Manchester United inatarajia nini kutoka kwa Pochettino?

Mauricio Pochettino and Toby Alderweireld
Maelezo ya picha, Toby Alderweireld alikuwa sehemu ya kikosi cha Tottenham kilichofika fainali ya ligi ya mabingwa chini ya Mauricio Pochettino
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mauricio Pochettino anaingia Old Trafford akiwa na sifa ya kuwa kocha anayesimamia maandalizi magumu ya kabla ya msimu mpya, anayezingatia sana utimamu wa mwili wa wachezaji na mwenye msimamo usioyumba katika usimamizi wake.

Anaikuta Manchester United ikiwa hoi bin taabani 'kwenye shimo la mamba', nafasi 3 za chini kwenye mstari wa kushuka daraja. Ina alama 8 katika michezo 10, moja ya mwanzo mmbaya zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Kuinusuru, Manchester United ikathibitisha Ijumaa kuwa Pochettino atakuwa kocha wake mkuu kuanzia Novemba 18, akichukua nafasi ya Michael Carrick. Kocha huyo raia wa Argentina amesaini mkataba utakaodumu hadi Juni 2029.

Hivyo basi, wachezaji na wafanyakazi wa Manchester United wanapaswa kutarajia nini atakapoanza kazi mwishoni mwa wiki ijayo?

BBC Sport ilizungumza na Toby Alderweireld, ambaye alicheza chini ya Pochettino kwa miaka minne Tottenham, katika kipindi ambacho klabu hiyo ilifanya vizuri na kufanikiwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya England.

'Ni mtu mwenye kauli ya mwisho'

.
Maelezo ya picha, Si mashabiki wala wachezaji wa Manchester wenye furaha na matokeo ya timu yao kwa sasa. Ikishinda mchezo mmoja tu kati ya 10 ya Ligi Kuu msimu huu.

Alderweireld, mwenye umri wa miaka 37, anasema Pochettino ni kocha mwenye msimamo na asiyezunguka maneno anapotekeleza majukumu yake. Anaamini ana uwezo wa kupata kiwango bora kutoka kwa kikosi, lakini kwa sharti wachezaji wafuate mfumo na maelekezo yake.

"Ni mtu ambaye unaweza kumfikia na kuzungumza naye kwa urahisi, lakini unapaswa kufuata mpango wake. Usipofuata mpango wake, unawekwa pembeni na hakuna kurudi tena kikosini.

"Unapaswa kufikiria kuhusu timu tu. Ukiwa unajifikiria mwenyewe, basi huna nafasi tena.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Kama mchezaji unaweza kuwa na maisha yako binafsi na changamoto zako, lakini anakuambia, 'angalia, ninaelewa na unaweza kuzungumza nami kuhusu hilo, lakini timu ndiyo kipaumbele cha kwanza'. Ndivyo ilivyo. Usipofuata hilo, atakuweka pembeni.

"Anasema wazi, hapindipindi, ana mawazo na misimamo yake. Unaweza kukubaliana nayo au usikubaliane nayo, hilo ni juu yako. Lakini unapaswa kumfuata. Na nafikiri hicho ndicho Manchester United inachohitaji sasa; mtu mwenye ushawishi mkubwa, anayehakikisha kila mtu anaelekea njia mmoja na kufuata mpango. Mtu asipofanya hivyo, hakuna tatizo, anaweza kuondoka. Ni mtu mwenye kauli ya mwisho'.

"Ni mtu mwenye akili sana, anajua namna ya kuzungumza na waandishi wa habari na nini cha kusema. Atajenga mazingira ambayo wachezaji watajihisi kuwa ni sisi dhidi ya dunia nzima. Tunafanya kazi ya kujiweka fiti, tuko pamoja kama timu. Haijalishi watu wanasema nini, tufanye kazi pamoja na tupate matokeo kwa pamoja.

"Tottenham kulikuwa na benchi la ufundi, lakini yeye mwenyewe alikuwa akifuatilia kila kitu. Anajua kila kitu. Kama hayupo uwanjani, basi anatazama video na takwimu. Anajua kila kitu kuhusu wachezaji, ndani na nje ya uwanja. Wachezaji watafuatiliwa.

"Kwa namna nzuri, yeye ni mtu anayependa kudhibiti kila kitu kwa sababu anaamini mwili wako ndiyo silaha yako na unapaswa kuwa tayari kuutumia kufanya vizuri."

'Jambo la msingi ni kuwa fiti'

Mauricio Pochettino and Spurs players celebrate Champions League semi-final win
Maelezo ya picha, Pochettino alikua kiungo muhimu cha ushindi A spurs ikitoka nyuma dhidi ya Ajax na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Manchester United imekuwa ikikosolewa msimu huu kutokana na kile kinachoonekana kuwa utimamu mdogo wa mwili wa wachezaji na kutokimbia vya kutosha wakati wa mechi. Kwa sasa ipo miongoni mwa timu tano za mwisho kwenye ligi kwa umbali unaokimbwa na wachezaji wake na hata kwa idadi ya mbio za kasi kubwa.

Alderweireld anasema hitaji la kwanza kabisa la Pochettino kwa wachezaji wake ni kuwa na utimamu wa mwili na uwezo wa kukimbia.

"Kwanza kabisa, alitufanya tuwe na utimamu mkubwa wa mwili. Maandalizi ya kabla ya msimu mpya yalikuwa magumu sana.

"Namna anavyotaka timu icheze, kushambulia kwa kasi, kuwabana wapinzani, kutumia safu ya ulinzi inayokabia mbele na kucheza kwa nguvu na kasi kubwa, inahitaji ukimbie. Unapaswa kuwa na uwezo wa kukimbia mbio zikiwemo za kasi kubwa. Jambo la msingi ni kuwa fiti.

"Kila kocha anahitaji maandalizi mazuri kabla ya msimu mpya ili kupata muda wa kuwafundisha wachezaji mawazo yake na kuwaandaa kimwili. Lakini wachezaji watahisi mara moja kwamba kiwango cha mazoezi kimepanda.

"Kila siku uwanjani wakati wa mazoezi, unatakiwa kutoa asilimia 100. Hicho ndicho anachotaka na anachodai kutoka kwa wachezaji. Itakuwa tofauti kubwa kwa wachezaji na wataanza kuona matokeo ya mabadiliko hayo mara moja.

"Kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, tulikuwa tumefungwa mabao 3-0 na Ajax. Lakini wakati wa mapumziko hakutoa maelekezo ya mbinu za mchezo. Alituambia tu, 'mtatumia nguvu zenu, mtapambana, mnahitaji bao moja tu ili mrudi kwenye mchezo. Amini kwamba kila kitu kinawezekana'.

"Huo ulikuwa wakati muhimu sana kwa sababu wakati huo tulikuwa nyuma sana ya Ajax, hasa kwa namna mchezo ulivyokuwa ukienda. Lakini tulibadilisha kila kitu kupitia nguvu, kasi na kupambana katika kila pambano la kuwania mpira.

"Naikumbuka ile pasi ndefu kwenda kwa (Fernando) Llorente na namna tulivyopambana. Tulikuwa tunaulizana, 'mnaitaka hii kwa kiwango gani?'. Kuanzia hapo, mambo yalibadilika."