Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sayansi yafichua sababu za jicho kucheza
Jicho lako kucheza kunaweza kukukera, lakini mara nyingi si jambo la kuhofia. Hizi ndizo sababu zake.
Hali ya kope la jicho kucheza mara kwa mara inaweza kukera, lakini kwa kawaida si jambo la kuwa na wasiwasi nalo. Hali hii inayojulikana kitaalamu kama myokymia, ni mtikisiko usio na madhara unaohusishwa na uchovu, msongo wa mawazo, matumizi ya kafeini au muda mrefu wa kutazama skrini.
Wakati mwingine, wanawake hujiuliza ikiwa hali hiyo inahusiana na mabadiliko ya homoni. Hata hivyo, ingawa mabadiliko ya homoni wakati wa kipindi cha kuelekea ukomo wa hedhi (perimenopause) yanaweza kusababisha kukaza kwa misuli, wasiwasi na matatizo ya usingizi, mambo ambayo yanaweza kuchangia hali hiyo kwa njia isiyo ya moja kwa moja, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha uhusiano kati ya mabadiliko ya homoni ya estrojeni na kucheza kwa kope la jicho.
Unaweza kuanza kwa kuangalia muda wako wa kulala, kiwango cha msongo wa mawazo na matumizi ya kafeini ili kudhibiti vichocheo hivyo. Hata hivyo, kwa kawaida hali hii huisha yenyewe.
Jicho kucheza ni nini?
Jicho kucheza ni hali ya kope au misuli ya jicho kutikisika au kusinyaa bila mtu kuwa na uwezo wa kudhibiti mwendo huo. Kuna aina mbalimbali za hali hii, na kila aina inaweza kuwa na chanzo tofauti.
Aina inayotokea mara nyingi zaidi inajulikana kama myokymia. Hali hii ni ya kawaida sana na watu wengi huipata angalau mara moja katika maisha yao.
Inaweza kuathiri kope la juu au la chini, lakini kwa kawaida hutokea katika jicho moja kwa wakati mmoja. Mtikisiko huo unaweza kuwa mdogo kiasi cha kutotambulika kwa urahisi au kuwa mkubwa kiasi cha kukera.
Mara nyingi hali hiyo huisha baada ya muda mfupi, ingawa inaweza kujirudia ndani ya saa kadhaa, siku au hata kuendelea kwa muda mrefu zaidi.
Aina nyingine inajulikana kama benign essential blepharospasm. Hali hii huanza kwa mtu kupepesa macho mara nyingi zaidi kuliko kawaida katika macho yote mawili, na baadaye inaweza kusababisha kope kujifunga kwa nguvu.
Aina hii si ya kawaida, lakini inaweza kuwa kali sana na kuathiri shughuli mbalimbali za maisha ya kila siku.
Pia kuna hali inayojulikana kama hemifacial spasm, ambayo huhusisha mtikisiko wa misuli katika upande mmoja wa uso, ukiwemo eneo la kope la jicho. Mtikisiko unaweza kuanza kuzunguka jicho na baadaye kusambaa katika sehemu nyingine za uso.
Nini husababisha jicho kucheza?
Chanzo halisi cha jicho kucheza hakijulikani. Hata hivyo, hali hiyo inaweza kusababishwa au kuchochewa zaidi na mambo mbalimbali, yakiwemo:
- Msongo wa mawazo.
- Kuchoka kwa macho.
- Baadhi ya dawa na vitu vinavyochochea mfumo wa fahamu, ikiwemo kafeini.
- Ukavu au muwasho wa macho.
- Kukosa usingizi wa kutosha.
Dalili za jicho kucheza ni zipi?
Jicho kucheza huathiri misuli ya kope na kusababisha mtikisiko au kupepesa macho bila hiari.
Mtikisiko mdogo wa kope unaweza kumfanya mtu ahisi kuwa unaonekana zaidi kuliko uhalisia wake. Kwa kawaida, watu wengine hawawezi kutambua kwa urahisi kuwa kope la mtu linacheza.
Katika hali kali zaidi, mtikisiko unaweza kusababisha kope kufunga kwa nguvu kwa sekunde, dakika au hata saa kadhaa.
Dalili zinaweza kuongezeka na kuonekana zaidi kadiri muda unavyopita.
Ninawezaje kuzuia jicho kucheza?
Mara nyingi, hali ndogo ya jicho kucheza huisha yenyewe bila kuhitaji matibabu. Hata hivyo, kuna hatua unazoweza kuchukua ili kusaidia kupunguza hali hiyo:
- Lala kwa muda wa kutosha.
- Punguza matumizi ya kafeini na/au pombe.
- Jaribu njia za kupunguza msongo wa mawazo kama vile kufanya mazoezi, mazoezi ya kupumua au kutafakari.
- Tumia matone ya macho ya kuongeza unyevunyevu (artificial tears) ili kupunguza ukavu wa macho.
Jicho kucheza hutibiwaje?
Ikiwa jicho kucheza kutaendelea kwa wiki kadhaa, au kukusababishia ugumu wa kufungua jicho au kuona vizuri, wasiliana na daktari wa macho ili kupata ushauri kuhusu hatua zinazofuata.
Daktari anaweza kupendekeza matumizi ya dawa au mpango wa matibabu unaohusisha sindano za sumu ya botulinum (Botulinum toxin).
Sindano hizo hudungwa chini ya ngozi inayozunguka macho. Sumu hiyo husaidia kulegeza na kudhoofisha misuli iliyo chini ya ngozi, na kila awamu ya sindano inaweza kuzuia misuli kusinyaa bila hiari kwa takribani miezi mitatu.
Madhara yanayoweza kujitokeza baada ya sindano hizo ni pamoja na:
- Michubuko midogo katika maeneo yaliyodungwa sindano.
- Kushuka kwa kope kwa muda.
- Kukauka kwa macho.
- Kuona vitu viwili kwa muda.
Katika hali nadra, upasuaji unaweza kupendekezwa kwa watu wenye tatizo kali la jicho kucheza, hasa pale ambapo dalili hazidhibitiwi ipasavyo kupitia sindano za sumu ya botulinum.