mengi," alisema.

Kauli hizi zinakuja siku chache baada ya malalamiko dhidi ya Petro kuwasilishwa bungeni na mkurugenzi wa sasa wa Idara ya Utawala ya Ofisi ya Rais (DAPRE), Carlos Ríos.

Ríos, ambaye ni mmoja wa watu wa karibu na Rais Abelardo de la Espriella, alizungumzia "wanawake 48 ambao rais wa zamani Gustavo Petro aliwaweka katika Ofisi ya Rais, na kwa bahati mbaya akawatumia kama nyenzo kupitia mikataba ya utoaji huduma (OPS)."

Kufuatia kauli hizo na mahojiano na Deicy Jiménez, wakili wa Petro alimshtaki Carlos Ríos mbele ya Ofisi ya Mwendesha mashtaka, akidai kuwa alipanga njama ya kutengeneza ushahidi wa uongo kutoka kwa wanawake dhidi ya Petro.

Awali, Angie Rodríguez, aliyekuwa mkurugenzi wa DAPRE wakati wa utawala wa Petro, naye alizungumza katika mahojiano kuhusu madai ya kuwepo kwa mtandao wa ukahaba katika Ikulu (Casa de Nariño).

Kuhusu Rodríguez, Petro amesema kuwa ni mtu mwenye matatizo ya akili (psychotic).

2. Ushahidi unaodaiwa kujulikana

Katika mfumo wa Secop II (Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma), kuna mikataba 10 ya utoaji huduma iliyosainiwa na Deicy Jiménez na taasisi tatu za Serikali.

Mikataba hiyo ilisainiwa kati ya mwaka 2021 na 2026, na thamani yake jumla ni pesa za Colombia 126,544,432 (takriban Dola za Marekani 38,000 kwa kiwango cha sasa cha kubadilisha fedha).

Baadhi ya maelezo yaliyotolewa na Jiménez katika ushahidi wake yanaendana na taarifa zilizomo kwenye mikataba hiyo, lakini mengine hayalingani.

Kwa mfano, anasema kwamba alipofika Bogotá alianza kufanya kazi katika Seneti. Kwa hakika, mkataba wa kwanza uliopo kwenye kumbukumbu ni taasisi hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo yake, hilo lilitokea mwaka 2019, lakini mkataba huo una tarehe ya Julai 29, 2021.

Ili kuweka muktadha, kati ya mwaka 2018 na 2022, Gustavo Petro alikuwa seneta.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Jiménez, hakufanya kazi moja kwa moja na Petro katika Seneti, bali alifanya kazi na Seneta Maria José Pizarro, ambaye ni mwanachama mwenzake wa chama na mshirika wa karibu wa rais huyo wa zamani.

Mwanamke huyo alieleza kuwa baadaye alikuwa na mikataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Ulinzi na Usalama wa Kibinafsi (Superintendency of Surveillance and Private Security), pamoja na Wizara ya mambo ya ndani, kama ilivyoandikwa katika mfumo wa Secop II.

Taasisi hizo mbili ni sehemu ya Utendaji, na Jiménez aliajiriwa huko hasa wakati Petro akiwa rais, ambaye ndiye mamlaka ya juu zaidi ya kiutendaji.

Mkataba wa hivi karibuni zaidi uliopo kwenye kumbukumbu ulisainiwa Januari 21 mwaka huu na bado unaendelea kutekelezwa. Mkataba huo unaelekeza malipo ya kila mwezi kwa Deicy Jiménez ya pesa za Colombia 2,648,443 (Dola za Marekani 800) kwa kipindi chote cha mwaka 2026.

Haijabainishwa wazi ikiwa Jiménez bado anaendelea kupokea fedha kutoka kwa Serikali.

Taarifa inayofahamika kufikia sasa kuhusu uhusiano unaodaiwa kuwepo kati ya Jiménez na rais yanatokana na video iliyochapishwa na yeye mwenyewe, pamoja na video nyingine iliyotolewa na mwandishi wa habari D'Arcy Quinn.

Video ya kwanza inaonekana kuwaonyesha Petro na Jiménez wakiwa ndani ya chumba. Petro anavaa koti na Jiménez anamwambia, "Unaonekana nadhifu sana pia." Petro anajibu, "Je, unafikiri hivyo?" Mazungumzo hayo kisha yanaelekea kwenye kifaa cha kujitosheleza kingono ambacho hakionekani kwenye video hiyo, na kisha rais huyo wa zamani anamshika Jiménez kichwani na kumbusu.

Deicy Jiménez aliweka video hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram akisema: "Ninaweka video hii kama ushahidi kwamba ninasema ukweli."

Video nyingine ni rekodi ya kile kinachoonekana kwenye skrini inayodhaniwa kutoka kwenye simu ya Jiménez wakati wa kile kinachodaiwa kuwa ni mazungumzo ya video na Petro.

Kwa mujibu wa rekodi hiyo, Petro, akitumia jina bandia, anazungumza na Jiménez: "Unapendeza sana. Simama." Pia anamtumia busu la hewani na kumpa ishara ya kunyamaza kimya.

BBC News Mundo haikuweza kuthibitisha kwa njia huru video hizo au mazungumzo yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ambayo yanadaiwa kufanyika kati ya Jiménez na akaunti bandia zinazosimamiwa na Petro.

3. Wasemayo Petro na kundi lake

Petro amekanusha shutuma za Jiménez na ameomba kuheshimiwa kwa faragha yake.

"Sijawahi kutoa mkataba kwa ajili ya kupata mahusiano ya kimapenzi," alisema katika taarifa iliyochapishwa siku hiyo hiyo ambapo ushahidi wa mwanamke huyo ulijulikana.

Aliongeza: "Kusaidia wanawake maskini, akina mama wasio na waume, na wafanyabiashara ya ngono kuwa na chaguzi tofauti za maisha (...) ni tofauti sana na kupeana mkataba ili kubadilishana na ngono."

"Uhusiano wangu wa kimapenzi hauhusu matumizi ya madaraka, bali unahusu utafutaji wa upendo."

Hivi karibuni zaidi, alidai kuwa hakuwahi kukutana na Deicy Jiménez wakati akiwa rais. "Je, video ya takribani miaka nane iliyopita ni ushahidi?" aliuliza.

Katika malalamiko yake dhidi ya Carlos Ríos, wakili wa utetezi wa Petro anatetea nadharia kwamba kuna operesheni iliyoanzishwa kutoka kwa serikali ya De la Espriella kutengeneza ushahidi kutoka kwa wanawake dhidi ya rais huyo wa zamani.

Chama cha rais wa zamani, kimeunga mkono simulizi hiyo.

"Operesheni ya kufichua maisha yangu ya kibinafsi inatoka kwa serikali ya Abelardo de la Espriella na kuna pesa zinazohusika," Petro alisema katika taarifa yake ya kwanza kuhusu suala hilo hilo.

Jumatatu hii, akinukuu kipande cha simu iliyorekodiwa ambayo anaonekana akipiga busu, rais huyo wa zamani aliandika kwenye akaunti yake ya X: "Sasa busu limekuwa haramu lakini ni la msingi."

Kwa upande wake, seneta wa zamani Maria José Pizarro, mshirika wa karibu wa Petro, alikiri kwamba Deicy Jiménez alifanya kazi katika Seneti alipokuwa makamu wa rais.

Alisema, hata hivyo, hakujua kamwe kwamba Jiménez alikuwa na uhusiano wa karibu na Petro na akasema kwamba hakuwa amebadilishana mkataba kwa "hisani ya aina yoyote".

Aliyekuwa mgombea urais Ivan Cepeda, wa chama chake, alisema katika mahojiano na podcast El Reporte Coronell kwamba tabia ya Petro ambayo imebainika ingechunguzwa na chama.

"Lakini hatutakubali kile wanachotaka kutulazimisha, ambacho ni kuharibu serikali yetu," Cepeda alisema.

4. Uchunguzi

Kutokana na sakata hilo, aina mbalimbali za uchunguzi tayari zinaendelea katika Ofisi ya mwendesha Mashtaka, Mahakama kuu ya haki, na Ofisi ya mwanasheria Mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa alizotoa yeye mwenyewe na kuthibitishwa na vyombo vya habari vya ndani, Deicy Jiménez alikabidhi simu yake ya mkononi kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, ambapo ilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu kwa saa kadhaa.

Anatarajiwa kutoa maelezo kwa chombo hicho Ijumaa hii.

Wakati huo huo, hakimu wa mahakama ya Juu ameagiza kuchunguzwa kwa mikataba ambayo Jiménez alikuwa nayo katika Seneti.

"Bila kujali maelezo binafsi, jambo la msingi hapa ni kubaini kama kuna vipengele vya jinai, hasa kuhusiana na iwapo kulikuwa na mikataba iliyohusisha fedha za umma," Hakimu Carlos Roberto Solórzano aliwaambia waandishi wa habari.

Matukio yaliyotokea kabla ya Petro kuwa rais yanaweza kuchunguzwa kwa mtazamo wa kisheria na jinai na Ofisi ya mwendesha mashtaka pamoja na Mahakama ya Juu.

Mambo yaliyotokea wakati wa muhula wake wa urais yako chini ya mamlaka ya Kamati ya Mashtaka, ambayo inaundwa na wabunge na inajulikana kwa kutopiga hatua kubwa katika uchunguzi.

Licha ya hayo, wabunge wawili kutoka chama tawala cha National Salvation wamewasilisha malalamiko dhidi ya Petro mbele ya kamati hiyo, wakidai kuwa anaweza kuwa "hafai kushika wadhifa huo kutokana na kukosa uadilifu".