"Ninakuacha, Tayari Nimekuacha": Ujumbe uliovunja ndoa ya Jane baada ya siku tano

Chanzo cha picha, Jane
Siku tano tu baada ya kufunga ndoa ya Kiislamu, Jane alipokea ujumbe uliogeuza maisha yake kabisa.
"Ninakuacha na tayari nimekuacha," ujumbe huo uliandikwa na mume wake mpya.
Jane, ambaye BBC imekubali kutotumia jina lake halisi, anasema alikutana na mwanaume huyo miezi 10 iliyopita kupitia tovuti ya kutafuta wachumba ya Waislamu iitwayo Muzz.
Wakati huo, Jane aliamini kuwa jina lake lilikuwa Adam na kwamba aliishi Manchester.
"Ni jambo gumu sana kwangu. Nilidhani ninaingia kwenye ndoa, lakini kumbe nilikuwa naingia katika ndoto mbaya zaidi maishani mwangu," alisema.
"Hili haliaminiki. Sielewi kwa nini watu wanaweza kufanya mambo kama haya kwa ajili ya ngono."
Kwa mujibu wa Jane, walikuwa wakiandikiana ujumbe na kuzungumza kwa njia ya video kwa muda wa miezi sita kabla ya kukubaliana kukutana ana kwa ana.
Aliiambia BBC kuwa aliamini uhusiano wao ulikuwa wa dhati na hakuwa na sababu yoyote ya kumtilia shaka mwanaume huyo alipomposa.
"Alinihakikishia kuwa ananipenda na anataka kujenga maisha pamoja nami. Ndiyo maana sikuwa na sababu ya kumtilia shaka," alisema Jane.
Hata hivyo, baadaye Jane aligundua kuwa jina halisi la Adam lilikuwa tofauti na kwamba tayari alikuwa na mke.
Mawakili wa Adam wamesema mteja wao atakanusha vikali tuhuma zote zinazotolewa na Jane.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jane, ambaye alisilimu, alisafiri hadi Brierfield, Lancashire, nchini Uingereza, Juni 2 kwa ajili ya kufunga ndoa ya Kiislamu.
Ndoa hiyo, inayojulikana kama Nikah, ni mkataba au sherehe ya ndoa ya Kiislamu inayofungwa kwa kuzingatia taratibu za Sharia.
Hata hivyo, ndoa ya aina hiyo haitambuliwi kisheria nchini Uingereza na Wales.
Jane anasema awali alipanga kufunga ndoa hiyo katika mji alikozaliwa wa Glasgow, akiwa amezungukwa na marafiki na familia yake. Hata hivyo, mwanaume huyo alipinga wazo la kufunga ndoa nchini Scotland.
Sasa Jane anasema anatambua kuwa alipaswa kuanza kuwa na mashaka wakati huo.
"Uskoti, tulitakiwa kufunga ndoa ya kisheria sambamba na ndoa ya kidini," alieleza.
"Alisema: 'Kwa nini wanahitaji kuona kitambulisho changu? Kwani ndoa si jambo rahisi tu? Hawahitaji kuona kitambulisho changu kwa ajili ya hilo.'
"Hakuwa ameridhishwa kabisa na utaratibu huo."
Kwa mujibu wa Jane, ndoa hiyo iliyofungwa Brierfield ilishuhudiwa na maimamu wawili. Baada ya hapo, wanandoa hao walikaa pamoja hotelini kwa usiku mbili.
Lakini siku tano tu baada ya kufunga ndoa, Jane alipokea taarifa kuwa ndoa yao imevunjika.

Chanzo cha picha, Jane
Jane anasema alipatwa na mshtuko mkubwa kufuatia tukio hilo, akashindwa kuelewa kilichotokea na kuitaja ndoa hiyo kuwa ndoa ya udanganyifu.
Kwa mujibu wake, tukio hilo lilikuwa aina ya unyonyaji wa kisaikolojia na kingono.
BBC inasema mwanaume huyo bado anaishi katika ndoa inayotambuliwa kisheria na kidini na mwanamke mwingine.
Katika majibu ya kina kupitia mawakili wake, mwanaume huyo ameeleza kuwa tuhuma za Jane ni sehemu ya kampeni ya muda mrefu inayolenga kumchafua.
Kwa mujibu wake, tuhuma hizo hazina ushahidi wowote na si za kweli.
Mawakili wake waliiambia BBC kuwa mwanaume huyo hakumdanganya Jane kuhusu ndoa yake ya awali kwa sababu hakuwahi kuzungumzia suala hilo kabisa.
Aidha, wanasema mwanaume huyo aliwasilisha leseni yake ya udereva wakati wa kufunga ndoa na Jane, hivyo hakuficha utambulisho wake halisi.
"Tunajutia sana kilichotokea"
BBC imeiona nakala ya cheti cha ndoa ya Kiislamu alichopewa Jane na msikiti, ambacho kinaonyesha kuwa baadhi ya taarifa ziliachwa nje na nyingine hazikuwa sahihi.
Kwa mujibu wa imamu na mufti Adil Zaman, aliyeendesha shughuli za ndoa hiyo, ndoa ilifungwa kati ya watu wazima waliokubaliana na ambao walionekana kuwa na furaha.
Hivyo, hakuliona kuwa jukumu lake kuuliza maswali ya ziada.
"Tunajutia sana hali hii," aliiambia BBC.
"Tangu mwanzo, tulijitahidi kutoa msaada unaofaa na kuwasaidia wahusika wote kwa haki. Wakati huohuo, tulipendelea kutoa maoni kuhusu mambo tunayoyafahamu moja kwa moja pekee."
Imamu huyo alikiri kuwa kulikuwa na makosa katika uhakiki wa nyaraka za utambulisho. Hata hivyo, alisema alisaidia kubaini utambulisho halisi wa mwanaume aliyefunga ndoa na Jane.
Baraza la Misikiti la Lancashire, ambalo lilisaidia kuwapatanisha wahusika baada ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, limesema watu wanaoendesha sherehe za aina hiyo wana wajibu wa kufanya uchunguzi na uhakiki unaostahili.

Shirika la New Beginnings, lililopo Oldham, Greater Manchester, husaidia watu waliosilimu.
Wawakilishi wa shirika hilo wanasema wamewahi kukutana na matukio ya watu wanaojaribu kuwadanganya wengine ndani ya jamii ya Waislamu.
"Tunaelewa kuwa kuna matapeli wa aina hiyo ndani ya jamii yetu ya Waislamu. Wanatafuta fursa za kuwadanganya watu," alisema Bilal Brown, mwanzilishi wa shirika hilo.
Kwa mujibu wake, kuharakisha uhusiano au ndoa, pamoja na kutohusisha wanafamilia wengine katika mchakato huo, kunaweza kuwa ishara muhimu za tahadhari kuwa kuna jambo lisilo sawa.
Brown anasema watu ambao wameingia katika dini ya Kiislamu hivi karibuni wanaweza kuwa katika hatari zaidi ya kudanganywa katika mazingira kama hayo.
Saima Afzal, aliyewahi kuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi na Masuala ya Uhalifu wa Lancashire, aliiambia BBC North West Tonight kuwa kutotambuliwa kisheria kwa ndoa za Kiislamu kunaweza kusababisha matatizo kwa baadhi ya wanawake.
"Tunasikia mengi kuhusu mianya ya kisheria inayohusiana na ndoa. Kwa mfano, wanaeleza kuwa hawawezi kuwawajibisha watu kwa ndoa za wake wengi kwa sababu ndoa za Kiislamu hazitambuliwi kisheria nchini Uingereza," alisema.
"Lakini tuweke suala la ndoa pembeni na tuangalie matendo yaliyofanyika hapa.
"Hapa tunaona vitendo vya udanganyifu, hila na kumtega mwanamke.
Kwa hiyo, hicho ndicho alichokosea mwanaume huyo."

Kwa mujibu wa uchambuzi huru uliowasilishwa katika Bunge la Uingereza mwaka 2018, idadi kubwa ya ndoa za Kiislamu hazikuwa zimeambatana na usajili wa ndoa za kisheria.
Hali hiyo inawanyima watu walio katika ndoa hizo ulinzi wa kisheria unaotolewa kwa wanandoa ambao ndoa zao zimetambuliwa kisheria.
Polisi Scotland wamesema hakuna kosa la jinai lililofanyika nchini humo.
Polisi wa Greater Manchester wamethibitisha kuwa wameombwa kuchunguza malalamiko yaliyotolewa na Jane.
Kwa upande wake, mtandao wa Muzz umetangaza kuwa akaunti ya mwanaume huyo imefungiwa kabisa.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Shahzod Yunus, alisema:
"Tunawataka watumiaji kuthibitisha kama wameoa au wameolewa, bila kujali kama ndoa hiyo ni ya kisheria au ya kidini.
"Ikiwa mtu ameoa au ameolewa, hatutamruhusu kutumia programu yetu wakati wa mchakato wa usajili."
Alisema kampuni hiyo hufanya uhakiki wa watumiaji kupitia anwani za barua pepe, namba za simu, vifaa wanavyotumia na picha za selfie kama sehemu ya ukaguzi wake wa kawaida.
Hata hivyo, uhakiki kupitia kitambulisho si wa lazima.
Wasifu wa watumiaji huonyesha ni hatua zipi za uhakiki walizokamilisha na zipi hawajakamilisha.
Jane anasema anataka uzoefu wake uwe funzo litakalosaidia kuwazuia wanawake wengine kuingia katika mazingira kama aliyopitia.
"Hili ni tatizo ndani ya jamii yetu," alisema.
"Ikiwa ninaweza kumsaidia mwanamke mwingine ambaye huenda akadanganywa kama mimi, hilo litakuwa mafanikio makubwa sana kwangu."
































