Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini wananchi wanakichoka chama tawala Afrika Kusini?
Kwa miongo mitatu chama kimoja tu kilichokuwa kinatawala siasa za Afrika Kusini. Chama kimoja tu kilichokuw ana nguvu na kutawala, chama cha ANC (African National Congress).
Kwaidi ya miaka 30, ANC imekuwa alama ya ukombozi wa Afrika Kusini, chama kilichomtoa Nelson Mandela gerezani na kuongoza nchi baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi.
Lakini matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 4, 2026, yanaonyesha jinsi chama hicho kinavyopoteza nguvu. ANC imepata asilimia 31 ya kura, ikiwa ni matokeo yake mabaya zaidi katika uchaguzi wa aina hiyo.
Ni mabadiliko makubwa kwa chama kilichowahi kupata karibu asilimia 70 ya kura katika uchaguzi mkuu na kutawala bila kutegemea vyama vingine kwa miongo mitatu. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, kilipata asilimia 40.18 na kupoteza wingi wa viti bungeni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994.
Hali ya ANC inakumbusha historia ya vyama vingine barani Afrika vilivyoongoza mapambano ya uhuru, vikachukua madaraka na baadaye kuanza kupoteza uungwaji mkono. Baadhi vimeondolewa madarakani, vingine vinaendelea kutawala huku vikikabiliwa na upinzani unaoongezeka.
Lakini kwa nini vyama vilivyokuwa na nafasi kubwa katika historia ya ukombozi wa Afrika vinapoteza mvuto? Je, ANC inakaribia kuwa chama kingine cha zamani cha ukombozi ambacho historia yake itabaki kwenye vitabu, huku nafasi yake ya kisiasa ikiendelea kufifia?
Turufu ya ukombozi inaanza kupoteza nguvu
ANC ilianzishwa mwaka 1912 ikiwa na lengo la kupigania haki za Waafrika Kusini weusi dhidi ya ubaguzi na utawala uliowatenga kisiasa na kiuchumi. Baada ya miongo kadhaa ya mapambano, ikiwemo kupigwa marufuku na viongozi wake kufungwa jela, chama hicho kilishinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994. Ushindi huo ulimuwezesha Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini. Kwa mamilioni ya wananchi, kuipigia kura ANC kulikuwa sehemu ya kuunga mkono ukurasa mpya wa historia ya nchi hiyo.
Kwa muda mrefu, historia hiyo iliifanya ANC kuwa na nguvu kubwa katika siasa za Afrika Kusini. Lakini taratibu umaarufu na kukubalika kwakwe kumeanza kuporomoka. Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa heka heka za ubaguzi wa rangi (apartheid), u chaguzi wa mwaka 2024 , uliulazimika ANC kukubali kushiriki serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kushindwa kupata wingi wa viti bungeni.
Na sasa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 2026 yameongeza ukubwa wa tatizo hilo. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEC), ANC imepata asilimia 31 ya kura, ikilinganishwa na asilimia karibu 46 katika uchaguzi kama huo wa mwaka 2021. Chama cha Democratic Alliance (DA) kimepata asilimia 25, huku uMkhonto weSizwe (MK) cha aliyekuwa rais Jacob Zuma kikikusanya asilimia 9.76. ANC bado ni chama kikubwa zaidi kitaifa, lakini tofauti yake na wapinzani imeendelea kupungua.
Miongoni mwa malalamiko yanayoelekezwa kwa ANC ni kushindwa kwa serikali za mitaa kutoa huduma muhimu. Katika maeneo mbalimbali, wananchi wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji, kukatika kwa umeme, barabara zilizoharibika, taa za barabarani zisizofanya kazi na taka kutokusanywa.
Matatizo hayo yanaambatana na ukosefu wa ajira na kashfa za ufisadi zinazohusisha viongozi wa chama na serikali. Kwa wananchi wanaokabiliana na changamoto hizo kila siku, kumbukumbu za mapambano ya miaka ya 1980 haziwezi kuchukua nafasi ya huduma wanazohitaji leo.
Sandile Mnguni, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal, anasema kupungua kwa kura za ANC kunapaswa kuwa onyo kwamba chama hicho hakiwezi tena kutegemea historia yake ya kutawala na mchango wake katika ukombozi ili kuendelea kuaminiwa.
Akizungumza na Al Jazeera, Mnguni amesema: "Ikiwa malalamiko ya msingi ya wapiga kura hayatafanyiwa kazi, chama kinaweza kukabiliwa na changamoto kubwa zaidi za uchaguzi."
Akizungumza na DW News, William Gumede, Profesa Mshiriki katika Shule ya Utawala ya Chuo Kikuu cha Witwatersrand mjini Johannesburg, anaunga mkono suala la kushindwa kwa serikali kutoa huduma muhimu kwa wananchi pamoja na rushwa ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia kupungua kwa uungwaji mkono wa ANC.
Hatima ya vyama tawala vikongwe Afrika mtegoni
ANC si chama cha kwanza Afrika na hasa katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kujikuta kikishuka na kuporomoka kwa mvuto. Nchini Zambia, United National Independence Party (UNIP) ya Kenneth Kaunda ilitawala tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1964. Kaunda alikuwa rais kwa miaka 27, lakini mwaka 1991 alishindwa na Frederick Chiluba wa Movement for Multi-Party Democracy (MMD), katika uchaguzi ulioashiria mwisho wa utawala wa chama kimoja. UNIP haikufutika, lakini haikurejea tena katika nafasi yake ya zamani ya kuwa na nguvu na kutawala.
Botswana nayo ilitoa somo jingine katika uchaguzi wa Oktoba 2024. Botswana Democratic Party (BDP), iliyokuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1966, ilipoteza utawala baada ya miaka 58. Muungano wa upinzani wa Umbrella for Democratic Change (UDC), ulioongozwa na Duma Boko, ulipata viti 36 kati ya 61, wakati BDP ilibaki na viti vinne pekee.
Japo BDP si chama chama cha ukombozi kama ANC; lakini kutawala tangu uhuru kuna maana kubwa kwa vyama tawala na vikongwe vya aina hii.
Nchini Namibia, SWAPO, chama kilichoongoza mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini kabla ya uhuru mwaka 1990, nacho kimeanza kupoteza nguvu. Katika uchaguzi wa mwaka 2019 kilipata viti 63 vya Bunge, lakini katika uchaguzi wa 2024 kilipata viti 51 kati ya 96.
Pamoja na kupungua huko, SWAPO mgombea wake, Netumbo Nandi-Ndaitwah, alishinda urais. Hivyo, tofauti na ANC, SWAPO bado ina wingi wa viti bungeni, lakini matokeo yanaonyesha kuwa ushindani wa kisiasa nchini humo umeongezeka.
Msumbiji ni mfano mwingine wa chama cha ukombozi kinachokabiliwa na upinzani unaoongezeka. FRELIMO, kilichoongoza mapambano dhidi ya ukoloni wa Ureno, kimeitawala nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1975. Katika uchaguzi wa mwaka 2024, mgombea wake Daniel Chapo alitangazwa mshindi wa urais kwa asilimia 65 ya kura baada ya uthibitisho wa mwisho wa matokeo. Hata hivyo, uchaguzi huo ulizua mgogoro mkubwa, ukikosolewa na waangalizi.
Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania ambacho kimetawala nchi hiyo kwa miaka zaidi ya 60, baada ya vyama vya TANU na ASP kuungana mwaka 1977. Katika Uchaguzi wa mwaka 2025 ulioambatana na ghasia na vifo vya watu 518, chama hicho kilipata ushindi mnono na wa kihistoria viti vya ubunge kwa zaidi ya wa 90% na urais kwa 98%.
Hata hivyo, waangalizi wa kimataifa, vyama vya upinzani na Jumuia zingine za kimataifa zimekosoa matokeo hayo huku upinzani inaoupata sasa CCM ukiongezeka tangu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete amalize muda wake mwaka 2015.
Angola na Zimbabwe nazo zinaonyesha upande mwingine wa simulizi hii. MPLA imeendelea kutawala Angola tangu uhuru mwaka 1975, lakini katika uchaguzi wa 2022 ilipata asilimia 51.17 ya kura, kutoka asilimia 61.08 mwaka 2017, huku upinzani wa UNITA ukiongeza nguvu. Zimbabwe, kwa upande mwingine, imeendelea kutawaliwa na ZANU-PF tangu uhuru mwaka 1980, licha ya upinzani wa muda mrefu kuhusu mazingira ya uchaguzi na hali ya uchumi.
Kwanini ANC na vyama vingine tawala vinaelekea shimoni?
Katika andiko lake Anguko la Vyama vya Ukombozi na Tishio la Ukoloni-Mamboleo, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya siasa Muhemsi Mwakihwelo anaangazia mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yaliyotokea baada ya vyama vya ukombozi kuingia madarakani.
Katika uchambuzi huo, Mwakihwelo anazitaja CCM, ZANU-PF na MPLA kuwa miongoni mwa vyama vinavyoendelea kutawala kwa kile anachokiita "ujanja ujanja". Anaonya kuwa kudhoofika kwa vyama vya ukombozi na misingi yake ya kutetea wananchi na kuongezeka kw arushwa na ufisadi, kunaiweka Afrika katika mazingira magumu ya kulinda rasilimali zake dhidi ya maslahi ya nje.
Nchini Afrika Kusini, hoja kuhusu ufisadi na kushindwa kwa huduma za umma inaonekana pia katika maoni ya wachambuzi kuhusu matokeo ya uchaguzi wa 2026. Ralph Mathekga, mwandishi wa kitabu The ANC's Last Decade na mchambuzi wa siasa, ameiambia Al Jazeera kuwa wananchi wametuma ujumbe mzito kwa ANC kwamba kutopatikana kwa huduma za umma na ufisadi ni vitu ambavyo haviwezi tena kuvumiliwa.
Mathekga anaeleza kuwa wapiga kura hawaioni tena ANC kama suluhisho la matatizo yao, bali wanaanza kukiona kama chanzo kikuu cha matatizo hayo. Kwa maelezo yake, uchaguzi huo ulikuwa kama kura ya maoni kuhusu uwezo wa chama hicho kuongoza na kubadilisha hali ya nchi.
Mchambuzi mwingine, Sipho Seepe, anasema matokeo hayo ni ujumbe pia kwa Rais Cyril Ramaphosa kuhusu uongozi wake. Akizungumza na Al Jazeera, Seepe amesema: "Wamekuwa wakiipa ANC nafasi, lakini sasa wanasema imetosha."
Kwa sasa, ANC haijapoteza kabisa nafasi yake ya kisiasa. Bado ni chama kikubwa zaidi kitaifa na kinaendelea kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa baada ya uchaguzi wa 2024.
Lakini matokeo ya uchaguzi wa sasa wa serikali za mitaa yanaonyesha kuwa safari yake ya kisiasa imebadilika na sababu za kufanya ipitie nyakati hizi, zimeonekana pia kwa vyama vingine vilivyotawala muda mrefu na vikaondolewa.
Changamoto za wananchi sasa si kuhusu Nelson Mandela na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, sasa wanataka ajira, maendeoe yao, hawataki kufa na njaa na kukosa huduma muhimu kama maji, umeme, huduma za afya na barabara.
Hali hii inavikuta vyama vingine ikiwemo CCM. Iwapo vitasalia kufikiria kwamba wananchi wa sasa wanavitazama vyama hivi kama vyama vya ukombozi, vitapoteza nguvu zaidi. Wananchi wa leo wanataka maji, ajira na mambo mengine hawajali hisotria na nguvu ya vyama hivi.
Kwa maneno mafupi hatima ya vyama tawala vingi Kusini mwa Afrika, inaonekana iko mikononi mwao ama kwa kusikiliza na kuhudumia wananachi, ama kwa udanganyifu kwenye sanduku la kura au kutumia nguvu ya dola kuendelea kusalia madarakani, lakini umaarufu na kukubalika kwao kunazidi kutaendelea kuhojiwa siku hadi siku.