Kwa nini vyama tawala vinazidi kupoteza uchaguzi duniani?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Katika miaka ya hivi karibuni, vyama vilivyotawala kwa muda mrefu vimejikuta vikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wapiga kura. Baadhi vimeondolewa madarakani, vingine vimepoteza wingi wa viti bungeni, huku hali ya uchumi, gharama za maisha na kutoridhishwa na uongozi vikitajwa miongoni mwa mambo yanayochangia mabadiliko hayo.

Ukiangalia matokeo ya chaguzi nyingi katika miaka miwli iliypita kuanzia 2024, utajiuliza; wapiga kura duniani wameanza kuvichoka vyama vilivyokaa madarakani kwa muda mrefu?

Hilo linaonekana kuanzia bara la Afrika, Ulaya, mpaka Amerika. Je, ni uchumi na gharama za maisha zinazozidi kuwa mzigo kwa wananchi? Je, ni kuchoshwa na viongozi wale wale, ahadi zisizotekelezwa na tuhuma za ufisadi? Au vyama vya upinzani vimeanza kutoa chaguo linalowavutia zaidi wapiga kura?

Afrika: Vyama vilivyotawala kwa miaka mingi vyaondolewa

.
Maelezo ya picha, Sanduku la kura limekuwa silaha kubwa la kuviondoa vyama tawala

Mwaka 2024 ulikuwa na matokeo muhimu ya kisiasa katika nchi kadhaa za Afrika, huku baadhi ya vyama vilivyokuwa madarakani kwa muda mrefu vikishindwa katika uchaguzi.

Nchini Botswana, chama cha Botswana Democratic Party (BDP), kilichokuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1966, kilipoteza uchaguzi wa Oktoba 30, 2024.

BDP, iliyokuwa imetawala kwa miaka 58, ilishuka hadi viti vinne katika bunge lenye viti 61 vya kuchaguliwa, kutoka viti 38 ilivyokuwa navyo katika uchaguzi uliopita.

Muungano wa upinzani wa Umbrella for Democratic Change (UDC), ukiongozwa na Duma Boko, ulishinda viti 36 na kumwezesha kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

Ghana nayo ilishuhudia mabadiliko katika uchaguzi wa Desemba 2024, ambapo chama tawala cha New Patriotic Party (NPP) kilishindwa na National Democratic Congress (NDC), kilichoongozwa na John Dramani Mahama.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mahama alirejea madarakani baada ya kushinda uchaguzi wa urais, huku chama chake kikishinda pia wingi wa viti bungeni.

Nchini Afrika Kusini, mabadiliko hayakuishia katika kuongezeka kwa nguvu za upinzani. African National Congress (ANC), chama kilichotawala tangu mwaka 1994, kilipoteza wingi wake wa viti bungeni kwa mara ya kwanza.

Katika uchaguzi wa Mei 2024, na hata wa Novemba 2026, ANC kimepoteza nguvu yake kwenye sanduku la kura. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEC), matokeo ya Novemba mwaka huu ANC imepata asilimia 31 tu ya kura, ikiwa ni matokeo yake mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu iingie madarakani mwaka 1994

Hali hiyo ilimlazimisha Rais Cyril Ramaphosa kuingia katika mazungumzo na vyama vingine, ikiwemo Democratic Alliance (DA), ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa Nordic Africa Institute, chaguzi za mwaka 2024 nchini Botswana, Ghana, Senegal na Mauritius zilisababisha mabadiliko ya viongozi, huku Afrika Kusini ikilazimisha chama kilichokuwa kikitawala kwa miaka 30 kushirikiana na vyama vingine.

Marekani na Amerika ya Kusini: Pigo kwa vyama vilivyokuwa madarakani

d

Nchini Marekani, uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Novemba 3, 2026, umekuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kisiasa mwaka huu baada ya chama cha Republican cha Rais Donald Trump kupoteza udhibiti wa mabunge yote mawili ya Congress.

Chama cha Democratic kimefanikiwa kupata udhibiti wa Seneti na Baraza la Wawakilishi, baada ya kuwashinda wagombea wa Republican katika majimbo kadhaa yaliyokuwa yakionekana kuwa ngome ya chama hicho.

Katika Seneti, Democrats wameongeza viti saba, huku katika Baraza la Wawakilishi wakipata ongezeko kubwa la viti, na hivyo kupata nafasi ya kuwa na udhibiti wa mihimili hiyo miwili ya kutunga sheria kuanzia Januari 2027.

Amerika ya Kusini nayo imeshuhudia mabadiliko ya vyama vilivyokuwa madarakani.

Nchini Panama, chama cha Democratic Revolutionary Party (PRD), kilichokuwa madarakani chini ya Rais Laurentino Cortizo, kilipata pigo kubwa katika uchaguzi wa Mei 2024.

Mgombea wake wa urais, aliyekuwa makamu wa rais José Gabriel Carrizo, alishika nafasi ya sita, huku chama hicho kikishuka kutoka viti 35 katika bunge la awali hadi viti 13 katika uchaguzi huo.

Ushindi wa urais ulikwenda kwa José Raúl Mulino wa chama cha Realizing Goals, aliyeungwa mkono na aliyekuwa rais Ricardo Martinelli.

Nchini Uruguay, uchaguzi wa mwaka 2024 pia ulisababisha mabadiliko ya serikali baada ya chama cha National Party cha Rais Luis Lacalle Pou kushindwa na muungano wa upinzani wa Broad Front.

Mgombea wa Broad Front, Yamandú Orsi, alishinda uchaguzi wa rais wa duru ya pili Novemba 24, 2024, dhidi ya Álvaro Delgado, aliyekuwa mshirika wa karibu wa rais aliyemaliza muda wake.

Broad Front pia ilipata viti 48 kati ya 99 vya Baraza la Wawakilishi na viti 16 kati ya 30 vya Seneti, na hivyo kurejea madarakani baada ya kuwa upinzani kwa miaka mitano.

Ulaya: Hata vyama vyenye historia ndefu vinashindwa

.

Katika bara la Ulaya, uchaguzi wa Uingereza wa Julai 2024 ulikuwa miongoni mwa mifano ya wazi ya mabadiliko ya kisiasa.

Chama cha Conservative, kilichokuwa madarakani kwa miaka 14, kilishindwa na Labour chini ya Keir Starmer.

Labour ilipata viti 411 kati ya 650 vya bunge, huku Conservatives wakipata viti 121 pekee, kutoka viti 365 walivyokuwa navyo katika uchaguzi wa mwaka 2019.

Matokeo hayo yalihitimisha kipindi cha utawala wa Conservative kilichohusisha mawaziri wakuu kadhaa, wakiwemo David Cameron, Theresa May, Boris Johnson, Liz Truss na Rishi Sunak.

Mabadiliko makubwa zaidi yalionekana Hungary katika uchaguzi wa Aprili 2026.

Chama cha Fidesz cha Viktor Orbán, kilichokuwa madarakani tangu mwaka 2010, kilishindwa na chama cha upinzani cha Tisza kilichoongozwa na Péter Magyar.

Tisza ilishinda viti 141 kati ya 199 vya bunge, huku Fidesz ikipata viti 52 pekee.

Magyar, ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa Fidesz kabla ya kujitenga na chama hicho, aliendesha kampeni iliyogusia masuala ya ufisadi, utawala bora, huduma za umma na uhusiano wa Hungary na Umoja wa Ulaya.

Ushindi huo ulimaliza miaka 16 ya Orbán kuwa waziri mkuu, na kuashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Hungary.

Nchini Austria, uchaguzi wa Septemba 2024 uliweka chama cha kihafidhina cha ÖVP katika nafasi ya pili nyuma ya chama cha mrengo wa kulia cha FPÖ. Hata hivyo, matokeo hayo hayakusababisha mara moja chama hicho kuondoka serikalini; baadaye ÖVP iliingia katika muungano wa serikali na SPÖ na NEOS.

Nchini Serbia, uchaguzi wa mapema wa Oktoba 25, 2026 pia ulileta pigo kwa chama kilichokuwa kikitawala chini ya Rais Aleksandar Vučić. Orodha ya wagombea iliyoungwa mkono na vuguvugu la wanafunzi ilishinda viti 140 kati ya 250 vya bunge, dhidi ya viti 103 vya chama tawala cha Serbian Progressive Party.

Vuguvugu hilo lilipata nguvu kutokana na maandamano yaliyoanza baada ya kuporomoka kwa paa la kituo cha treni katika mji wa Novi Sad mwaka 2024, tukio lililosababisha vifo vya watu 16.

Nini kinaviangusha vyama tawala?

Ingawa mazingira ya kisiasa yanatofautiana kati ya nchi hizo, kuna mambo yanayojirudia katika kampeni na matokeo ya uchaguzi.

Moja ni hali ya uchumi na gharama za maisha. Katika nchi nyingi, wananchi wanapiga kura wakati wakikabiliwa na changamoto za ajira, kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, pamoja na kushuka kwa uwezo wa kipato.

Botswana ni mfano mmoja. Kudorora kwa soko la almasi kulikuwa na athari kubwa kwa uchumi wake, huku masuala ya ajira na huduma za kijamii yakiwa sehemu ya mjadala wa uchaguzi.

Ghana nayo iliingia katika uchaguzi ikiwa na changamoto za kiuchumi zilizokuwa zimeathiri maisha ya wananchi.

Sababu nyingine ni ufisadi na uwajibikaji. Nchini Serbia, kwa mfano, maandamano yaliyotokana na ajali ya kituo cha treni yaligeuka kuwa vuguvugu pana la kudai uwajibikaji wa viongozi.

Hungary pia ilishuhudia kampeni ya upinzani iliyotilia mkazo madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Katika baadhi ya nchi, migogoro ya ndani ya chama, uongozi, sera za serikali kwa mfano za uhamiaji kw anchi kama Marekani au kuibuka kwa vyama vipya vyenye mvuto vimechangia kubadilisha ushindani wa kisiasa.

Bado vyama tawala 'vinapambana'

.
Maelezo ya picha, CCM ya Tanzania inaendelea kusalia madarakani

Pamoja na mifano hiyo, si kila nchi imefuata mkondo wa vyama tawala kuondolewa madarakani. Tanzania Chama tawala CCM, Rais Samia Suluhu Hassan ameshindwa kwa asilimia 98% ya kura katika uchaguzi wa Oktoba 2025 uliokumbwa na ghasia zilizosababisha vifo vya watu 518.

Nchini Australia, chama cha Labor chini ya Waziri Mkuu Anthony Albanese kilishinda tena uchaguzi wa Mei 2025 na kuongeza wingi wake wa viti bungeni.

Labor ilipata viti 94 kati ya 150, kutoka viti 77 katika uchaguzi uliopita, na hivyo kupata nafasi ya kuendelea kuongoza serikali.

Nchini Canada, chama cha Liberal chini ya Mark Carney kilishinda tena uchaguzi wa Aprili 2025, kikibaki madarakani licha ya changamoto za kisiasa zilizokikabili chama hicho wakati wa uongozi wa Justin Trudeau.

Kwa hiyo, je, dunia inataka mabadiliko? inawezeka lakini vyama tawala bado vinapambana na vingine kujikongoja kuendelea kusalia madarakani, kwa njia za sanduku la kura, kwa njia za kimabavu kwa kutumia dola ama kw amapinduzi ya nyuma ya mlango.