Lissu kutupwa gerezani kunabadilisha siasa za upinzani Tanzania?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Tanzania ina vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, lakini linapozungumziwa suala la upinzani dhidi ya Serikali, jina la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndilo linalotajwa zaidi.

Kwa miaka mingi, chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuikosoa Serikali na kupigania mabadiliko ya kisiasa. Vyama vingine vimeshindwa kujenga nguvu inayolingana nacho. Baadhi vimekuwa vikiiunga mkono Serikali katika masuala mbalimbali, huku vingine vikishindwa kujijengea ushawishi mkubwa kwa wananchi.

Katika safari hiyo, uongozi umekuwa na nafasi kubwa. Freeman Mbowe alikiongoza CHADEMA kwa takriban miaka 20 kabla ya Tundu Lissu kuchukua nafasi hiyo Januari 2025. Lissu alikuja na msimamo mkali zaidi kuhusu mabadiliko ya katiba na mfumo wa uchaguzi, akisisitiza kuwa uchaguzi haupaswi kufanyika bila mageuzi ya msingi.

Sasa Lissu amehukumiwa miaka minne jela, baada ya kukaa mahabusu kwa siku 577. Hakuwa nje ya gereza wakati wa uchaguzi mkuu wa 2025, ambao CHADEMA pia haikushiriki. Uchaguzi huo ulifuatwa na machafuko yaliyosababisha vifo vya watu 518, kwa mujibu wa ripoti rasmi.

Kutokuwepo kwake kunazua maswali kuhusu mwelekeo wa chama alichokiongoza na nafasi ya upinzani kwa ujumla. Je, CHADEMA inaweza kuendelea na siasa za Lissu bila yeye? Je, vyama vingine vinaweza kutumia nafasi hiyo kujijenga? Na je, Serikali itakabiliwa na upinzani wa aina gani katika miaka ijayo?

CHADEMA bila Lissu

.
Maelezo ya picha, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche mara baada ya hukumu ya Lissu alisema msimamo uko palepale, na ni ushindi kwa chama hicho

Lissu amekuwa mmoja wa viongozi wanaotambulika zaidi katika upinzani wa Tanzania. Msimamo wake kuhusu katiba na uchaguzi ulimpa nafasi ya kipekee ndani ya CHADEMA na kumfanya kuwa sauti muhimu katika mijadala ya kisiasa nchini Tanzania. Lakini sasa chama hicho kinapaswa kuendelea na shughuli zake bila mwenyekiti wake kuwa nje ya gereza.

Kazi hiyo inawaangukia viongozi waliobaki, akiwemo makamu mwenyekiti John Heche na katibu mkuu John Mnyika. Watalazimika kuendeleza ajenda ya chama, kukusanya wanachama na kuhakikisha kuwa CHADEMA haipotezi nafasi yake katika siasa za upinzani.

Hata hivyo, si rahisi kujua kama wanaweza kujenga ushawishi unaofanana na ule wa Lissu. Umaarufu wa kiongozi na uwezo wa chama kama taasisi ni vitu viwili tofauti. CHADEMA kinaweza kuwa na viongozi wengi, lakini bado kikakabiliwa na ugumu wa kupata mtu anayeweza kuunganisha wafuasi wake na kusimamia ajenda zake kwa namna ileile.

Katika uchaguzi wa 2020, Lissu alipata kura 1,933,271, sawa na asilimia 13.04, na kushika nafasi ya pili nyuma ya Rais wa wakati huo, John Magufuli, aliyepata kura 12,516,252. Matokeo hayo yanaonyesha nafasi aliyokuwa nayo katika ushindani wa kisiasa, ingawa kura za mgombea mmoja haziwezi kuwa kipimo pekee cha nguvu ya chama.

Kuna uwezekano pia wa Lissu kuendelea kuwa alama ya kisiasa hata akiwa gerezani. Historia ya siasa inaonyesha kuwa kufungwa kwa kiongozi hakumaanishi lazima wafuasi wake waache kumuunga mkono. Wakati mwingine hali hiyo huimarisha zaidi mshikamano wa wafuasi, hasa wanapoamini kuwa kiongozi wao ameadhibiwa kwa misimamo yake.

Upinzani utabadilisha mbinu?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kabla ya uchaguzi wa 2025, Lissu alisimamia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi bila kufanyika kwa mageuzi ya msingi. Kauli yake ya "No Reforms, No Election" iliweka CHADEMA kwenye njia tofauti na vyama vingine vilivyoamua kushiriki uchaguzi.

Msimamo huo ulizua mjadala ndani na nje ya chama kuhusu kama kususia uchaguzi ni njia sahihi ya kushinikiza mabadiliko. Kwa wanaounga mkono msimamo huo, kushiriki uchaguzi bila mazingira wanayoyaona kuwa huru na ya haki ni kuhalalisha mfumo wenye matatizo. Lakini kwa wanaoutazama kwa upande mwingine, kutoshiriki kunaweza kukinyima chama nafasi ya kushindana na kujenga ushawishi kupitia sanduku la kura.

Kutokuwepo kwa Lissu kunaweza kufanya mjadala huo kuwa mkubwa zaidi ndani ya CHADEMA. Viongozi waliobaki watalazimika kuamua kama wataendeleza msimamo wake au kutafuta njia nyingine za kushinikiza mageuzi. Huo si uamuzi mdogo, kwa sababu unaweza kugusa umoja wa chama na namna wanachama wanavyouona uongozi mpya.

Pia, nafasi iliyoachwa na CHADEMA katika uchaguzi wa 2025 inaweza kuwa fursa kwa vyama vingine vya upinzani. Hata hivyo, bado havijaonyesha kwa kiwango kikubwa uwezo wa kuchukua nafasi ya chama hicho katika kuongoza mijadala ya kitaifa. Kujenga ushawishi kunahitaji zaidi ya kukosoa Serikali; kunahitaji viongozi wanaotambulika, ajenda zinazogusa maisha ya wananchi na uwepo wa chama katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa Salim Amin, akizungumza na BBC, anasema mara nyingi kufungwa au kuuawa kwa kiongozi wa upinzani hubadilisha mwenendo wa siasa.

"Anapofungwa, ama kufa kiongozi wa upinzani, siasa haziwezi kuwa zilezile, lazima zitabadilika," anasema Amin na kuongeza Lissu kuwa ndani, siasa za CHADEMA na nchi zitabadilika na hata CCM hawatakuwa wakizungumza kwa namna ile ile ambayo wangezungumza Lissu angekuwa huru uraiani.

Kauli hiyo inaendana na hali inayokikabili CHADEMA sasa. Hata kama chama kitaamua kuendeleza msimamo wa Lissu, kitahitaji kuutafsiri katika mazingira ambayo mwenyekiti wake hawezi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kisiasa. Na kama kitaamua kubadilisha mbinu, kitahitaji kuwaeleza wanachama na wafuasi wake kwa nini kinafanya hivyo. Huo ni mtihani ambao si rahisi kuushinda kirahisi kisiasa.

Serikali na mustakabali wa mazungumzo ya kisiasa

.
Maelezo ya picha, Rais Samia ameshakutana na viongozi wa vyama vya upinzani isipokuwa CHADEMA mara kadhaa tangu uchazuzi wa mwaka 2025. CHADEMA wamejiweka kando wakitaka maridhiano yenye msuluhishi kutoka nje

Kufungwa kwa Lissu kunaibua pia hoja nyingine kuhusu uhusiano wa Serikali na upinzani. Kwa muda mrefu, madai ya mabadiliko ya katiba na mfumo wa uchaguzi yamekuwa sehemu ya mvutano kati ya pande hizo. Sasa hukumu ya mwenyekiti wa CHADEMA inaweza kufanya iwe vigumu zaidi kurejesha mazungumzo yenye kuaminiana.

Profesa Mohamed Bakari, akizungumza na gazeti la The Citizen, anaonya kuwa hukumu hiyo inaweza kuongeza wasiwasi miongoni mwa wanasiasa kuhusu mipaka ya uhuru wa kujieleza.

Mchambuzi wa siasa Suguta Mkami, aliyezungumza na The Citizen pia, anasema kuachiwa huru kwa Lissu kungeweza kuipa Serikali nafasi nzuri zaidi ya kuwarudisha wapinzani kwenye meza ya mazungumzo. Kwa mitazamo hii suala la Lissu haliishii kwenye hukumu yake pekee, bali linagusa pia kwenye uhusiani wa Serikali na vyama vya upinzani. Lakini pia uhusiano wa Serikali na wafuasi wa upinzani na hata wananachi wa kawaida wasio na vyama, wanaotazama mambo kwa jicho la kawaida na sio la kitikadi ya vyama.

Wasiwasi huo unaongezeka kutokana na mazingira yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa 2025. Licha ya CHADEMA kutoshiriki, uchaguzi huo ulifuatiwa na machafuko. Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan iliripoti vifo vya watu wasiopungua 518.

Rehema Mema, mchambuzi wa siasa aliyezungumza na BBC, anasema kutokuwepo kwa Lissu na chama chake katika uchaguzi uliopita kunaweza kuongeza joto la kisiasa kama hawatashiriki uchaguzi ujao.

"Lissu na chama chake hawakushiriki uchaguzi uliopita, tuliona uchaguzi huo ulivyokuwa. Kwa vyovyote vile, kutokuwepo kwake na chama chake kutaongeza joto la kisiasa katika uchaguzi Mkuu ujao," anasema Mema.

Sura ya upinzani kuelekea 2030

.
Maelezo ya picha, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Chama Cha AAFP Said Soud Said mara baada ya mkutano na Viongozi wa Vyama vya Siasa nchini, uliofanyika Julai 30, 2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam

Kuanzia sasa mpaka 2030 kitakuwa kipindi muhimu kwa vyama vya upinzani kujipanga upya. CHADEMA italazimika kutafuta namna ya kudumisha nguvu yake, ikiwa Lissu ataendelea kusalia jela ama kukwama kwa rufaa yake aliyoanza kuikata kupinga hukumu ya miaka minne aliyopewa. Huku vyama vingine vikikabiliwa na nafasi ya kujijenga na kuvutia wananchi wanaotaka kuona ushindani mpana zaidi wa kisiasa.

Inawezekana pia vyama hivyo vikatafuta kushirikiana katika masuala yanayovigusa kwa pamoja, hasa mabadiliko ya katiba, uchaguzi na utawala bora. Ushirikiano wa aina hiyo unaweza kuwa na nguvu zaidi kuliko kila chama kuendesha ajenda yake kivyake. Lakini historia ya upinzani nchini inaonyesha kuwa kuunganisha vyama vyenye viongozi, misimamo na maslahi tofauti si jambo rahisi.

Kwa upande wa CHADEMA, unaweza kujiuliza kinaweza kuendelea kuwa chama kinachoongoza ajenda za upinzani hata bila Lissu? Kwa vyama vingine, nao je kama vitaweza kutumia mazingira haya kujenga ushawishi wa kudumu badala ya kuonekana zaidi pale chama kikuu cha upinzani kinapokuwa na changamoto?

Wakati majibu ya maswali hayo yakisalia vichwani mwa watu, kwa upande wa Serikali, namna itakavyoshughulikia madai ya mageuzi na nafasi ya wapinzani katika siasa za nchi itakuwa na mchango mkubwa katika kuamua mazingira ya ushindani wa kisiasa. Mazungumzo yanaweza kufungua njia ya kupunguza mvutano, lakini kutokuwepo kwa maelewano kunaweza kuendeleza mgawanyiko uliopo.

Kwa hiyo, kufungwa kwa Lissu si suala linalomuhusu Lissu tu, au uongozi wa CHADEMA pekee. Kunaweza kubadili nani anayeongoza ajenda za upinzani, namna vyama vinavyoshindana na mbinu wanazotumia kushinikiza mageuzi. Pia kunaweza kuamua kama Serikali na upinzani watapata nafasi ya kujenga upya uhusiano wao.