Kesi mpya zamsubiri Lissu siku chache baada ya hukumu ya miaka minne jela

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, anakabiliwa na mashtaka mengine matatu baada ya kuhitimishwa kwa kesi ya hivi karibuni iliyomkuta na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela.

Lissu anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo, Novemba 19, kujibu mashtaka matatu ya madai ya kuchapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa YouTube, makosa yanayokiuka sheria ya makosa ya mtandao nchini humo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za mtandaoni za Mahakama, kesi hiyo ya makosa ya mtandao imepangwa kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Novemba 19.

Kesi hiyo inahusiana na matamshi ambayo anadaiwa kuyachapisha kupitia YouTube Aprili 3 mwaka jana. Hati ya mashtaka inaonesha kuwa shtaka la makosa ya mtandao liliwasilishwa Aprili 10, 2025, siku hiyo hiyo alipofunguliwa mashtaka ya uhaini na uchochezi kutokana na matamshi aliyoyatoa katika mkutano wa kisiasa.

Kesi hiyo ya uhaini ilihitimishwa wiki iliyopita baada ya Mahakama Kuu kumwachia huru dhidi ya shtaka la uhaini, lakini kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.

Alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela baada ya mahakama kuamua kuwa kaulimbiu yake ya kampeni ya "No Reforms, No Election" (Hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi) ilikuwa na viashiria vya uchochezi.

Wakili mmoja ameiambia BBC kuwa sheria za Tanzania zinawaruhusu waendesha mashtaka kufungua na kuendesha kesi tofauti za jinai dhidi ya mtu mmoja, hasa pale makosa yanayodaiwa kutendwa yanapotofautiana au yanapokuwa chini ya mamlaka ya ngazi tofauti za mahakama.

Hukumu na adhabu ya hivi karibuni dhidi ya Lissu zimekosolewa na mashirika ya haki za binadamu.

Shirika la Amnesty International lilielezea mwenendo wa kesi hiyo kuwa na dosari kubwa, likitaja wasiwasi kuhusu upatikanaji wa Lissu kwa mawakili wake pamoja na namna waangalizi wa kimataifa wa kesi hiyo walivyoshughulikiwa. Shirika hilo limetaka aachiwe huru mara moja.

Mashirika ya Human Rights Watch na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania nayo yameeleza wasiwasi kuhusu haki katika mwenendo wa kesi hiyo pamoja na vikwazo vipana vinavyokabili upinzani wa kisiasa nchini.

Lissu amekata rufaa kupinga hukumu ya kosa la uchochezi pamoja na adhabu aliyopewa.

Hata hivyo, kesi hiyo tofauti ya makosa ya mtandao bado inaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.