Jinsi magazeti ya Iran yanavyomkejeli Trump baada ya kushindwa kwa uchaguzi

Trump
    • Author, BBC Monitoring
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Vyombo vya habari nchini Iran vimeripoti matokeo ya uchaguzi wa Marekani huku kila chombo kikitoa mtazamo wake kuhusu matokeo hayo na athari zake kwa utawala wa Rais Donald Trump.

Baadhi ya vyombo hivyo vimeelezea matokeo hayo kuwa yamezua hali ya sintofahamu, mivutano na kurushiana lawama, hali inayohusishwa na vita dhidi ya Iran.

Magazeti yanayounga mkono msimamo wa kihafidhina yameelezea matokeo hayo kama ishara ya mabadiliko katika uongozi wa kisiasa wa Marekani na kuongezeka kwa migawanyiko ndani ya Chama cha Republican cha Rais Trump.

Kwa upande mwingine, baadhi ya vyombo hivyo vimeangazia mgawanyiko ndani ya serikali ya Marekani kuhusu namna ya kushughulikia Iran. Baadhi ya viongozi wanataka kurejeshwa kwa mazungumzo na serikali ya Iran, wengine wanataka vita viendelee, huku kundi jingine likisisitiza kuendelezwa kwa shinikizo la kiuchumi dhidi ya Tehran.

Baadhi ya magazeti ya Iran pia yameripoti kuwa Mkuu wa Utumishi wa Ikulu ya Marekani, Susie Wiles, amejiuzulu na nafasi yake kuchukuliwa na Stephen Miller.

Aidha, shinikizo dhidi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, limeongezeka huku kukiwa na maswali kuhusu nafasi yake katika vita dhidi ya Iran.

Gazeti moja pia limeangazia kuhojiwa kwa majukumu ya maafisa wakuu wa kijeshi, akiwemo Admiral Brad Cooper, kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), na Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani.

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, naye ametoa taarifa akihusisha kushuka kwa kisiasa kwa Chama cha Republican na makubaliano kuhusu Iran.

'Vita vimeanza ndani ya Ikulu ya Marekani'

Aqalka cad
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gazeti la kihafidhina la Keynes limeandika kuwa vita vimehamia ndani ya Ikulu ya Marekani, likidai kuwa maafisa wa serikali wanaendelea kujiuzulu mmoja baada ya mwingine.

Gazeti hilo limeelezea hali iliyopo ndani ya Ikulu kuwa imegubikwa na mvutano mkubwa na hasira.

Limehusisha hali hiyo na kile lilichokiita pigo kubwa la kihistoria ambalo Iran imempiga Rais Donald Trump na Chama cha Republican.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, wafuasi wa msimamo mkali wanaamini kuwa vita dhidi ya Iran vilichangia kushindwa kwa Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa urais.

Gazeti hilo pia limeangazia mfululizo wa mabadiliko na kujiuzulu kwa baadhi ya maafisa katika Wizara ya Sheria ya Marekani, huku likitaja kupewa majukumu makubwa zaidi kwa Stephen Miller kama hatua muhimu katika mabadiliko hayo.

Limesema Miller, ambaye awali alikuwa akiunga mkono vikali vita dhidi ya Iran, sasa anaripotiwa kuwa miongoni mwa wanaoshinikiza kusitishwa kwa mzozo huo.

'Trump ameibua fursa ya mabadiliko ya uongozi nchini Marekani'

Gazeti la Jam-e-Jam, linalohusishwa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya Iran, limechapisha kichwa cha habari kinachosomeka, "Ikulu ya Marekani yakumbwa na msukosuko kutokana na mgogoro wa ndani."

Nalo gazeti la kihafidhina la Jawan limeandika, "Trump apanga kubadilisha mfumo wa madaraka nchini Marekani!"

Gazeti hilo limehusisha hatua hiyo na matamshi ya hivi karibuni ya maafisa wa Marekani kuhusu uwezekano wa kubadilisha mfumo wa uongozi nchini Iran, likiyaelezea kama majibu ya Washington.

Jawan pia limerejelea kauli zinazohusishwa na Trump, akitambua uwezekano wa kufanya mabadiliko katika timu yake baada ya chama chake kushindwa katika uchaguzi.

Gazeti jingine lenye msimamo mkali, Watan-e-Emroz, limechambua msukosuko wa kisiasa unaoendelea Washington, ambako wanachama wa Republican wanaopinga vita na wale wanaoviunga mkono wanashindana kushawishi mkakati wa Trump.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kumekuwa mojawapo ya vipaumbele vikuu vya serikali ya Marekani.

Limesema hatua hiyo inalenga kupunguza bei ya mafuta na kurejesha uungwaji mkono wa wananchi kwa serikali.

Mgawanyiko ndani ya kambi ya Trump

Kooxda Trump

Gazeti la kihafidhina la Agah limechapisha kichwa cha habari kinachosomeka, "Njia za wenye hatia zimekuwa tupu."

Gazeti hilo limesema matokeo ya vita na kushindwa katika uchaguzi sasa yanaanza kujidhihirisha.

Kwa upande wake, gazeti la Arman-e-Milli, linalounga mkono mageuzi, limeripoti kile lilichokiita kutokubaliana ndani ya Ikulu ya Marekani.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, gharama za kisiasa na kiuchumi za mgogoro wa Iran zimegawanya kambi ya Trump.

Limesema kuna makundi matatu makuu ndani ya serikali yenye mitazamo tofauti kuhusu namna ya kushughulikia hali hiyo.

Kundi la kwanza linaamini kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz unapaswa kufunguliwa tena kupitia mazungumzo na utatuzi wa mzozo.

Kundi la pili linaunga mkono kurejea kwa operesheni za kijeshi, huku kundi la tatu likitaka kuendelezwa kwa shinikizo la kiuchumi na vikwazo dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, tofauti hizo za misimamo zinaonyesha changamoto zinazoikabili serikali ya Trump katika kuandaa mkakati wake wa kukabiliana na Iran.

Trump bado hajajifunza kutokana na makosa yake

Gazeti la kihafidhina la Sazandegi limeibua swali, "Nani atafutwa kazi?"

Gazeti hilo limeelezea vita dhidi ya Iran kama mgogoro wa kisiasa ambao umeitumbukiza Marekani katika hali ya sintofahamu.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mzozo huo unaweza kuhatarisha mustakabali wa kisiasa wa maafisa kadhaa waandamizi, wakiwemo Pete Hegseth na JD Vance, pamoja na wengine wanaotarajiwa kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2028.

Gazeti la Shargh nalo limeandika kuwa majukumu mapya aliyopewa Stephen Miller wakati kukiwa na kutokubaliana kuhusu sera ya Iran yameibua maswali kuhusu uwezekano wa kupungua kwa ushawishi wa Vance ndani ya serikali.

Baada ya Chama cha Republican kupata pigo katika uchaguzi wa katikati ya muhula, Trump alimpa Miller mamlaka na majukumu zaidi ya kusimamia baadhi ya mipango muhimu ya serikali yake.

Hatua hiyo imechukuliwa licha ya wapiga kura kuonyesha kutounga mkono sera hizo, kwa mujibu wa gazeti la Tehran Times, linalochapishwa kwa lugha ya Kiingereza na kuhusishwa na Shirika la Kiislamu la Uenezi la serikali ya Iran.

Gazeti hilo limemwelezea Miller kama mwanasiasa mwenye misimamo mikali, likisema sera zake zimechangia kuwafanya wapiga kura wengi kujitenga na serikali.

Kwa mujibu wa Tehran Times, kumpa Miller nafasi hiyo yenye mamlaka makubwa kunaonyesha kuwa Trump huenda bado hajajifunza kutokana na ujumbe uliotolewa na wapiga kura kupitia matokeo ya uchaguzi.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid